NYUMA YA PAZIA: Infantino na washkaji zake wakiwa katika ubora wao

KIGALI juzi, Gianni Infantino alichaguliwa kuwa Rais wa FIFA kwa mara nyingine tena. Nimecheka. Alichaguliwa bila ya kupingwa na mtu yeyote yule. Kila mtu ukumbini alikubali kwamba Infantino anafaa kuwa Rais kwa mara nyingine tena.

Imenikumbusha usela wa watu wa FIFA. Infantino ni mzungu, lakini hapo hapo Wazungu ndio wana nguvu zaidi FIFA. Hawa ndio wahubiri wa demokrasia. Inakuwaje mtu mmoja anagombea peke yake na anapita bila ya kupingwa? Sikiliza, kuna FIFA halafu kuna dunia nyingine ambayo tunaishi. Hii nakukumbusha kwa mara nyingine tena.

FIFA ni kama vile nchi kubwa ambayo haina dola. Haina jeshi, haina polisi, haina watu wa usalama, haina serikali lakini ina nguvu kubwa duniani. Ni kama Kanisa Katoliki. FIFA wana uamuzi wao binafsi. Wana watu wao wao. Wana akili zao. Kitu kinachofurahisha zaidi ni kwamba hakuna anayeweza kuingilia uamuzi wao.

Haishangazi kuona ukiwa Rais wa FIFA unaweza kutawala miaka mingi bila ya kuguswa. Ni suala tu la kulinda maslahi ya wenzako wanaokuchagua. Mbrazil Joao Havalange aliongoza FIFA kwa miaka 24. Kuanzia mwaka 1974 mpaka 1998. Kuna huyu Mswisi, Sepp Blatter naye aliongoza FIFA kwa miaka 17. Hata Infantino anaweza kupiga miaka 20 na zaidi kama akitulia.

Inachotakiwa ni kula na watu vizuri. Kwa mfano, Infantino alikuwa anatetea michuano ya Kombe la Dunia kufanyika Qatar. Pale alikuwa na mambo mawili. Kwanza ana bahasha yake lakini pili anapata kura za uhakika kutoka katika nchi za Falme za Kiarabu ambazo zinamuona muungwana kwa kupigania maslahi yao.

Infantino anapeleka pesa kila mahali. Baada ya Kombe la Dunia pale Qatar, FIFA imekuwa tajiri zaidi. Kwa sasa ina utajiri wa dola 4 bilioni ambazo inabidi zigawanywe kwa nchi zote wanachama wa FIFA katika kipindi kijacho cha bwana Infantino. Hapo kuna bahasha binafsi kwa wakubwa wa nchi zote lakini pia kuna maendeleo ya kweli. Kwanini usichaguliwe?

Wakubwa wa nchi wanachama wana uhakika gani kama mtu mpya anayetaka kuchukua nafasi ya bwana wao ataweza kuhakikisha maslahi yao? Ndio maana hawa marais wanakaa vipindi virefu. Kwa mfano, kama Marekani isingeingilia kati na kuamua kumng’oa Blatter hapana shaka mpaka leo angekuwa madarakani. Blatter asingeng’oka kwa boksi la kura. Sahau kuhusu hilo.

Anachofanya Infantino kuendelea kubakia madarakani ni kile kile alichofanya Blatter. Unatakiwa kuwapenda wanachama wako wote. Jaribu kufikiria, ungeweza kuamini kwamba mkutano wa kumchagua aendelee kuwa Rais ungefanyika Kigali? Kwanini usifanyike London, Rio de Janeiro, Miami au Melbourne? Hapana umefanyika Kigali.

Upendo huu aliufanya sana Blatter. Unasambaza upendo katika kila kona ya wapiga kura wako. Kwa kufanya hivyo tu tayari ametukosha watu wa Afrika Mashariki. Lakini kabla ya hapo, ni mara ngapi tumemuona Infantino akizurura katika kila kona ya dunia? Hata hapa kwetu amewahi kufika kwa sababu mbalimbali. Akitoka Kigali utasikia yupo New Zealand. Baada ya hapo utasikia yupo Malawi.

Angalia namna ambavyo Kombe la Dunia linavyogawanywa. Lilikuwa Afrika mwaka 2010. Mwaka 2014 likaenda Amerika Kusini kwa Brazil. Mwaka 2018 likaenda Ulaya pale Russia. Mwaka 2022 likaenda Asia pale Qatar na mwaka 2026 itafanyika Amerika Kaskazini katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Hii ina maana Kombe la Dunia litakuwa limefanyika katika mabara matano tofauti katika kipindi hiki. Hili ndio lengo la kina Infantino katika kube-mbeleza wanachama wake. Kila mmoja anajisikia kuwa sehemu ya FIFA. Hapo hapo kumbuka kuna michuano ya wanawake na vijana. Huwa fainali zake zinasambazwa katika nchi mbalimbali tofauti.

Mwaka jana tulishuhudia michuano ya Kombe la Dunia ya vijana ikifanyika India. Ungeweza kuifikiria India? Nchi ambayo inajulikana zaidi kwa mchezo wa kriketi. Soka unaweza kuwa mchezo wa nne kama sio wa tatu kwa kupendwa pale India lakini wamepelekewa kuandaa Kombe la Dunia.

Kura zote anazopata ni hiyari ya wapigakura wake. Wala hawalazimishi lakini hakuna mwenye ubavu wa kujaribu kumuondoa kwa sababu anaigawanya keki yake katika usawa ambao unatakiwa. Ni kazi rahisi ambayo ingeweza kuwashinda wanadamu wengine wenye choyo au dharau. Ukiwa na akili nzuri unaweza kukaa madarakani miaka 34.

Kitu kingine ambacho kinawaweka madarakani muda mrefu ni namna ambavyo wanawatetea watu wao kutoka katika makucha ya serikali zao. FIFA haiguswi na wakubwa lakini pia wanachama wao hawatakiwi kuguswa na wakubwa wa nchi zao. Ndio maana nilicheka pale ambapo walitoa msimamo wa kuendelea kuzifungia Zimbabwe na Sri Lanka.

Serikali za nchi hizo zimeingilia masuala ya kiutawala ya soka. FIFA wamezifungia. Hapo watawala wa soka wa nchi hizo wanacheka tu. Hawana cha kupoteza. Urafiki wao na FIFA uko pale pale na juzi walikuwepo Kigali. Wanaoumia ni serikali za Zimbabwe na Sri Lanka pamoja na wananchi kwa ujumla ambao hawaoni timu zao zikishiriki katika michuano mbalimbali.

Urafiki wa Rais wa soka wa nchi kwenda kwa Infantino ni mkubwa kuliko uhusiano wa Rais huyo kwenda kwa Rais wa nchi yake. Huu ndio ukweli ambao unawaumiza wakubwa wa serikali nyingi duniani. Ni ukweli ambao wanaukubali kwa shingo upande tu.

Kura za Rais wa soka wa Zimbabwe na yule wa Sri Lanka lazima zimekwenda kwa Infantino kwa sababu amewatetea dhidi ya makucha ya serikali zao. Na hili linatokea kwa nchi zote wanachama wa FIFA. Iwe Marekani, Zambia, Argentina na kwingineko. Wanateteana katika kila kitu. Hauwezi kuwaambia kitu watu wa Infantino.

Kuonyesha mshikamano zaidi huwa wananiachia hoi pale wanapojiita familia. Wanajiita ‘football family’. Ni ngumu kwa mtu kutoka nje yao kuja kuwaongoza. Wao ni kama familia. Ni ngumu pia kwa mtu kutoka nje na kuja kuingia kwao kama hawakukubali. Inabidi uwe mwenzao. Wanaishi kama familia na wana mshikamano kama familia.

Bahati nzuri hata ndani ya nchi huwa wanajiita football family. Kwa mfano, ni ngumu kumuondoa Rais wa Shirikisho la soka la Tanzania kama Fifa wanamtaka. Wanampa sapoti zote wakati wa uchaguzi kwa sababu ni mwenzao. Ni ngumu kwa mtu kujitokeza ghafla hapa na kumuondoa Wallace Karia kwa sababu FIFA inamtambua kama mwanafamilia mwenzao zaidi ya kila kitu.

Kama ambavyo Infantino atamsaidia Karia kushinda uchaguzi nchini ndivyo ambavyo Karia atamsaidia Infantino kushinda uchaguzi tena bila ya kupingwa pale Fifa kama ilivyotokea juzi Kigali. Hawa ndio FIFA. Waelewe vyema. Ni genge fulani la washkaji wanaopendana na wenye agenda moja. Uzuri ni kwamba hakuna mtu kutoka nje anaweza kuingia ndani na kuwaingilia mambo yao. Mfano ni kama Infantino alivyogombea peke yake pale FIFA na akapita kwa kura zote juzi pale Kigali.