PUMZI YA MOTO: Zamani mpira ulichezwa vizuri ila sasa unachezwa vizuri zaidi

Muktasari:
- Video hiyo ni ya mechi ya raundi ya pili ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1975, kati ya Enugu Rangers ya Nigeria na Yanga ya Tanzania.
KUNA video inazunguka mitandaoni ambayo ilianzia kwa mwandishi mkongwe, Muhidin Issa Mchuzi, aliyeposti kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kupitia mfululizo wa makala zake za kumbukumbu mbalimbali za kihistoria.
Video hiyo ni ya mechi ya raundi ya pili ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1975, kati ya Enugu Rangers ya Nigeria na Yanga ya Tanzania.
Mechi hii ilifanyika Mei 10, 1975 kwenye Uwanja wa Surulele jijiji Lagos nchini Nigeria na iliisha kwa sare tasa yaani 0-0.
KIWANGO CHA CHINI SANA
Ukiwasikiliza wazee wetu walioshuhudia mpira wa zamani utadhani wakati huo 'mbungi' lilipigwa zaidi ya play station.
Lakini video hii imeonyesha uhalisia wa mpira wa wakati huo.
Hakuna mipango zaidi ya kuupiga mpira uende mbele. Kila anayeupata mpira kazi yake ni kuupiga uende mbele kwa kubutua.

Kwa kifupi mechi ile ilichezwa kama mpira wa mtaani unaochezwa na watu wasio na kocha.
Hii ni tofauti kabisa na mpira wa sasa ambao unachezwa kwa pasi za uhakika na mipango ya hali ya juu.
Video hii inamaliza kabisa ule ubishi wa kwamba zamani mpira ulikuwa mkubwa kuliko sasa, hapana hata kidogo.
Ni kwamba tu wazee husifia mambo ya nyakati zao kwa kuyataja kwa ukubwa kuliko kila kitu cha sasa.
Hii bila shaka inatokana na ukweli kwamba mambo hayo huwakumbusha nyakati walizopitia na kuwapa hisia kali sana.
Lakini kiufundi mpira wa sasa unachezwa vizuri zaidi kuliko zamani.

Mpira wa sasa unahusisha vitu vingi vinavyoufanya uwe bora kuliko wakati ule.
Mpira wa sasa unatumia makocha wasomi wa madaraja ya juu ya ukocha kuliko wakati ule.
Mpira wa sasa unatumia sayansi ya hali ya juu kuliko wakati ule.
Mpira wa sasa una mifumo bora zaidi na iliyoendelezwa kuliko wakati ule.
Mpira wa sasa uko juu sana.
OKALA WA MWANRI
Kama unaikumbuka video moja ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, akisema yeye alikuwa mchezaji mzuri wa mpira na alikuwa anapiga chenga hadi anaukalia mpira.
Katika video hiyo, Mwanri alimtaja mtu wa kuitwa Emmanuel Okala.

Sasa kwenye video ile ya mechi ya Enugu Rangers na Yanga, Okala ndiyo alikuwa golini kwa Enugu Rangers.
Okala alikuwa kipa mkubwa Afrika wakati ule akiidakia Enugu Rangers na timu ya taifa ya Nigeria.
SHERIA YA BAO LA UGENINI
Baada ya kuukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CAF mwaka 2022 kwa sheria ya bao la ugenini, Yanga waliilalamikia sana sheria ile.
Lakini hata hivyo, sheria hiyo haikuanza kuwaumiza kwenye hiyo fainali.
Sheria hii ilianza kuwatesa Yanga katika mechi hii.
Video ya Ankali Michuzi ni ya mechi ya mkondo wa kwanza.
Lakini mechi ya mkondo wa pili ya Dar es Salaam ndiyo iliyozua balaa.
Baada ya sare ya 0-0 ya ugenini, Yanga ilitarajiwa kushinda nyumbani na kuingia robo fainali.
Lakini haikuwa hivyo, mechi iliisha kwa sare ya 1-1 na Yanga kutolewa kwa sheria ya bao la ugenini.

MKASA WA MECHI
Hii ni mechi iliyosababisha mpasuko mkubwa wa Yanga wa mwaka 1976 na kuigawa klabu hiyo vipande viwili.
Mwaka 1974 Yanga ilishinda ubingwa wa ligi na kupata tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika 1975.
Ratiba ilipotoka, Yanga walitakiwa kuanzia raundi ya pili, na mpinzani wao akawa Enugu Rangers.
Kujiandaa na mechi hii Yanga ikapanga ikaweke kambi nchini Kenya, kwa mwaliko wa chama cha soka cha nchi hiyo.
Kocha wa Yanga, Tambwe Leya, katika kikosi chake akamkata nyota mkubwa zaidi wa klabu hiyo, Sunday Manara, kwenye safari.
Sababu ni utovu wa nidhamu wa nyota huyo ambaye aliamua kujipa mapumziko ya wiki moja bila ruhusa ya viongozi wake.
Aliomba ruhusa akakataliwa hivyo akaamua kujipa mwenyewe mapumziko, ndipo kocha akachukua hatua, kwanza akimshusha kufanya mazoezi na timu za vijana kisha kumuacha kwenye safari.
Na baada ya Yanga kutolewa, kocha Tambwe Leya aliwalaumu wachezaji kwamba wameihujumu timu kwa kutojituma.
Mgogoro ukawa mkubwa hadi kufikia wachezaji kufukuzwa na kusababisha mpasuko mkubwa sana ulioigawa Yanga na kuzaliwa timu mpya ya Pan African.