NYUMA YA PAZIA: Kesi ya kushangaza ya beki Ben White

SIMU iliita katika ofisi za FA ya England wiki iliyopita. Ilipopokewa muongeleaji alikuwa anazungumza Kiingereza chenye lafudhi ya Kireno. Edu. Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal alikuwa na ujumbe kutoka kwa beki wake, Ben White kuelekea kwa kocha wa England, Gareth Southgate.

Kwamba? White amemwambia kuwa hataki kufikiriwa kuchaguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England. Inashangaza. Ndoto ya kila mchezaji hasa mchezaji wa Kiingereza. White ana mgomo wake ambao utashangaza kidogo. Sio kawaida.

Inadaiwa kwamba wakati Waingereza wakiwa katika Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar, kocha msaidizi wa England, Steve Holland alimuuliza maswali kadhaa White kuhusu kampeni ya Arsenal ambayo ilikuwa na msimu bora kuelekea mwishoni mwa msimu wa mwaka jana. White hakuonekana kuelewa lolote kuhusu swali la Holland ambalo alikuwa amemuuliza mbele ya wachezaji wenzake.

Baadaye Holland akaonekana kukasirishwa na upeo mdogo wa White kuhusu soka. Aliamini kwamba White hakuwa na mpango wowote na soka, hivyo ‘commitment’ yake katika kikosi hicho ingekuwa ndogo. Alichoongea mbele ya White na kundi la wachezaji hakikwenda vyema katika ubongo wa staa huyo wa zamani wa Brighton and Hove. White akahisi kudharauliwa mbele ya wenzake. Ni kweli. Hakuwa na ufahamu kuhusu soka, lakini hilo lilikuwa jambo lake binafsi. Akaamua kuondoka zake kambini na kurudi nyumbani England. Na sasa ameigomea timu ya taifa. Nadhani ni kwa sababu Holland bado yupo katika kikosi hicho.

Labda atarudi kikosini kama Holland na Southgate wakiondoka. Lakini huenda pia akaamua asirudi tena katika kikosi hicho. Mpira sio mapenzi yake. Ni stori ya kuchekesha kidogo  White anatajwa kama miongoni mwa wanasoka wa kushangaza ambao tunaishi nao katika dunia ya kisasa. Hana mapenzi kabisa na kazi anayofanya.

Anacheza soka kwa sababu anaweza. Anacheza soka kwa sababu linampatia pesa. Anakiri kwamba tangu alipokuwa mdogo mpaka sasa huwa hatazami soka katika televisheni. Hata yeye mwenyewe huwa anajitazama mara chache kwa sababu za kiufundi tu. Anadai hawezi kabisa kukaa chini na kutazama mechi ya soka. Bora afanye kitu kingine.

Wapo wanasoka wachache wa dizaini hii na hawajifichi. Usimshangae sana White. Kuna Carlos Tevez. Mwaka 2008 aliwahi kukaririwa akidai kwamba hapendi kabisa soka. Alidai kama kuna mechi ya El Clasico inaendelea kati ya Barcelona na Real Madrid halafu kando yake kuna chaneli nyingine inayoonyesha gofu basi angependelea zaidi kutazama gofu.

Kuna rafiki yetu mwingine anaitwa Marc-Andre ter Stegan. Yeye anadai hapendi mpira. Hapendi kutazama mechi. Mechi chache ambazo anatazama ni zile ambazo kuna rafiki zake wanacheza. Anadai kwamba hawafahamu wachezaji kibao ambao wanacheza La Liga licha ya kwamba ni maarufu ulimwenguni.

Mwingine? Rafiki yetu Gabriel Batistuta. Bonge la mshambuliaji. Alitesa vizuri katika jezi ya Argentina na mashabiki wa klabu yake maarufu ya Fiorentina walimchukulia kama ‘mungu mtu’. Aliwahi kukiri wazi kwamba hapendi mpira. Anapenda kucheza mchezo wa polo na ndipo mapenzi yake yalipo. Kitu kingine anachopenda ni kuvua samaki.

Unamkumbuka rafiki yetu Benoit Assou-Ekotto? Wakati fulani alikuwa anacheza Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Cameroon. Aliwahi kuwakera Waingereza alipohojiwa na kudai anacheza soka kwa sababu ya pesa. Hapendi soka. Mapenzi yake yapo kwenye muziki na marafiki zake. Anacheza soka kwa sababu analijua na anapata pesa. Rafiki yake mwingine White ni staa wa zamani wa Italia, Christian Vieri. Huyu aliwahi kukiri wazi kwamba hapendi soka. Anapenda sana kriketi. Alitamani kuwa mcheza kriketi mzuri kuliko mwanasoka mzuri. Bahati mbaya kwake ni kwamba aliangukia kuwa mwanasoka mzuri kuliko kuwa mcheza kriketi mzuri.

Na sasa mikononi tunaye pia White. Wanasoka wa aina yake huwa wanashangaza. Baadaye huwa wanachukua uamuzi wa ajabu bila ya kutegemea. Unaweza kukuta anastaafu soka katika umri mdogo kwa sababu hapendi anachofanya. Kuna wanasoka wanastaafu wakiwa na umri wa miaka 29 tu baada ya kutamani maisha mengine nje ya soka.

Lakini kuna wale ambao wanapenda sana soka. Wengine wanapenda kwa namna wanavyocheza. Wanatamani pambano la soka lisimalizike. Hawa ndio kina Lionel Messi. Wanapenda tu soka kiasi kwamba kuna wakati unahisi wangeweza hata kucheza bure. Unaona kabisa wanacheza soka kwa furaha.

Halafu kuna wengine ambao wanapenda zaidi soka na mbinu zake kiasi kwamba wanaangukia katika kazi ya ukocha. Hawa ndio kina Pep Guardiola. Inaelezwa kwamba Pep anapumua soka. Kila anachofanya anawaza soka. Alianza kuwakosoa makocha wake tangu akiwa mchezaji. Alikuwa akiwaelekeza makocha wake namna ambavyo mpira unapaswa kuchezwa. Haishangazi kuona leo amegundua vitu vingi katika soka.

Sidhani kama rafiki yetu White angeweza kutugundulia mambo haya. Kwamba kipa atumie miguu zaidi kuliko mikono. Kwamba mabeki wa pembeni wanaweza kucheza katikati kama viungo. Kwamba unaweza kucheza soka bila mshambuliaji na mambo yakawa safi na timu ikachukua ubingwa.

Unaweza kumkuta White katika kucheza soka lakini hauwezi kumkuta katika kufundisha soka. Katika kufundisha lazima uwe na mapenzi. Sidhani kama unaweza kufundisha mpira kama hauupendi na unafikiria vitu vingine na kuvipenda kuliko soka.

Na kuhusu White nasubiri kuona hatima yake itakuwa nini. Nasubiri kuona pindi Southgate na Holland wakiondoka England ataweza kurudi katika kikosi cha England au atakuwa ametumia kama kisingizio kuondoka moja kwa moja katika kikosi cha timu yataifa hilo. Ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli kuhusu maisha yake ya soka.