Picha ilivyo kwa mzunguko wa kwanza TPL

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Ligi Kuu Bara tayari imeanza tangu wiki iliyopita huku michezo ya awali ikitamatika keshokutwa wakati bingwa mtetezi Yanga ikiikaribisha KMC Uwanja wa Azam Complex na kesho Singida Fountain Gate ikicheza na Tanzania Prisons Uwanja wa Liti.

Vita imeanza kuwa kali kwa kila timu kusaka alama tatu kwenye michezo ya awali na wale waliokuwa na siku njema basi waliambulia alama tatu bila kujali wapo uwanja wa ugenini.

Hata hivyo tayari kengele ya hatari imeanza kulia kwa timu ambazo zimeshacheza kwa kuangalia michezo yao ya awali namna walivyokuwa na kikosi cha kubapamba na Ligi Kuu katika kusaka ubingwa.

Ihefu FC rekodi mbaya
Tangu ipande kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2020/21 timu hiyo haijawahi kushinda mchezo wake wa kwanza na ikumbukwe msimu wa kwanza kupanda haikudumu kwani ilishuk tena daraja na msimu uliopita ilianza vibaya ligi hadi ilipofanya maboresho ya kikosi kwenye dirisha la usajili la wachezaji Januari.

Msimu wa mwaka 2020/21 ilianzia nyumbani dhidi ya Simba na kuchapwa mabao 2-0 na msimu uliopita ilichapwa bao 1-0 na Ruvu Shooting na msimu huu imepoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Geita.

Tabora United mambo magumu awali ilikuwa inajulikana kama Kitayosce ambayo ndio kwanza imepanda Ligi Kuu lakini mambo yao yanaonekana sio mazuri, kwanza kocha wao hakutakiwa kusimama kwenye benchi kwa kutokizi vigezo katika mchezo dhidi ya Azam kama ilivyoelezwa na mamlaka husika.

Pia ilifungiwa kusajili hadi pale itakapowalipa wachezaji wake wanaowadai na hii ni mara ya pili ndani ya miezi miwili baada ya hapo awali kufungiwa ikiwa inadaiwa Sh17 milioni na aliyekuwa kocha wao, Mostafa Soliman.

Kinachofanyika kwa uongozi wa Tabora United ni kutaka kuishi maisha kama yale waliyoyazoea wakiwa Ligi ya Championship kwa kutafuta njia ya mkato na wasipokuwa makini watashuka daraja.

JKT Tanzania safi
Ikirejea kwa mara nyingine Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa mwaka 2020/21 wakati timu nne zikishuka ikiwemo Mwadui, Ihefu na Gwambina lakini imeanza vyema kwenye ligi msimu huu.

Pamoja na ushindi huo kocha mkuu, Malale Hamsini amesema bado kuna kazi ya ziada anatakiwa kuifanya kutokana na ushindani aliouona na namna walivyocheza sababu timu zimejipanga na ushindani ni mkubwa.

Kaze balaa zito
Namungo imeanza kwa kichapo nyumbani chini ya Cedric Kaze. Timu hiyo haijawahi kuvumilia makocha na imekuwa na utaratibu wa kubadilisha makocha kila msimu. Msimu uliopita ilianza na Hemed Suleiman 'Morocco' kisha Hanoor Janza na baadaye Denis Kitambi.

Namungo msimu wake wa kwanza Ligi Kuu 2019/20 ilimaliza nafasi ya nne na kushiriki kimataifa, msimu uliofuata ikamaliza nafasi ya tisa, msimu wa 2021/22 ikamaliza nafasi ya tano kama ilivyo msimu uliopita.

Namungo huu ndio mchezo wa kwanza kupoteza ukiwa ufunguzi wa ligi kwani msimu wa kwanza iliichapa Ndnada 2-1, msimu uliofuata ikaichapa Coastal Union bao 1-1 na msimu uliopita ikatoka sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar.

Maguli afungua akaunti
Mshambuliaji wa Geita Gold, Elias Maguli msimu uliopita ndiye alikuwa kinara wa mabao mengi (5) kwenye kikosi na msimu huu amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao, akifanya hivyo wakati wakiichapa Ihefu bao 1-0.

Hii ni ishara nzuri kwa Geita kufungua ukurasa wa alama tatu kwenye ligi tena ikiwa ugenini katika Uwanja (Highland Estates), ambao haijawahi kupata ushindi dhidi ya Ihefu FC.

Dodoma Jiji kicheko
Ulikuwa msimu mzuri kwa walima zabibu hao katika Uwanja wa Jamuhuri, Dodoma ilipoichapa Coastal Union mabao 2-1 licha ya wageni kutangulia kupata bao kupitia Haji Ugando lakini Meshack Abraha na bao la kujifunga la kipa wa Coastal Union, Justin Ndikumana yaliwasaidia wenyeji kuaambulia alama tatu.

Bila shaka kutakuwa na mengi mazuri ikiwa itakuwa na ari ile ambayo imeonyeshwa katika mchezo wa kwanza wa miamba hiyo ya Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Coastal beki tatizo
Ukiangalia mchezo wa kwanza dhidi ya Dodoma, safu ya ulinzi ya Coastal Union ilikuwa inakabia macho na kuruhusu wapinzani wao kila wakati kuingia kirahisi eneo lao la hatari.

Robertinho mmh!
Kocha wa Simba Roberto Oliveira Goncalves do Carmo 'Robertinho' hali ya kikosi chake bado hakiwapi amani wapenzi wa timu hiyo kwa namna soka lake lilivyo tangu michezo ile ya Ngao ya Jamii.

Robertinho asipokuwa makini mwaka huu anaweza asimalize ndani ya kikosi hicho chenye hamu kubwa ya mafanikion hasa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu walioukosa kwa misimu miwili mfululizo.

Licha ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar lakini lile soka ambalo Simba ilikuwa ikicheza kwa misimu kadhaa ya nyuma bado halionekani huku mashabiki wakiwa wenye hofu na mwenendo wa timu yao.

Aibu mapema
Maajabu yalianza katika mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Kitayosce ambao haukumalizika, kila mmoja akimtupia lawama mwenzake. Mmoja wa viongozi wa Kitayosce anasema kilichotokea kilikuwa nje ya uwezo wao.

"Tulikamilisha taratibu zote na kuwalipia wachezaji ili wapewe leseni lakini mwisho wa siku wengi taratibu zao hazikukamilika ndio maana walicheza wachezaji nane."

Hii ni aibu kwenye soka letu, viongozi wa timu na mamlaka inayosimamia soka lazima wawe wanayatazama mambo haya kwa upana ili kuepuka vitu vinavyoweza kuweka taswira mbaya kwenye mpira wetu.

Yanga kuendeleza ilipoishia
Kikubwa wanachokitaka mashabiki wa Yanga ni kuona kocha wao, Miguel Gamondi anafanya zaidi ya mtangulizi wake, Nassredine Nabi tofauti na hapo mambo yatamwendea vibaya.

Tayari amepoteza Ngao ya Jamii ambayo kwa misimu miwili, Nabi alikuwa anaimiliki sambamba na kunyakua makombe ya Ligi Kuu na kufanya vyema kimatafa.

Kagera Sugar
Walima Miwa hao wameanza vibaya msimu wao wa Ligi Kuu kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC ambao ni wageni wa ligi hiyo huku wapenzi wa soka Mkoa wa Kigoma ukiwa wenye furaha kubwa.

Jambo kubwa na lenye furaha kwa wanasoka wa Kigoma lakini huzuni kubwa kwa Kagera timu kongwe kwa kuanza vibaya msimu chini ya kocha, Mecky Mexime mwenye uoefu mkubwa katika soka la Tanzania.

Mashujaa ilipanda Ligi Kuu kupitia hatua ya mtoano dhidi ya Mbeya City iliyokuwa Ligi Kuu lakini ikashinda nyumbani mabao 3-1 kisha ikashinda tena ugenini bao 1-0.

Timu hiyo ipo chini ya Abdallah Mohamed 'Bares' aliyetoka kuinusuru Tanzania Prisons na sasa ameanza vyema na Mashujaa kwenye mchezo wa Ligi Kuu.