NYUMA YA PAZIA: AFADHALI EL CLASICO FEKI IMEPITA KIMYAKIMYA

Muktasari:

WALIOMUONA mwanamke aliyeitwa Cleopatra wa pale Misri wanadai alikuwa mrembo sana. Mrembo akiwa na nguo na mrembo wakati hana nguo. Mrembo akiwa na nguo mbovu, lakini mrembo pia akiwa na nguo nzuri. Alibakia kuwa mrembo.

WALIOMUONA mwanamke aliyeitwa Cleopatra wa pale Misri wanadai alikuwa mrembo sana. Mrembo akiwa na nguo na mrembo wakati hana nguo. Mrembo akiwa na nguo mbovu, lakini mrembo pia akiwa na nguo nzuri. Alibakia kuwa mrembo.

Kama urembo wa Cleopatra ungewekwa katika kila kitu duniani, basi katika soka mechi ya El Clasico pale Hispania ingeweza kuwa Cleopatra. Hata hivyo nadhani hiyo ingekuwa zamani. Sina uhakika sana kama zama hizi hii mechi ni Cleopatra tena.

Zamani kidogo, karibu kila msimu hii ilikuwa mechi ambayo ingejaza mastaa. Ingeweza kuwa mbovu lakini ingejaza mastaa wenye mvuto. Ingeweza kuwa nzuri, lakini bado ingekuwa imejaza mastaa wenye mvuto. Ingeweza kuwa ya kawaida, lakini bado ingejaza mastaa wa kawaida. Ni kama Cleopatra mwenye nguo au asiyekuwa na nguo, bado angeendelea kuwa na mvuto.

Nilikuwa natazama pambano la El Clasico wiki iliyopita. Nyakati zimekwenda wapi? Kulikuwa na mastaa wawili tu wakubwa uwanjani. Lionel Messi kwa upande wa Barcelona na tunaweza kusema Karim Benzema kwa upande wa Real Madrid.

Waliobaki ni mastaa ambao ama wamepitwa na wakati na hawakuwahi kuitikisa duniani vilivyo, au wengine wanakaribia ustaa, au wengine ni wachezaji wa kawaida tu. Maana halisi ya El Clasico sio hii. Maana halisi ya El Clasico ni mechi ngumu na ambayo imekusanya mastaa wakali wa hadhi ya dunia (El Clasico)

Nje ya hapa inaweza kuwa mechi ngumu sana, lakini hata wakati mwingine Everton na Wolves huwa wanatupa mechi ngumu na ya kusisimua. Urembo wa El Clasico ni mastaa na bahati mbaya kuna mastaa wengi zaidi wa hadhi ya Clasico ambao hawachezi El Clasico kwa sasa. Inatia huzuni.

Zamani sana hii mechi upande mmoja kulikuwa na Zinedine Zidane, Claude Makelele, Raul Gonzalez, Luis Figo, langoni kuna Ilker Casillas, mabeki kuna Fernando Hierro au Ivan Helguera. Upande mwingine ungeweza kumkuta Rivaldo, Carles Puyol, Pep Guardiola, Patrick Kluivert, Zenden na wengineo.

Baadaye mechi hii ilikuwa na kina Ronaldinho, Deco, Samuel Eto’o, Ruud van Nisterlooy, Roberto Carlos, Mamadou Diara, Raul Gonzalez, Guti na wengineo wengi. Ilikuwa mechi ambayo ungeiwaza kwa wiki kadhaa kabla ya mwamuzi kupuliza kipenga cha kuanzisha mechi.

Miaka ya karibu tumeiona ikiwa na kina Messi, Cristiano Ronaldo, Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Sergio Ramos, Gareth Bale, Neymar, Thierry Henry, na wengineo wengi. Karibu wote ni mastaa watupu ambao wana heshima zao hapa duniani.

Pambano la wikiendi iliyopita nilikuwa nalitazama pambano ambalo lilikuwa na Benzema na Messi. Hata kama Sergio Ramos hakucheza lakini sifa za pambano hili sio la kuwasubiri Ramos na Sergio Busquets wakicheza. Pambano hili lina urembo mkubwa kwa wachezaji wa mbele.

Lakini ni wazi kwamba wakati tukitazama pambano la El Clasico wikiendi iliyopita hatukuweza kuwaona tena wachezaji hawa. Sio kwa sababu Ronaldo hayupo. Hapana, hata Ronaldo mwenyewe alikuta wachezaji wa maana pale Madrid lakini siku hadi siku wanaondoka.

Tatizo kuna wachezaji wengi wenye hadhi ya El Clasico ambao hawapo katika klabu hizi na wanapunguza ladha ya mechi yenye. Haijalishi mechi inakuwa tamu kiasi gani lakini wanaonogesha mechi hii siku zote ni wachezaji wenye majina makubwa.

Fumba macho ufikiri kwamba upande wa Real Madrid katika mechi hii kungekuwa na Karim Benzema, Kevin de Bruyne, Kylian Mbappe, Bruno Fernandes na Virgil van Dijik. Tayari ingekuwa mechi ambayo unatamani kuiona.

Fikiria upande wa pili kungekuwa na Paul Pogba, Neymar, Messi, Roberto Lewandowski, Mohamed Salah, Erling Haaland. Tayari kungekuwa na msisimko wa kutosha zaidi. Tatizo wachezaji wenye hadhi ya El Clasico wanacheza katika klabu nyingine.

Achilia mbali Messi ambaye amezeeka, katika kikosi cha Barcelona hakuna mchezaji yeyote ambaye anaweza kuuzwa kwa pauni 100 milioni. Upande wa Real Madrid ni hivyohivyo. Zamani El Clasico ilikuwa inabeba wachezaji wa aina mbili.

Kwanza ni wale ambao walinunuliwa kwa bei mbaya za uhamisho wa dunia, lakini pili ni wale ambao wamejikuta wakitamba na madau yao yamekwenda juu zaidi. Leo sokoni ni wachezaji wachache wa Madrid na Barcelona ambao wanazidi thamani za wachezaji wengine walio nje ya kikosi chao.

Kwa staili hii ladha ya El Clasico inapotea. El Clasico maana yake ni timu kubwa na majina makubwa. Mechi kali tunaweza kuletewa mezani hata tunapotazama Leicester City dhidi ya Everton. Tunahitaji majina zaidi kuliko mechi kali.

Nadhani pesa za Waarabu zimeharibu El Clasico. Siku hizi wachezaji wazuri kama kina De Bruyne wanaishia kucheza Man City au PSG.

Hii ndio halisi. Wachezaji wengine kutoka Amerika Kusini ambao ni mastaa wakubwa kama Neymar hawaoni shida kuondoka Barcelona na kwenda katika timu ambazo hazina historia nzito.

Matajiri wa Barcelona na Real Madrid inabidi wapambane kweli kweli kuturudishia mastaa wakubwa wenye hadhi katika mechi ya El Clasico.

Nyakati fulani ungeweza kutazama El Clasico na kugundua uwanjani kulikuwa na mwanasoka bora wa dunia wa mwaka juzi, mwaka jana, mwaka huu na ambaye alikuwa anatarajiwa kuchaguliwa mwakani. Hii ndio maana ya El Clasico.

Vinginevyo kwa sasa tumegundua kwamba El Clasico haifiki katika urembo wa Cleopatra. Ni afadhali kutazama pambano la Liverpool na Manchester City utakutana na mastaa wengi ndani yake kuliko pambano la El Clasico.