NYUMA YA PAZIA: Mzimu wa Messi hautuachi hadi astaafu

NYUMA YA PAZIA: Mzimu wa Messi hautuachi hadi astaafu

KWAMBA Lionel Messi hakustahili kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia? Labda. Inawezekana. Kabla ya kufikiria kwamba hakustahili kutwaa tuzo hiyo kazi ya kwanza ngumu inayopaswa kufanyika ni kumuondoka Messi mwenyewe katika ulimwengu wa soka. Tusimuue. Tuondoe jina lake katika fikra.

Sitaki kuongea kuhusu takwimu za nani alistahili kuwa mwanasoka bora wa dunia. Inawezekana ni Robert Lewandowski. Inawezekana ni Mbwana Samatta. Inawezekana ni Lorenzo Insigne wa Napoli. Wakati mwingine namba hazidanganyi.

Subiri. Wapo wengi ambao wanaamini kwamba labda ilikuwa ni zamu ya mtu mwingine nje ya Messi. Labda ilikuwa ni zamu ya Lewandowski. Amefunga mabao mengi katika misimu miwili iliyopita. Amefanya mambo mengi makubwa.

Hata hivyo, kuna mambo mawili yaliyoamua kutoka kwa wapigakura. Kwanza ni mapenzi yao kwa Messi. Na pili Messi alikuwa amewapa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni namba zake za mabao na pasi za mwisho akiwa na Barcelona msimu uliopita. Lakini kubwa zaidi ni kwamba alikuwa ameshinda Copa America Juni mwaka huu.

Hii sababu ya pili ilikuwa kubwa zaidi. Dunia ilikuwa inasubiri Messi atwae taji katika timu yake ya taifa. wapigakura ambao ni wazi ni mashabiki wa Messi nao wakafurahi na kukitumia kama kigezo kikuu kumpa Messi taji lenyewe.

Messi aliposimama akaongelea kuhusu tuzo za mwaka 2020 ambazo hazikufanyika. Alijua kwamba hakufanya kitu cha maana ambacho yeye na swahiba yake Ronaldo walifanya katika mwaka huo. Ni Kweli Lewandowski alikuwa amestahili. Tatizo dunia ilikuwa imeshambuliwa mno na Uviko na tuzo zenyewe hazikuwepo.

Messi alikuwa anacheza na akili za watu. Alijua kwamba kwa mwaka uliofuata ambao ni mwaka huu alikuwa na kitu cha kujitetea. Alikuwa na Copa Amerika kwapani kwake. Vyovyote utakavyosema kuhusu ubora wa Lewandowski kwa mwaka wa pili mfululizo lakini Copa Amerika ni kitu kikubwa kwa Messi kama ambavyo Euro ilikuwa kitu kikubwa kwa Ronaldo mwaka 2016 alipotwaa pale Ufaransa.

Tatizo la msingi ambalo nimeliona katika tuzo hizi ni jina lenyewe la Messi pamoja na mpinzani wake Ronaldo. Wale ambao wanasema Lewandowski alistahili zaidi ni wale ambao wapo katika upande wa Ronaldo. Inawezekana wana hoja au hawana lakini wapo zaidi upande wa Ronaldo.

Katika tuzo hizi za dunia watu wa upande wa Ronaldo hawataki Messi aende mbali zaidi kuliko Ronaldo. Imetosha. Wangependa wote Messi na Ronaldo wasiwe katika kinyang’anyiro hiki tena. Kama Messi alikuwa amechukua mara sita na Ronaldo mara tano basi imetosha. Messi kuongeza hatua kunakera wengi.

Ronaldo msimu huu hakuwa katika tatu bora na haio-nekani kama anaweza kurudi tena katika tatu bora. Hauwezi kumlaumu, Ronaldo ni mkubwa kuliko Messi. Messi naye inaonekana huu unaweza kuwa msimu wake wa mwisho kuwa katika tatu bora labda PSG ifanye maajabu Ligi ya Mabingwa Mei mwakani au Argentina itwae Kombe la Dunia Qatar. Vyote viwili ni vigumu.

Kitu cha msingi ni majina yote mawili kutokuwepo katika tatu bora. Kuanzia hapo dunia inaweza kustarehe na wale wapigakura wanaweza kuchagua watu kwa uhuru zaidi kuliko ambavyo ilivyo sasa. Kwa mfano, hata kama Messi asingekuwepo katika tatu bora katika tuzo hizi na jina la Ronaldo likajitokeza sidhani kama wapigakura wasingempa Ronaldo.

Haya majina mawili inabidi yatoweke ili tuanze kuishi kwa uhuru zaidi. Luka Modric licha ya kuwa na vigezo lakini alinufaika zaidi kwa kuwepo kwa majina yote mawili. Wapigakura wakaona bora wampe Luka kuepusha lawama.

Wapigakura watakuwa huru zaidi yatakapoingia majina kama Kylian Mbappe, Karim Benzema na Lewandowski. Dunia itakuwa imeanza upya na tutakuwa tumekata minyonyoro ya kina Ronaldo na Messi katika tuzo hizi.

Ninachodhani ni kwamba kwa sasa wapigakura wanapofanya yao na jina la Messi linapojitokeza huwa wanashindwa kuelewa kwamba wanachagua mchezaji bora wa mwaka au mwanasoka bora wa muda wote. Mambo ya ajabu aliyofanya Messi yamewakaa akilini kiasi kwamba wanampima mtu kama Lewandowski na ubora wake kisha wanalinganisha na matukio makubwa ambayo Messi amewahi kuyafanya katika soka. Hawafuati kalenda ya mwaka.

Hii sio mara ya kwanza. Kwa mfano, iliwahi kutokea mwaka 2010. Mchezaji kama Wesley Sneijder alitwaa ubingwa wa Ulaya na Inter Milan na mataji mengine mawili ya Italia. Mwaka huo huo pale Soweto huyu Mdachi aliifikisha Uholanzi katika nusu fainali za Kombe la Dunia.

Mwaka huo huo, Andres Iniesta aliipa Hispania taji la Kombe la Dunia na alikuwa moto kweli pale Barcelona. Hata hivyo, mwisho wa siku licha ya yote ambayo Iniesta na Sneijder walifanya bado tuzo ilikwenda kwa Lionel Messi.

Kuanzia hapo na mengineyo mengi ambayo yaliwahi kutokea nyuma niliamini kwamba tuzo hizi hazihitaji vigezo sana. Inatokana tu na matamanio ya wapigakura. Lakini pia kama kuna mchezaji mkali akiongeza vigezo kadhaa kama ambavyo Messi amefanya mwaka huu maisha yanakuwa rahisi kwa Messi. Na ilikuwa hivyo hivyo kwa Ronaldo.

Hili ni jinamizi ambalo tutaishi nalo kwa miaka mingi. Kuanzia wale ambao wanapendekeza majina hadi kwa wapigakura. Kuliona jina la Messi katika sanduku la kura kunabadili mawazo ya wapigakura wengi. Jina lake halistahili kuwepo dhidi ya kina Lewandowski.

Wakati dunia ikiwa inabishana kama Messi ni mchezaji bora zaidi kuliko kina Diego Maradona, Pele, Johan Cruyff na wengineo, maisha yanakuwa magumu zaidi kwa watu kama kina Lewandowski kupata nafasi ya kushinda chochote hata kama wanastahili.