ONYANGO NUSU MTU NUSU CHUMA

UMESHAWAHI kuangalia filamu za kibabe zinazohusisha roboti kama Terminator, Cyborg au Robo Cop ama Robo War? Si huona namna watu waliotengenezwa kama roboti wanavyofanya kazi au wanavyopigana zaidi ya binadamu? Ndani ya Simba kuna mtu mmoja ambaye anafanya kazi kubwa, licha ya awali alipotua Msimbazi alichukuliwa sivyo.

Ndio. Ndani ya Simba miongoni mwa nyota wa kigeni walioibeba msimu huu huwezi kuliacha jina la Joash Onyango.

Beki huyo wa kati aliyesajiliwa kutoka Gor Mahia ya Kenya, awali alibezwa na hasa kwa muonekano wake akipewa majina ya ovyo ikiwamo babu, kikongwe na kadhalika.

Hata hivyo, kwa kile anachofanya uwanjani kimewafanya waliombeza kunywea, kwani jamaa ni kama nusu mtu nusu chuma.


KAZI KUBWA

Katika kikosi hicho haikuwa kazi rahisi kwa Onyango kupenya mpaka kuanza kikosi cha kwanza kwani mabeki waliokuwa wanacheza mara kwa mara walikuwa Pascal Wawa na Erasto Nyoni.

Onyango alipenya katikati yao na kuchukua nafasi kikosi cha kwanza akipishwa na Nyoni ambaye amekuwa akicheza akitokea benchi au muda mwingine akitumika kiungo mkabaji.

Tangu kuanza kwa msimu mpaka sasa Onyango amepitia mambo mengi kwenye mashindano yote aliyocheza - Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Kombe la Mapinduzi.


DAKIKA 810

Simba msimu huu walianza Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali wakicheza dhidi ya Plateau United mechi mbili na baada ya kuitoa walicheza pia mechi mbili dhidi ya Platinum ya Zimbabwe.

Mechi zote nne Onyango alicheza bila kutoka ikiwa ni sawa na dakika 360.

Ukiachana na mechi ambayo Simba walicheza jana Ijumaa dhidi ya Al Ahly, Onyango alikuwa amecheza mechi zote za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika iliyokamilika kwa timu yake kuwa vinara.

Ukijumlisha na mechi ya jana Onyango atakuwa ameitumikia Simba dakika 450 kwenye hatua ya makundi ambayo imefuzu robo fainali.


BAO MOJA

Kwa muda aliokuwa Simba, Onyango ameifungia timu hiyo bao moja katika mechi dhidi ya watani zao, Yanga, ambayo ilichezwa Novemba 7, mwaka jana.

Bao hilo alifunga dakika 86 kwa mpira wa kichwa akipokea kona iliyochongwa na Luis Miquissone na lilikuwa la kusawazisha baada ya wapinzani wao kuwatangulia kwa bao moja lililofungwa kipindi cha kwanza.


AINGIA CAF

Baada ya kucheza mechi za mzunguko wa pili katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba walikutana na mabingwa watetezi, Al Ahly katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuwafunga bao 1-0, ambalo lilifungwa na Miquissone.

Duru hilo lilipomalizika Shirikisho la Soka Afrika lilitangaza kikosi bora cha wiki na likawajumuisha wachezaji wawili kutoka Simba, Onyango na Miquissone kutokana na ubora waliouonyesha.

KUBADILISHIWA MABEKI

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika ukiondoa mchezo dhidi ya Al Merrikh ambao Simba walicheza nyumbani, mechi nyingine zilizobaki Onyango ameanza katika kikosi cha kwanza pamoja na Pascal Wawa.

Katika mechi ya Al Merrikh ambayo Simba walishinda mabao 3-0, Onyango alicheza pamoja na Kennedy Juma baada ya Wawa kukosekana kutokana na kupata kadi tatu za njano katika michuano awali.

Katika Ligi Kuu Bara Onyango ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi katika kikosi cha Simba na mara nyingi amekuwa akibadilishiwa mabeki wa kati kama Wawa akikosekana.

Kuna wakati Onyango amekuwa akicheza na Kennedy, Ibrahim Ame au Erasto Nyoni ambaye wakati mwingine hucheza kama kiungo mkabaji.


PENALTI

Katika Kombe la Mapinduzi msimu huu Simba walifika mpaka hatua ya fainali, licha ya kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu waliokuwa katika mapumziko na majukumu ya timu zao za taifa.

Katika mechi ya fainali iliyochezwa Januari 13, Simba walicheza dhidi ya Yanga ambapo dakika 90 zilimalizika kwa suluhu na katika hatua ya mikwaju ya penati Onyango na Meddie Kagere kila mmoja alikosa.

Kukosa penalti kwa Onyango na Kagere kuliifanya Yanga kutwaa kombe hilo kwa ushindi wa penalti 4-3.

Katika kombe hilo Onyango aliitumikia Simba kwenye mechi tatu za hatua ya makundi, nusu fainali na fainali yenyewe na hakuna hata mechi ambayo alitolewa.

Kutumika huko katika mechi zote tano na dakika 90 anakuwa ameitumikia Simba katika dakika 450 kwenye michezo yote ya michuano hiyo.


MCHEZAJI BORA

Licha ya kukosa penati, Onyango katika mechi hiyo ya fainali dhidi ya Yanga alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango ambacho alionyesha na kuifanya Simba kuwa salama muda wote.

Katika mechi hiyo ambayo Yanga walianza na wachezaji bora kama Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe na wengineo mbele ya Onyango walionekana kushindwa kuonyesha makali yao kwani aliwabana.

ANAKABA BALAA

Kabla ya msimu kuanza Onyango alikuwa ni moja ya wachezaji ambao wanabezwa kutokana na muonekano wake ulivyo kwani kuna waliokuwa wanaamini mchezaji huyo tayari ameshazeeka.

Baada ya kuanza kwa msimu mambo yamekuwa tofauti kwani amekuwa beki anayeokoa mashambulizi ya mipira ya vichwa ambayo yalikuwa shida kabla ya uwepo wake kuokolewa.

Mchezaji huyo ameonyesha ubora katika kuzuia mashambulizi ya timu pinzani hata yale ambayo wanakuja kwa kutumia mipira ya chini na muda mwingine washambuliaji wasumbufu wamekuwa wakiona moto kutoka kwake.

Katika ubora ambao ameuonyesha imefikia wakati habezwi na sasa amepewa jina la utani ‘Mtu chuma’ kutokana na ufiti wake, na akifika kwa washambuliaji huwa hana mzaha.


MSIKIE MWENYEWE

Onyango anasema tuzo mbalimbali ambazo amezipata Simba kama kuchaguliwa mchezaji wa kikosi cha wiki CAF, ni kama deni kwake ili kuonyesha kiwango bora zaidi kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri.

“Kikubwa ambacho nahitaji kuona Simba inafanikiwa katika michuano yote ambayo tutashiriki, kwani baada ya hapo ndipo mafanikio binafsi ya mchezaji mmoja mmoja yatakuja kwa nafasi yake,” anasema Onyango.

Kuhusu kuzungumzwa kuwa ni mzee anasema wala hajali kwani anaamini siyo mzee, ila kile ambacho atakuwa anaonyesha uwanjani na yote hayo yatajibiwa kwa vitendo na kuacha kumuita jina hilo.