NYUMA YA PAZIA: Haaland kwenda City, majibu saba ya wazi

NYUMA YA PAZIA: Haaland kwenda City, majibu saba ya wazi

NDOTO? Ndio, tena ya kutisha. Tafuta msimamo wa Ligi Kuu ya England. Utazame tena na tena. Kufikia juzi usiku wa manane pale Moneliux, Manchester City walikuwa wamefunga mabao 94 na kufungwa mabao 22 tu. Piga hesabu za vidole. Hesabu rahisi. Tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ni mabao 72.

Ndani ya hesabu hizi za kutisha, dakika chache kabla hawajasafiri kwenda Wolves, City walikuwa wamemtangaza yule ‘Jini’ kuwa mchezaji wao. Jini? Ndio mtaani kwetu, Erling Bruut Haaland anaitwa jini. Sijui kwanini wahuni wa mtaani kwetu wanamuita jini. Nadhani ni kwa sababu ya kulivamia lango bila ya kuonekana na kisha kuacha madhara makubwa.

Kwa sasa usiombee kukutana na washambuliaji hawa hapa. Roberto Lewandowski. Halafu kuna Karim Benzema Halafu kuna Harry Kane. Lakini zaidi kuna huyu hapa, Erling Haaland. Kwa Haaland kwenda City, timu ambayo mpaka sasa imekaribia kufunga mabao mia ya ligi ikiwa mara nyingi haichezi na mshambuliaji pale mbele, ni jambo linalotisha.

Kuna maswali saba nimejijibu kwanini Haaland amekwenda City. Awali alionekana kuning’inia na kukosa mwelekeo. Ubora wake ulikuwa umemuhusisha na kila timu kubwa lakini hatimaye ameangukia City.

Swali la kwanza. Kwanini uhamisho wake umekamilika licha ya wakala wake, Mino Raiola kufariki dunia wiki mbili zilizopita? Watu kadhaa walijiuliza swali hili. Ukweli ni kwamba Raiola alikuwa kiongozi wa taasisi tu. Nyuma yake kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wanafanya kazi kwa niaba yake. Yeye alikuwa bosi tu.

Nyuma yake kulikuwa na wanasheria wabobevu, maskauti wa kuchungulia vipaji visivyo vya kawaida, wataalamu wa mazungumzo, watunza kumbukumbu na watu wengi. Kifo chake hakijamaliza dili. Ofisi inaendelea. Ni kama ambavyo ofisi nyingi zinafiwa na watendaji wakuu lakini ofisi zinaendelea.

Wateja wa Raiola kuanzia Haaland, Romelu Lukaku, Paul Pogba, Moise Kean na wengineo wote wapo salama. Wana mikataba na kampuni ya Raiola na sio Raiola binafsi. Hata kama Raiola angekuwa hai hakuna ambacho kingebadilika. Haaland angekwenda zake City.

Tunarudi katika sababu nyingine. Kwanini Haaland amekwenda City? Hawakuwa na mshindani mkubwa. Angeenda wapi kwingine? Real Madrid walinusa kwake lakini wana Karim Benzema aliye katika moto. Usingekuwa uhamisho bomba zaidi kwake.

Madrid waliamua kutopoteza pesa. Badala yake wamewekeza nguvu zao kwa Kylian Mbappe. Huyu ataenda kucheza pembeni halafu Benzema ataendelea kucheza katikati. Katika dunia ya leo ambayo timu inacheza mshambuliaji mmoja, Benzema na Haaland hauwezi kuwaweka pamoja.

Lakini watazame Barcelona. Wana umaskini. Kwa sasa hawana nguvu ya pesa na wameendelea kukusanya wachezaji wa bure kina Pierre-Emerick Aubameyang. Usajili wa Haaland una fungu kubwa ingawa inaonekana kama amesajiliwa kwa dau dogo.

Mshahara wake unakaribia Pauni 500,000 kwa wiki. Achilia mbali bonasi zake. Kumbuka kilichomuondoa Lionel Messi. Bajeti yake ilikuwa inabana kiasi kwamba La Liga wenyewe walinyoosha mikono juu.

Kwa sasa Barcelona hawana afya ya kumchukua mchezaji mkubwa kama walivyofanya kwa kina Luis Suarez, Ousmane Dembele, Phillipe Coutinho na wengineo.

Angeenda wapi kwingine? Manchester United akacheze Europa? Hapana. Miaka kumi iliyopita Haaland alikuwa ana sababu tano za kwenda Manchester United lakini sasa hivi labda ana sababu moja tu ya United. Pesa. Lakini kama kuna timu inakupa pesa, soka safi na katika benchi kuna Pep Guardiola kwanini usiende?

Bayern Munich? Ilikuwa inanitia hofu. Wachezaji wazuri wanaotamba katika klabu nyingine zote za Ujerumani ni kama vile wanaandaliwa kucheza Bayern Munich. Haaland lazima alitamaniwa na Bayern Munich lakini katika kesi kama ileile ya Madrid kumbuka kwamba Bayern wana Lewandowski. Hauwezi kuwaweka Lewandowski na Haaland pamoja.

Liverpool? Wana ukubwa wa mafanikio lakini sio ukubwa wa pesa. Mpaka sasa wanateseka kuwapa mikataba mipya mastaa wao kwa kile wanachoita sera za klabu yao za kulipa mishahara kiduchu. Sijui watakwenda hivyo mpaka lini. Mpaka leo hatujui kama Sadio Mane atabakia. Hatujui kama watamlipa Mo Salah anachotaka.

Hatimaye walikuwa wamebakia City tu hasa ukizingatia kwamba Chelsea hawaeleweki kuhusu umiliki wa timu yao. Kufikia hapo Pep Guardiola akamnasa kijana wake kiulaini. Hapo hapo unaweza kuongeza kwamba baba yake, Haaland, Alf Inge Haaland alicheza City kwa miaka mitatu. Urafiki wa Mzee Haaland umesaidia pia kusababisha dili.

Hizi zote ni sababu nzuri za kawaida, lakini kitu cha msingi. Kipi bora kuliko pesa? Katika umri wa miaka 21 tu, Haaland anaenda kupokea zaidi ya Pauni 400,000 kwa wiki. Maisha yanataka nini zaidi? Kipengele cha mauzo ya Haaland kutoka Borrusia Dortmund kilikuwa na dau kiduchu tu la Pauni 61 milioni. Hata Arsenal wangeweza kumchukua lakini katika mshahara ndipo City walitanua kifua.

City inawezekana walimkadiria Haaland thamani ya Pauni 150 milioni. Kama wameona wamempata kwa Pauni 61 milioni kwanini wasipeleke pesa nyingine katika mshahara wake? Wengine hata kwa dau la Pauni 61 milioni wasingeweza kumpa Haaland mshahara huo.

Kumbuka kwamba fursa hiyo imejitokeza huku Guardiola akiwa hajaziba pengo la Sergio Aguero tangu alipoondoka mwaka 2020. Alijaribu kwa Kane mwaka jana lakini dau lake lilikuwa mara mbili ya hili la Haaland na bado Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy aligoma.

Na sasa Haaland amekwenda zake City. Ni ndoto inayotisha unapojikumbusha kwamba anakwenda kusimama mbele huku nyuma yake kukiwa na Kelvin De Bruyne, Riyad Mahrez, Phil Foden, Ilkay Gundogan na wengineo. Ni ndoto inayotisha. Labda pia watakuwa wamemaliza tatizo lao linalowasumbua katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Tusubiri.