NJIA NYEUPE : Tunasubiri kwa hamu ‘dabi’ ya watani wa jadi

Muktasari:

Miamba hiyo miwili yenye makazi yake Kariakoo itachuana katika ‘Dar Derby’ inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi ya Oktoba Mosi mwaka huu.

IMEBAKI wiki moja na ushee kabla ya pambano la watani wa jadi katika soka nchini, Simba na Yanga za Dar es Salaam zionyeshane ubavu.

Miamba hiyo miwili yenye makazi yake Kariakoo itachuana katika ‘Dar Derby’ inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi ya Oktoba Mosi mwaka huu.

Pambano hilo linatarajiwa kuwa la kukata na shoka litashirikisha timu kongwe zaidi nchini ambazo zimefikisha miaka 80 na linapaswa lionyeshe dhahiri ukongwe wa timu zinazohusika.Pambano hilo la wapinzani wa jadi ndilo linalotakiwa liwe la mfano kuliko mechi zote za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambayo inashirikisha timu 16.

Mechi ya Yanga na Simba haipaswi kuzungukwa na ushabiki wa hali ya juu tu kama ambavyo mara zote inaonekana, lakini pambano hilo linapaswa pia kutawaliwa na ufundi wa hali ya juu wa mchezo.

Makocha wakuu wa Yanga, Hans Pluijm kutoka Uholanzi na Mcameroon wa Simba, Joseph Omog, wanapaswa kuwaelekeza vizuri wachezaji wao ili mchezo huo wa wapinzani wa jadi uwe maridadi zaidi ikiwezekana kuliko mechi zote za Ligi Kuu.

Hii ndio njia pekee ya klabu hizo kuthibitisha kwamba wao ndio timu kongwe za soka nchini na mbali na kuwa na mashabiki wengi zaidi kuliko timu zote pia kandanda yao ni ya hali ya juu.

Itakuwa haina maana kwa Simba na Yanga kujivuna na kujigamba na wakati mechi yao itakuwa ni ya kubutua butua na kupiga mpira mbele bila ya kuonesha ufundi wowote.

Kwa maana hiyo wachezaji wa Simba na Yanga wasiingie katika mtego wa kugubikwa na hofu ya mechi na kuanza kucheza ovyo badala yake watuliane na waoneshe ufundi wao kwa kucheza mpira wenye pasi maridadi.

Watakuwa hawawatendei haki watazamaji watakaoufunika uwanjani iwapo watakuwa na mihemko wa kucheza ovyo na kufanyiana rafu zisio na msingi kwani jambo hilo halitadhihirisha ukongwe wao.

Watazamaji watakaokuwa uwanjani na mamilioni watakaoliangalia kupitia Televisheni wanapaswa kupata burudani safi na itatokea tu iwapo wachezaji wa timu zote mbili wataamua kuonyesha ufundi wa mchezo na kuacha papara papara zisizo na faida.

Hii ni nafasi murua kwa wachezaji wa Yanga na Simba kujitafutia soko na kuongeza thamani yao ya uwezo wao wa kucheza kandanda hasa ikizingatiwa pambano hilo kwa kawaida huwa linawavutia mawakala wanaowatafuta wachezaji kwa ajili ya kuwauza timu za nje.

Hayo ni kwa upande wa wachezaji lakini kwa upande wa waamuzi watakaopangiwa kuchezesha pambano hilo la watani wa jadi nao wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wanazifuata vyema sheria 17 za mpira wa miguu.

Waamuzi hao wanapaswa kuwa makini kuhakikisha kwamba wanafanya maamuzi ya haki na haki inaonekana katika maamuzi yao ili wasiwatoe wachezaji mchezoni na pia wasiamshe hasira kutoka kwa mashabiki.

Pamoja na kwamba kuna baadhi ya watu hawaukubali ukweli huu kuwa Simba na Yanga zina nafasi kubwa katika soka nchini kwa hiyo pambano lao linapaswa kuchukuliwa kwa hadhari kubwa kwa kila aliyehusika.

Kuanzia viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF), Bodi wa Ligi, klabu hizo, Waamuzi, Wachezaji na hata mashabiki kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili pambano hilo lisiwe na dosari.

Pambano hilo huwa linagusa mioyo ya Watanzania walio wengi na hata baadhi ya wananchi wa nchi jirani kwa hiyo linapaswa kucukuliwa kwa uzito wa hali ya juu ili liwe na mvuto unaolingana na hadhi yake.

Pamoja na wachezaji na waamuzi kutimiza wajibu wao uwanjani mashabiki nao hawana budi kuhakikisha kwamba wanakuwa watulivu na hawafanyi vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama. Utulivu wa mashabiki haina maana kwamba wasishangilie lakini wasifanye vitendo vya kuudhi wenzao kwani vitendo hivyo vina hatari ya kuzua fujo jambo ambalo litapoteza ladha ya mchezo huo.

Jeshi la Polisi nalo liwe makini katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama katika mchezo huo na kwa vile tiketi za kuona pambano hilo zinatarajiwa kuuzwa kwa njia ya Elektroniki badala ya kununua tiketi kwenye magari kama ilivyozoeleka hali inatarajiwa kuwa ya shwari.

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi TV Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020.