Nonga: Majeraha yamenistaafisha
MBEYA. KILA jambo lina mwanzo wake na mwisho wake katika maisha ya binadamu yeyote katika ulimwengu huu wa mapambano kila kukicha katika kutafuta liziki.
Nahodha wa Mbeya City, Paul Nonga aliyetangaza kustaafu soka mara baada ya mchezo dhidi ya Yanga katita Uwanja wa Sokoine uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Nonga alianza soka la ushindani JKT Oljoro kisha akajiunga na Mbeya City akaenda Mwadui, Yanga, akarudi tena Mwadui, Lipuli, Gwambina na sasa Mbeya City amemaliza safari yake kama mchezaji.
NINI KINAMSTAAFISHA
Anasema sababu kubwa inayomfanya kuacha kucheza ni kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara hivyo akaona hataweza kudumu katika soka la ushindani.
Nonga anasema aliamua kutundika daruga katika mchezo huo sababu amezitumikia timu zote kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji hiyo ni heshima kwa timu hizo.
Amesema umekuwa wakati mwema kwake katika soka na sasa ataonekana uwanjani kwa majukumu mengine na sio kama mchezaji kama ambavyo wengi wamemzoea kwa muda mrefu.
"Nipende kumshuru Mungu kuniwezesha kufika hatua niliyonayo kwenye soka sababu sio wote wanamaliza salama safari yao ya soka kama mchezaji,”
"Pia niwashukuru viongozi wa Mbeya City kwa kunilea kama mtoto wao katika nafasi ya mchezaji na kunisomesha ukocha hadi leo hii najivunia na kusimama mbele za watu," anasema Nonga.
Nonga ambaye wazazi wake walipenda awe mchungaji anasema hakuweza kutekeleza mapendekezo ya wazazi sababu asingefurahia kazi hiyo na ndiko jina la 'Baba Paroko' lilikoanzia.
Mbeya City ni timu ambayo imenipa heshima na ndio timu ambayo imenifanya nikatambulika zaidi kwenye soka.
“Ukiangalia Yanga nayo imenisaidia kubadilisha maisha yangu kwa asilimia kubwa sana hadi leo hii naweza nikafanya jambo langu.”
Naondoka kama mchezaji lakini bado nipo kwenye timu kwa majukumu mengine ya soka ndani ya Mbeya City sababu nimesomeshwa na sasa mimi ni kocha.
JAMAA MSOMI
Kama unamchukulia poa Nonga kwa kuamini kuwa maisha yake anategemea soka tu basi unajidanganya na kupoteza muda wako bure kwani nyota huyo ni msomi.
Nonga anabainisha kuwa yeye ni msomi ngazi Stashahada na amesomea kozi ya kulipua miamba ambayo ingeweza kumpa ajira nje ya soka analocheza.
"Nina diploma ya madini, mimi ni mlipua miamba hivyo sina shaka yoyote, hata nikiamua kwenda kwenye ajira nje ya soka naweza kuishi vizuri."
Anasema elimu ni jambo la msingi hata kama unacheza halafu ukawa unataaluma nyingine nje ya soka hiyo inakupa upana zaidi katika maisha.
“Wengi wetu tunaelimu ya kawaida kitu ambacho sio kibaya lakini kujiendeleza ni bora sababu inakupa upana mkubwa wa kujua vitu nje ya soka.”
ATOA USHAURI
“Mafanikio tunayatafuta kwa njia tofauti na changamoto ni moja ya vitu tunavyokutana navyo, hivyo vijana wanapoingia huku lazima watambue hilo.
“Unaposhindwa kukabiliana na changamoto inakufanya kuwa na kiwango ambacho hakieleweki maana msimu huu unakuwa hivi na msimu ujao ukashuka.”
Nonga amesema kila mtu kwenye maisha yake ana kuwa na ndoto za kuwa mtu fulani hapo baadaye kama ambavyo wazazi wake walitaka awe paroko lakini akachagua soka.
Kutokana na ushindani wa soka na uwepo wa vipaji vingi amesema kama mtu anajiona soka ndio sehemu yake aliyochangua anapaswa kuiheshimu zaidi anapopatanafasi.
”Nidhamu ndio msingi wa kila kitu unachokifanya na wengi tumekuwa tunajisahau hasa kwa kuangalia umri na mwisho kupoteza kipaji.
“Usimamizi kwa wachezaji wetu imekuwa changamoto, wengi wanaotusimamia hawapo makini ndio maana hata maendeleo yanakuwa yakishuka kila kukicha,” anasema Nonga.
Anasema mchezaji anapokuwa na msimamizi mzuri inarahisisha mambo mengi katika kazi sababu kila mmoja anasimamia eneo lake lakini wengi hawapo hivyo.
“Wazazi wangu walipenda niwe padri na huko ndiko jina la ‘baba paroko’ lilikoanzia lakini sikuweza kutimiza ndoto za wazazi wangu maana nilitafuta ninachokipenda.
“Niliwashawishi wazazi kwa kuwaeleza ukweli lakini na mazingira nayo yalichangia sababu licha ya kufaulu kwenda shule ya seminari ya Itaga, Tabora niliwaeleza sitaweza na licha ya kwenda shuleni lakini sikudumu.”
WASIFU:
Jina: Paul Nonga
Kuzaliwa: Juni 18, 1989
Mahali: Morogoro
Uraia: Tanzania
Nafasi: Mshambuliaji
Klabu: Mbeya City
Alikopita: JKT Oljoro, Mbeya City, Yanga, Mwadui, Lipuli, Gwambina