NIONAVYO: World Cup linaanza kuwa Kombe la Dunia

WATU husema mambo yanav yobadilika ndivyo yanavyorudi yalipokuwa.Timu inaifunga Argentina na kutangaza siku ya mapumziko nchi nzima.Tukio la kwanza lilikuwa ni ushindi wa mabao 4-2 wa Uruguay dhidi ya Argentina kwenye fainali za kwanza za Kombe la Dunia na la pili ni ushindi wa Saudi Arabia wa mabao 2-1 dhidi ya Messi na Argentina katika Kombe la Dunia linaloendelea Qatar. Argentina imekuwa ni muhanga wa matokeo ya kushangaza kwani mwaka 1990 wakiwa mabingwa watetezi na Diego Maradona wao walifungwa 1-0 na Cameroon, jambo lililoishangaza sana dunia.

Mashindano ya kwanza ya Kombe la Dunia yalizikutanisha timu za Ulaya na Amerika Kusini. Kwa miaka mingi ilionekana kuwa mashindano hayo yataendelea kuandaliwa na kutawaliwa na nchi za Ulaya na Marekani Kusini huku Ulaya ikiwa na faida ya kuingiza timu nyingi na pia kuwa na timu nyingi zenye uwezo wa kiuchumi wa kuandaa mashindano hayo.

Sidhani kama waanzilishi wa mashindano hayo waliwahi kutegemea kuiona timu ya taifa la Kiafrika Cameroon ikiwafunga mabingwa watetezi Argentina mwaka 1990, au timu ya Taifa la Kiafrika Senegal ikiwafunga Mabingwa Watetezi Ufaransa mwaka 2002, Taifa la Kiarabu la Afrika ya Kaskazini Tunisia wakiifunga Mexico mwaka 1978, Saudi Arabia ikiwafunga Argentina mwaka 2022, Japan haikutegemewa kuifunga Ujerumani 2-1 mwaka 2022. Orodha ya matokeo ya kushangaza itaendelea na kuendelea kwani mpira sasa ni utamaduni wa dunia nzima, hauna mwenyewe.

Kadhalika, waanzilishi wa fainali za Kombe la Dunia wakati wanakaa mwaka 1928 kuanzisha mashindano ya mwaka 1930 nchini Uruguay hawakutegemea kuwa siku moja nchi za Asia (Japan na Korea Kusini) zingekuwa wenyeji wa mashindano haya mwaka 2002 au Afrika Kusini 2010 na hata taifa dogo sana la ghuba ya Kiarabu lenye wazawa wasiofika milioni mbili, Qatar lingeweza kuandaa mashindano hayo yanapofikisha miaka 92.

Kadri Kombe la Dunia la Qatar 2022 linavyoendelea tutegemee kuona rekodi zikiwekwa na mataifa ambayo hapo awali hayakuchukuliwa kama ni mataifa ya mpira (footballing nations) na vilevile ubabe wa mataifa kama Brazil, Ujerumani, Italia na Ufaransa unaweza kupungua kutokana na kuongezeka kwa ushindani na kuongezeka kwa idadi ya washiriki kuanzia Kombe la Dunia litakaloandaliwa Amerika ya Kaskazini (Canada, Marekani na Mexico).

Sababu nyingi zimechangia mabadiliko tunayoyashuhudia leo. Kazi ya umisionari wa mpira iliyofanywa na mataifa ya kikoloni ya Ulaya ikiwa ni sehemu ya kueneza utamaduni wao. Mataifa kama Ufaransa, Uingereza, Ureno na Hispania yaliueneza mchezo wa mpira wa miguu na kuendesha mafunzo katika makoloni yao.

Mfumo wa mpira wa kulipwa na uhitaji wa wachezaji wa kutoka nje ya Ulaya kucheza katika timu kubwa za Ulaya hasa kwenye mataifa makubwa kimpira kama Hispania, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mataifa kama Senegal na Japan timu zao zinaundwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wanaotafuta mkate wao huko Ulaya hivyo wana uzoefu (exposure) ya mpira wa Ulaya na hivyo hawapati ugumu sana wanapokutana uwanjani na timu za mataifa ya Ulaya.

Shirikisho la Soka (FIFA) lenye makao makuu katika Jiji la Zurich, Uswiss kwa miaka mingi limeendesha miradi mbalimbali ya maendeleo ya mpira. Miradi hii ni pamoja na soka la vijana, uamuzi, tiba, utawala, uamuzi, biashara, miundo mbinu ya mpira n.k. Miradi hii imefanyika duniani kote hivyo mpira wa dunia unafanana katika vitu vya msingi.

Teknolojia na utandawazi pia vimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tofauti ya mbinu na ufundi wa mpira unaochezwa katika mataifa mbalimbali.Siku hizi mtu mmoja anaweza kufuatilia timu pinzani na kujua mbinu zake na wachezaji wake akiwa amekaa kwenye kiti chake nyumbani. Ndani ya siku moja mtu anaweza kuangalia kupitia runninga michezo ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Ufaransa, Afrika Kusini, Uingereza na hata Brazil. Hivyo yale ‘maajabu’ kutoka Amerika ya Kusini na Ulaya yataendelea kupungua kadri mpira unavyozidi kuwa sehemu ya utamaduni wa mataifa yote duniani. Sitashangaa Kombe la Dunia la mwaka huu likishuhudia timu zisizotegemewa au ambazo hazijawahi kufika nusu fainali zikifika huko na hata fainali. World Cup sasa limekuwa Kombe la Dunia haswa. Mwandishi wa safu hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na mtaalam wa masuala ya soka. Niandikie maoni yako kupitia namba hiyo hapo juu.