NYUMA YA PAZIA: Naweza kubeti kwa Mo Salah na De Bruyne

HATIMAYE ukurasa wa mwisho huwa unafika. Kitabu kinafungwa. Mambo hufika mwisho. Wakati mwingine inatokea ghafla. Wakati hatujajiandaa sana kiakili, iliibuka ghafla kwa Sir Alex Ferguson alipofunga kitabu chake Old Trafford mwaka 2013.

Kutoka mtaa wa Anfield L4 OTH hadi mtaa wa Manchester M11 3FF naweza ‘kubeti’ kwamba mwishoni mwa msimu huu kunaweza kuwa na kilio. Mmoja kati ya Mo Salah au Kevin de Bruyne anaweza kuondoka klabuni kwake.

Kama sio mmoja kati yao, basi wote wawili wanaweza kuondoka zao. Hakuna ambacho kitawasubirisha. Tuanze na De Bruyne. Ameshinda kila kitu muhimu ambacho kinapaswa kushinda akiwa Ettihad. Bonge la mchezaji.

Ameshinda Ligi Kuu England mara kadhaa, lakini amekuwa katika kundi la wachezaji wachache katika historia ya Manchester City ambao wameipa ubingwa wa Ulaya. Alifanya hivyo msimu uliopita. Huyu mtoto wa Drongen pale Ubelgiji atatimiza miaka 33 ifikapo Juni 28, mwaka huu.

Nahisi noti za Waarabu zitamuita. Ana kila sababu ya kuitikia sauti ya noti hizo. Mkataba wake unamalizika mwakani. Kwanini asiitike? Ukweli mchungu ni kwamba hakuna alichobakisha na Manchester City watataka asaini mkataba mpya. Mkataba wao mpya hauwezi kuupiku mkataba wowote ambao De Bruyne anaweza kuupokea Saudia Arabia.

Hakuna alichobakisha England, lakini zaidi ni kwamba bado hayupo katika nafasi ya kuwa mwanasoka bora wa dunia hata kama akibaki Ulaya. Tayari Erling Haaland na Kylian Mbappe wapo mbele yake katika mbio hizo.

Na katika timu ya taifa hakuna anachoweza kufanya tena kuisaidia Ubelgiji kutwaa taji lolote kubwa. Kizazi chao kimepita na Wabelgiji wameanza kutengeneza kizazi kingine cha kina Albert Sambi Lokonga. Kizazi cha kina De Bruyne kimeanza kustaafu. Ndio hawa kina Eden Hazard. Sasa hivi wapo mitaani wakinywa bia kwa wingi.

Manchester City wataona ni bora waambulie chochote kwa mauzo ya De Bruyne mwishoni mwa msimu ili asipotee bure mwishoni mwa msimu ujao. Na watamuuza pesa nyingi kwa Waarabu kuliko wanavyoweza kumuuza kwa timu za Ulaya.

Ofa yao ya mkataba mpya inaweza kupigwa chini kwa ofa nono zaidi kutoka Saudi Arabia ambapo wachezaji wenye uwezo wa chini ya De Bruyne wamechukua pesa nyingi kwa wiki kuliko hizi ambazo De Bruyne anachukua kwa sasa Ettihad. Labda Pauni 400,000 kwa wiki. Katika umri wa miaka 33 ukiwa umeshinda mataji lukuki Ulaya unawezaje kukataa mshahara huu?

Kuna Mo Salah. Ana deni Anfield? Hapana. Mambo hufika mwisho. Ilishatajwa kwamba noti za Waarabu zilimvuta msimu uliopita, lakini Liverpool walipambana kumbakisha. Kwanini isiwe mwishoni mwa msimu huu?

Ana kazi ya kuipa Liverpool ubingwa wa England kisha wa Europa halafu aage zake. Kwa mfano, kama atashindwa hizo kazi zote mbili, kwanini umlaumu? Anaingia katika historia kama miongoni mwa wachezaji wachache wa Liverpool ambao waliipa timu hiyo taji la Ligi Kuu England baada ya miaka 30 kupita.

Kazi hii iliwashinda wengi. Kina Steven Gerrard. Kina Luis Suarez. Kina Jamie Carragher na wengineo wengi ambao wanaonekana kuwa nguli (legends) wa Anfield. Salah na wahuni wachache waliiweza. Lakini papohapo amewapa taji la Ulaya kama ambavyo kina Gerrard waliwahi kufanya. Anadaiwa nini zaidi?

Kama ilivyo kwa De Bruyne na Mo naye amezaliwa Juni. Ifikapo Juni, mwaka huu atatimiza miaka 32. Miaka ambayo miguu inaanza kukusaliti Ulaya. Kwanini usipumzike Saudia na kuwaacha kina Bukayo Saka wakikimbizana na mabeki wenye roho mbaya pale England?

Zaidi ya kila kitu ni kwamba Salah ameshaondoka katika mbio za kuwania kuwa mchezaji bora wa dunia. Amewaachia kina Mbappe na Haaland ambao wana faida za umri na mambo mengine. Yeye Liverpool hii haiwezi kumfanya awe mwanasoka bora wa dunia hata kama wakishinda taji la Ligi Kuu England.

Lakini papohapo hauwezi kuwa mwanasoka bora wa dunia kwa kutwaa taji la Europa. Na kule Misri ndio kabisa hakuwezi kumsaidia kufanya chochote. Tulikuwa kule Ivory Coast wakati tuliposhuhudia namna ambavyo walishindwa kufanya chochote.

Salah ana kila sababu ya kwenda zake Saudia. Kitu kizuri zaidi ni kwamba atakuwa amekwenda kwa Waarabu wenzake kama Riyad Mahrez alivyofanya. Wakati wachezaji wengi Wazungu wakilalamika kuhusu maisha ya Saudia yeye atakuwa haoni tofauti na maisha ya Misri. Ni mtu wa swala tano na hakuna ambacho kitamshinda kwa Waarabu wenzake.

Mkataba wake kama ulivyo wa De Bruyne unamalizika mwakani. Kama itakuja ofa nzuri kwa Liverpool sidhani kama watakataa. Lakini papohapo kwa Salah mwenyewe nadhani atajiambia wazi kwamba wakati wake wa kubaki Anfield umemalizika.

Tayari mradi wao na Jurgen Klopp unaelekea kufika mwisho kwa sababu hata Klopp mwenyewe ametangaza kuondoka mwishoni mwa msimu huu. Rafiki zake aliotengeneza nao timu kali pale Anfield, Sadio Mane na Roberto Firminho wote wapo Saudia. Kwanini asijiunge nao?

Tusubiri na kuona nini kinaweza kutokea mwishoni mwa msimu, lakini kadri ninavyotazama naona wazi kwamba mmoja kati ya De Bruyne au Salah ataondoka England. Lakini ndani ya moyo nahisi wote wanaweza kuondoka kwa sababu wana sababu sawa za kuondoka. Sioni walichobakisha England. Na wakati huohuo kuna noti nyingi za Saudia zinawasubiri.

Uzuri wa noti za Saudia ni kwamba unazichuma nyingi huku ukiwa unapumzika. Kucheza Saudia ni tofauti na kukabana na kina William Saliba pale England. Unapata pesa nyingi huku ukiwa na upinzani mchache uwanjani. Fikiria kwamba unapewa jukumu la kumkaba Ronaldo wa leo.