Pacha matata WPL

Pacha matata WPL

Muktasari:

  • RAIS wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu hakukosea alipomtaka Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul kushughulikia soka la wanawake.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu hakukosea alipomtaka Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul kushughulikia soka la wanawake.

Gekul ametakiwa kuwasaidia wanawake katika michezo kwani wanafanya vizuri lakini hawapewi sifa inayostahili tofauti na wanaume.

Kauli hiyo ya Rais Samia wala haina chembe ya uongo hata kidogo, kwani huku kwenye Ligi ya Wanawake kuna wachezaji wana balaa na wanastahili kupewa sifa kubwa kwa jinsi wanavyozibeba timu zao.

Hawa ni baadhi ya wachezaji wanaotengeneza pacha matata zinazowapa wakati mgumu timu pinzani kwenye Ligi Kuu ya Wanawake inayoongozwa na Simba Queens yenye pointi 38, ikifuatiwa na Yanga Princess iliyo na pointi 38 wakati JKT Queens ikiwa nafasi ya tatu na pointi 36.


Opah, Shelda- Simba

Wachezaji hawa wamekuwa roho ya Simba wakiibeba kwa mabao yao licha ya kwamba mmojawapo ambaye ni Mwanahamis Omari ‘Gaucho’ amewakimbia na kujiunga na klabu ya Chabab Atlas ya Morocco.

Kati ya mabao 65 yaliyofungwa na Simba Queens mpaka sasa kwenye ligi, 33 yamefungwa na wachezaji Opah Clement akiwa amefunga 23 wakati Shelda Boniface akifunga 10 huku Mwanahamis kabla ya kuondoka akiwa ametupia mabao 12.

Washambuliaji hao licha ya ukali wa kuzifumania nyavu lakini wanapata sapoti kubwa ya kupata pasi za mabao kutoka kwa viungo mahiri wa timu hiyo, Kadosho Shaban mwenye mabao sita, Joelle Bukuru (matatu) na Mkenya Omita Bertha na Mcongo Mawete Musolo.


Aisha, Grace, Amina- Yanga Princess

Moja ya pacha matata kwenye ligi hiyo msimu huu ikitokea maeneo ya Jangwani, Yanga Princess.

Wachezaji hao wamekuwa wakicheza kwa ushirikiano mkubwa na kuipaisha timu yao kwa kiasi kikubwa msimu huu mpaka kuifanya kuwa ya kuogopwa na timu pinzani.

Kati ya mabao 50 yaliyofungwa mpaka sasa na Yanga Princess, wachezaji hao watatu Aisha Massaka, Grace Yusuph na Amina Ally wamefunga mabao 31 huku mengine yaliyobaki yakifungwa na wachezaji wengine.

Hata hivyo, licha ya kufunga Amina amekuwa mmoja ya viungo tegemeo ndani ya kikosi hicho kwani amechangia karibu asilimia 80 ya mabao yote ambayo timu hiyo imefunga mapaka sasa akisaidiana na Mrundi, Aniela Uwimana.


Aisha, Aliya - Alliance Girls

Licha ya kwamba Alliance Girls msimu huu inaonekana kushuka kiwango tofauti na misimu miwili ya nyuma, lakini wachezaji Aisha Juma na Aliya Fikiri wametengeneza pacha matata inayoendelea kuibeba timu hiyo kwenye ligi.

Alliance iko nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28 na mabao 41 lakini ni kama imetoka katika mbio za ubingwa kutokana na kuwa na tofauti ya pointi 10 na vinara Simba na Yanga.

Aisha mwenye mabao 21 na Aliya mwenye mabao nane wamekuwa roho ya Alliance msimu huu kwa kuifungia mabao muhimu huku mmoja akipewa nafasi kubwa ya kuchukua kiatu cha dhahabu kama akiendelea na kasi yake.

Wachezaji hao wawili inasemekana tayari wameanza kuwindwa na timu kubwa kwenye ligi hiyo hivyo ni jambo la kusubiri kuona kama wataitosa Alliance Girls kama alivyofanya mwenzao Aisha Massaka aliyetimkia Yanga Princess msimu huu?.


Fatuma, Stumai, Donisia- JKT Queens

Hii pacha ilikuwa hatari sana mwanzoni mwa msimu lakini majeruhi yakaleta mkosi ndani ya kikosi hicho na kujikuta wengi wakiishia njiani katika mbio za ufungaji.

Fatuma Mustapha ndiye aliyekuwa hatari zaidi akiwapeleka puta wafungaji wote wa Ligi Kuu ya wanawake lakini majeraha ya goti yamekatisha ndoto zake za kuibuka mfunagji bora kwa mara ya tatu mfululizo.

Si Fatuma tu kwani hata Stumai mwenye mabao 11 na Donisia Minja aliyefunga sabawote wamekumba na wimbi la majeraha ya mara kwa mara yaliyosababisha wakashindwa kutisha kama ilivyokuwa msimu uliopita.


Amina, Aidath- Ruvuma

Moja ya timu inayoogopwa kwenye ligi nje ya Simba na Yanga ni Ruvuma Queens kwani huwa haina shughuli ndogo kutokana na ubora wilionao uwanjani.

Ubora wa timu hiyo unabebwa na mapacha hao wawili, Amina Ramadhan na Aidath Zembindezi ambao ndio wamekuwa mhimili mkubwa na kuibeba timu hiyo wanapokuwa uwanjani.

Kati ya mabao 41 yaliyofungwa na kikosi hiho, 24 yamepachikwa wavuni na wachezaji hao wawili ambao wana nafasi kubwa ya kujiunga na timu kubwa msimu ujao.


Rehema Mohammed, Zainab Dubu- Mlandizi Queens

Wachezaji hawa Rehema Mohammed na Zainab Dubu wameendelea kuibeba timu yao ya Mlandizi Queens licha ya kwamba timu hiyo msimu huu haijafanya vizuri kama wengi walivyozoea.

Pacha ya wachezaji hao imefunga mabao 27 kati ya 37 ambayo timu hiyo imefunga mpaka sasa kwenye ligi hiyo ambayo iko mzunguko wa pili.

Rehema Mohamed amefunga mabao 10 wakati Zainab Dudu akifunga Saba na bado wanatarajiwa kuibeba timu yao mpaka mwisho wa msimu licha ya kwamba tayari wameshatoka katika mbio za ubingwa.


Hasnath Linus, Agness Pallango- Tanzanite SC

Pacha nyingine konki kutoka makao makuu ya nchi Dodoma katika timu ya Tanzanite ikiwa imepachika wavuni mabao 18 kati ya 28 ambayo timu hiyo imefunga hadi sasa kwenye ligi.

Wachezaji hao wamekuwa mhimili mkubwa kwa kikosi hicho na kuwa mwiba mkali kwa mabeki wa timu pinzani kwenye ligi ya wanawake.