Pipino: Kutoka Magnet, KMC hadi Stars
Muktasari:
- Kiungo huyo wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi, kukaba kwa akili na kutuliza mchezo katikati ya uwanja, alionyesha ubora mkubwa na kuitwa kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.
KATI ya majina 10 ya vijana yaliyochipukia kwa kasi Ligi Kuu Bara kwa kuonyesha kiwango bora msimu ulioisha hivi karibuni, jina la Ahmed Bakari ‘Pipino’ linazidi kuwa gumzo.
Kiungo huyo wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi, kukaba kwa akili na kutuliza mchezo katikati ya uwanja, alionyesha ubora mkubwa na kuitwa kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.
ALIKOANZIA, ATUA KMC
Maisha yake ya soka yalianza kwenye akademi ya Magnet Youth alikopata mafunzo ya soka kwa takribani miaka minane hadi kupata nafasi ya kujiunga na akademi ya Celta Vigo ya Hispania mwaka 2022, kabla ya kurejea nchini na dirisha dogo msimu uliomalizika, KMC ikamsajili kinda huyo na kuanza kuchezeshwa hadi kikosi cha kwanza akionyesha ubora wa kutuliza presha ya mchezo.
Mechi ya kwanza aliyoanza kutambulishwa kikosini hapo ilikuwa dhidi ya Azam FC, licha ya Kino Boys kupoteza kwa mabao 2-0 lakini alionyesha kiwango kikubwa akimaliza dakika zote 90, huku ya pili dhidi Singida Black Stars ambayo KMC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na alionyesha uwezo mkubwa wa kukaba na kuipandisha timu.
AITWA STARS
Kutokana na kiwango chake bora akiwa KMC, alimvutia Kocha wa Stars Hemed Suleiman ‘Morocco’ kumjumuisha kwenye kikosi kilichocheza mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Kwenye mashindano hayo, kiungo huyo (20) alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo kati ya Tanzania iliyoondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Eswatini na kuzidi kukuza jina lake baada ya Watanzania kuushuhudia mchezo huo kuona uwezo wake.
KUPITA NJIA YA HAWA
Ipo baadhi ya mifano ya nyota wa Tanzania waliowahi kuvuma na wakaendeleza ubora huo hadi leo wakiwa ndiyo nyota tegemeo kwenye vikosi vyao na kuchezea timu kubwa wakiwamo beki Dickson Job na Feisal Salum ‘Feitoto’.
Job aliyeangaza akiwa na Mtibwa Sugar kabla ya kusajiliwa na Yanga, uchezaji wake wa utulivu, usomaji wa mchezo na uwezo wa kujenga mashambulizi kutoka nyuma, umemfanya kuwa tegemeo la muda mrefu kwa Yanga na Taifa Stars.
Kwa upande wa Feitoto anayesifika kwa uwezo wa kupandisha mashambulizi na kufunga, ni mmoja wa nyota wazawa walioendelea kuwa midomoni mwa wadau wa soka nchini.
Hivyo, uwezo alioanza kuuonyesha Pipino ni wazi huenda akapita njia za baadhi ya nyota hao ambao hadi sasa wamekuwa mhimili mkubwa kwenye timu zao.
SIMBA, YANGA
Kama ataendelea kuonyesha kiwango bora msimu ujao, huenda asiendelee kusalia KMC kutokana na uhitaji wa nyota wenye uwezo wa aina yake.
Yanga, kwa takribani misimu mfululizo, imekuwa ikipambana kumpata mbadala wa kiungo Mganda, Khalid Aucho ambaye akikosekana, timu inaonekana kuyumba.
Vivyo hivyo kwa Simba, eneo la kiungo lilikuwa chini ya Yusuph Kagoma na Fabrice Ngoma ambao walikuwa wakicheza mara kwa mara na wakikosekana, kuna Augustine Okejepha, Debora Mavambo na Mzamiru Yassin ambaye alikuwa majeruhi.
Kwa aina ya uchezaji na utulivu Pipino, timu kubwa kama Simba ambayo inaendelea kujiimarisha huenda akala shavu na kwenda kushindana na nyota watakaokuwepo.
NAFASI STARS
Kikosi cha Stars kwenye eneo la kiungo mkabaji wapo nyota wanaocheza soka la ushindani – Novatus Miroshi (Goztepe, Uturuki), Himid Mao (Ghazl El Mahalla, Misri), Kagoma (Simba), Mudathir Yahya (Yanga) – ambao wamekuwa wakicheza eneo hilo na kitu kizuri kwa kocha Morocco, amekuwa mstari wa mbele kuamini vipaji vya wachezaji wachanga.
Kitendo cha Pipino kupewa nafasi kwenye mashindano ya COSAFA na kuitendea haki ni wazi kinaweza kuwa faida kwake huko mbele katika mashindano mengine ya CHAN na AFCON.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia kiwango chake, Pipino alisema ni faraja kwake kupata nafasi ya kucheza kwenye timu kubwa kama KMC, akimtaja Khalid Aucho wa Yanga kuwa ndiye mchezaji anayemtazama kwenye nafasi anayocheza.
“Aucho ni mchezaji mkubwa na amefanya mambo makubwa kwenye ligi yetu. Nitajitahidi nizidi kupambana ili kufikia malengo yangu na ni mchezaji ninayemtazama vitu anavyofanya na najifunza kutoka kwake.”