Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna sisi wengine halafu kuna Morocco katika dunia yao

Muktasari:

  • Sisi tunaendelea na ligi yetu kwa sababu Taifa Stars haipo kule kwa Wazungu. Hapo hapo hakuna mchezaji yeyote anayecheza katika ligi yetu ambaye ameitwa na timu yake ya taifa kucheza Kombe la Dunia kule majuu.

JINSI dunia inavyotuachanisha. Wakati mwingine inashangaza. Wakati huu Kombe la Dunia likiendelea kule Marekani, Canada na Mexico Ligi Kuu Bara inaendelea. Ligi Kuu Morocco pia inaendelea. Hata hivyo, zote zinaendelea kwa sababu tofauti.

Sisi tunaendelea na ligi yetu kwa sababu Taifa Stars haipo kule kwa Wazungu. Hapo hapo hakuna mchezaji yeyote anayecheza katika ligi yetu ambaye ameitwa na timu yake ya taifa kucheza Kombe la Dunia kule majuu.

Wengi mataifa yao hayashiriki na wachache ambao mataifa yao yanashiriki kama vile Pacome Zouzoua na Ivory Coast yake hajaitwa katika kikosi cha chao. Hakukuwa na haja ya kusimamisha ligi kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Ku-le Morocco hadithi ni tofauti. Hawajasimamisha ligi kwa sababu wachezaji wawili tu wa ndani ndio wameitwa katika kikosi chao kilichowatesa Wabrazili kisha Scotland katika kundi C. Unasimamishaje ligi kwa sababu ya wachezaji wawili tu?

Wachezaji wenyewe wamekwenda katika Kombe la Dunia wakiwa kama makipa wa akiba. Ahmed Reda Tagnouti anayecheza AF FAR na Munir El Jakoui anayecheza RS Berkane. Basi. Wasingeweza kusimamisha ligi yao kwa sababu ya wachezaji hawa.

Kitazame kikosi chao kamili: Yassine Bounou (Al Hilal), Munir El Kajoui (RS Berkane), Ahmed Reda Tagnaouti (AS FAR), Achraf Hakimi (Paris Saint-Germain), Noussair Mazraoui (Manchester United), Nayef Aguerd (Marseille), Chadi Riad (Crystal Palace), Issa Diop (Fulham), Zakaria El Ouahdi (Genk), Anass Salah-Eddine (PSV Eindhoven), Youssef Belammari (Al Ahly), Redouane Halhal (KV Mechelen), Sofyan Amrabat (Real Betis), Azzedine Ounahi (Girona), Bilal El Khannouss (Stuttgart), Ismael Saibari (PSV Eindhoven), Neil El Aynaoui (AS Roma), Ayyoub Bouaddi (Lille), Samir El Mourabet (Strasbourg), Brahim Díaz (Real Madrid), Soufiane Rahimi (Al Ain), Ayoub El Kaabi (Olympiacos), Abdessamad Ezzalzouli (Real Betis), Chemsdine Talbi (Sunderland), Yassine Gessime (Strasbourg), Ayoube Amaimouni (Eintracht Frankfurt).

Ta zama timu ambazo wanacheza ndio utagundua pengo lililopo baina yao na sisi. Na katika hali ya kawaida wachezaji wa Wydad Casablanca, Raja na FAR Rabat wanaweza kutengeneza timu yao na wakashinda vizuri tu pambano dhidi ya Taifa Stars.

 Licha ya kwamba mastaa wao tuliwachachafya katika pambano la Afcon palepale Morocco haiondoi ukweli kwamba Wamorocco wametuacha mbali. Sio tu kwamba wametuacha sisi mbali, lakini pia wamewaacha Waafrika wengine mbali.

Kuna faida nyingine ambayo hata hivyo Wamorocco wanayo na hakuna tunachoweza kufanya katika hilo. Wana wachezaji wengi wakubwa ambao wamezaliwa Ulaya. Hawa kina Amrabat, Hakimi, Diaz wote wamezaliwa hospitali za Ulaya. Babu zao walizamia miaka mingi Ulaya na hakuna tunachoweza kufanya katika hilo.

Wakati fulani tulikuwa tunajidanganya kwamba wakati ulikuwa umefika tuwaite nyumbani watoto wa Kitanzania ambao wamezaliwa Ulaya. Hata hivyo, tuna bahati mbaya kwamba hata watoto wetu waliozaliwa kule hawachezi soka la kiwango cha juu.

Ni Yusuf Poulsen tu ndiye ambaye amezaliwa na baba wa Kitanzania kule Ulaya na amecheza mpira katika kiwango cha juu. Rafiki zetu wahisani Denmark hawakutaka kutuachia. Wakaamua awe wao moja kwa moja. Wengine ni wachezaji wa kawaida tu ambao hawafiki hata nusu ya mafanikio ya Mbwana Samatta aliyeondoka Mbagala kwenda kucheza Ulaya.

Jambo la pili ndilo ambalo tunaweza kufanya, lakini halifanyiki ni hili hapa la kupeleka wachezaji nje. Kuna waliozaliwa Morocco, lakini wakaenda nje. Kuna ambao wanacheza hata ndani ya Bara la Afrika kama ulivyoona hapo juu. Sisi hatupeleki wachezaji Ulaya wala ndani ya Afrika. Idadi ni ndogo sana na ni wazi kwamba hatuwezi kushindana katika kiwango cha juu.

Tumewaachia Senegal wapambane na watu kama hawa kwa sababu na wenyewe wamewekeza zaidi wachezaji wao kucheza nje. Sisi tumewekeza wachezaji wetu kucheza ndani. Miaka michache ijayo utashangaa kuona wale vijana wa nchi tulizocheza nazo michuano ya mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 wakitamba Ulaya wakati sisi wa kwetu watakuwa Pamba ya Mwanza na Mtibwa. Huu ni ukweli mchungu.

Wakati bado tukijadili namna ambavyo ligi ya Morocco imetoa wachezaji wawili tu katika kikosi cha Morocco kinachocheza Kombe la Dunia sio mbaya tukijikumbusha namna ambavyo wachezaji wetu waliokwenda kule wakitokea katika ligi yetu walionekana kufeli. Kina Clatous Chotta Chama, Tuisila Kisinda na Aziz Ki.

Mchezaji kutoka ligi yetu ambaye aliimudu ligi ya Morocco ni Simon Msuva. Kuna kitu kinatafakarisha katika hili. Kwamba ligi ambayo wachezaji wetu wanaishindwa wenyewe bado haina ubavu sana wa kuwapa Wamorocco timu ya taifa. Wanakuja wanaume wengine kutoka Ulaya.

Hapo hapo unawaza kwamba kuna timu ambayo imecheza fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, RS Berkane. Imejaza wachezaji kibao wa Morocco lakini bado hawana nafasi katika kikosi cha timu yao ya taifa. Ni mafundi haswa. Tuliwaona katika mechi mbili walizocheza na Mamelodi Sundowns. Hata hivyo maisha ni magumu kwao kupata nafasi timu ya taifa.

Hili ndio pengo lililopo baina yao na sisi. Narudia, sio sisi tu, bali na Waafrika wengine. Wakati fulani ilionekana kama vile mataifa ya watu weusi huku Afrika yangeweza kuweka rekodi ya kuwa timu za kwanza kucheza nusu fainali za Kombe la Dunia. Hata hivyo, Morocco wameweka rekodi hiyo kule Qatar. Na ninavyoona hata mwaka huu wanaweza kufika hatua hiyo au kwenda mbali zaidi. Kwa namna wanavyocheza wanaweza hata kufika fainali. Kama wakifika fainali na wakatwaa taji lenyewe nani atashangaa?