NIONAVYO: Nusu fainali Simba, Yanga inawezekana

TANZANIA imefanikiwa kuingiza timu mbili hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Si jambo lililozoeleka sana, hasa kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa hesabu rahisi, robo ya timu zilizobaki katika hatua hii ni timu za Tanzania.

Msimu uliopita timu hizi zilifikia hatua hii kwa pamoja, lakini Yanga walikuwa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho ambalo ni shindano la chini kwa hadhi kulinganisha na Ligi ya Mabingwa Afrika. Baada ya Simba kutolewa na Wydad Casablanca, wenzao Yanga walienda hadi fainali na kupoteza mbele ya USM Alger kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini.

Hakuna aliyetegemea timu hizi zingerudia jambo la mwaka jana au kwenda zaidi. Ni ukweli usiopingika kwa sasa hakuna timu inayojisikia vizuri kupangiwa Simba au Yanga katika ngazi yoyote.

Pamoja na kuingiza timu mbili, Ijumaa Kuu na Jumamosi katika kipindi cha Pasaka mambo hayakuwa mazuri kwa Tanzania kwani si Simba waliocheza Ijumaa dhidi ya Al Ahly ya Misri au Yanga iliyocheza Jumamosi dhidi ya Mamelodi Sundowns iliyopata ushindi. Simba ilipoteza kwa kufungwa na Al Ahly kwa bao 1-0 na Yanga ikatoka suluhu na Sundowns.

Simba, pamoja na kupoteza mchezo wao dhidi ya Al Ahly, unaweza kusema kwa ufupi timu bora ilipoteza. Walikuwa wazuri kila sehemu na takwimu zote zilikuwa upande wao isipokuwa bao moja walilofungwa katika dakika za mwanzo za mchezo.

Huu ulikuwa miongoni mwa michezo ambayo Simba walicheza sana msimu huu, lakini udhaifu katika kuweka mpira wavuni ukawafanya wakubali kulala nyumbani.

Laiti kama si aibu yao mbele ya lango, Simba wangetoka na ushindi mnono dhidi ya Al Ahly. Ukiondoa kosa lililozaa bao, Simba ilikuwa vizuri sana kuanzia kwa kipa, mabeki na viungo. Kipa wa Simba, Ayoub Lakred alikuwa mapumzikoni katika sehemu kubwa ya mchezo ukilinganisha na Mostafa Shoubir wa Ahly ambaye alifanya kazi ya ziada kuwazuia Simba wasilione lango.

Mchezo wa Yanga dhidi ya Mamelodi, kwa waswahili ungesema, uliboa. Haukuwa mchezo wa kuvutia kwa sababu ni mchezo uliotawaliwa na mbinu zaidi kiasi cha kuonekana kama timu zilikuwa zinaogopana. Yanga ikikabiliwa na majeraha ya wachezaji nyota kama Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na Khalid Aucho ilichagua kuachia umiliki wa mpira kwa Mamelodi huku ikiziba mianya ambayo Mamelodi wangeitumia kuliona bao. Mamelodi walimiliki sana mpira, lakini katika upande wa bao lao, wakiongozwa na kipa Ronwen Williams.

Yanga ilisubiri ikitafuta kufunga kwa mashambulizi ya kushtukiza lakini haikuwa vizuri sana na karibu mara mbili ilizokaribia kuliona lango, kipa Williams alikuwa ni kikwazo. Matokeo yake mpira ukaishia suluhu kama zilivyokuwa mechi zote za mkondo huu isipokuwa ile ya Simba na Ahly.

Matokeo ya michezo ya kwanza kwa mashabiki wa Simba na Yanga hayakuwa ya kuridhisha sana. Mashabiki, hasa wa Simba wakilalama dhidi ya viongozi laiti wangelikuwa makini kufanya usajili wa maana katikati ya msimu basi mchezo ule ungekuwa riziki yao. Kuna mashabiki wanaona kwa kiwango cha siku ile kama Simba ingekuwa na washambuliaji wao walioondoka yaani Jean Baleke na Moses Phiri ingeweza kufanya kitu cha ziada na kuwa na uhakika wa kusonga mbele. Kuna mashabiki pia wanahoji kutotumika kwa washambuliaji wao wapya Pa Jobe na Freddy Michael.

Kwa mashabiki wa Yanga, labda kutokana na kutambua ugumu uliopo kucheza na Mamelodi au kwa kujua hali ya majeruhi iliyokuwa inawakabili, wengi wanaonekana kutokatishwa tamaa na uchezaji wa timu yao. Bila shaka kila shabiki hupenda timu yake ishinde, lakini mashabiki wa Yanga ni kama wanaona heri nusu shari kuliko shari kamili.

Wakati mashabiki wa Simba wakisikitika na matokeo ya mchezo wa kwanza, mashabiki wa Ahly bado wana kitete na mchezo wa nyumbani. Bila shaka Ahly wanayaangalia marudio ya mchezo wao wa Benjamin Mkapa na kugundua siku hiyo ni kama Mungu alikuwa upande wao. Bahati ilitabasamu upande wao. Pamoja na hilo, Ahly kwa siku za karibuni kiwango chake ni kama kimeshuka kiasi na mashabiki wake hawana uhakika sana wa kushinda nyumbani. Ikumbukwe mwanzoni mwa msimu Ahly ilikutana na Simba katika robo fainali ya michuano mipya ya Ligi ya Afrika (African Football League) na matokeo yalikuwa sare Dar es Salaam na Cairo, hivyo Ahly kusonga mbele kwa faida ya kufunga mabao mengi ugenini. Historia hiyo inawanyima usingizi Ahly ambao katika miaka ya nyuma ilikuwa kushinda nyumbani kwao ni lazima.

Huko Afrika ya Kusini mashabiki na wapenzi wa Mamelodi waliyachukua matokeo ya timu yao kwa hisia tofauti. Kuna wanaofurahhi kwamba suluhu ya ugenini ni matokeo chanya. Wako wanaokoshwa na ukweli Mamelodi ilikuwa timu bora, hasa katika umiliki wa mpira katika mchezo wa Benjamin Mkapa mbele ya maelfu ya mashabiki wa Yanga.

Hata hivyo, uzoefu wa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Wydad Cassablanca katika mashindano haya msimu uliopita unaamsha kengele ya onyo. Katika msimu uliopita ngazi ya nusu fainali Sundowns walikutana na Wydad iliyoonekana dhaifu baada ya kuitoa Simba kwa changamoto ya mikwaju ya penalti katika robo fainali.

Baada ya kutoka suluhu ugenini, Mamelodi walidhani kulikuwa na faida ya kuwa nyumbani lakini matokeo hayakuwa hivyo kwani timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na hivyo Sundowns kutolewa mashindanoni bila kupoteza mchezo wowote.

Mchezo wao na Yanga ni kama unarudisha picha hiyo. Tayari Kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena amelalamikia mbinu za wapinzani wao Yanga alizoziita za ‘kupaki basi’ na kusema analazimika kuja na mbinu mbadala ili kushinda mchezo wa leo.

Mambo hayatakuwa rahisi kwa Sundowns ambayo pamoja na kuchukua ubingwa wa ligi ya DSTV mara sita mfululizo, bado haikubaliki sana kama wapinzani wao wasiofanya vizuri yaani Chiefs na Pirates.

Tofauti na wasiwasi uliotanda hapa nchini, kwingineko Afrika Mashariki na dunia kwa jumla, wachambuzi na wafuatiliaji wa mashindano haya wanashangazwa na kupanda kwa kiwango cha uchezaji wa klabu za Tanzania. Wanaiona Tanzania kama nchi ya kuchungwa katika mpira wa klabu.

Mchambuzi mmoja kutoka Afrika ya magharibi anadai kuona dakika chache za mchezo wa Yanga na Mamelodi na kushangazwa na mbinu zilizoonyeshwa katika mchezo huo lakini zaidi anashangazwa na mapenzi ya Watanzania kwa mpira wa miguu.

Nionavyo mimi, timu za Tanzania bado zina nafasi ya kusonga mbele katika mashindano haya. Binafsi, sitashangaa sana hata kuona timu mojawapo inaingia fainali.Kuingiza timu mbili robo fainali halikuwa jambo la kubahatisha.

Kwa siku za karibuni, uwezo wa klabu za Tanzania umepanda kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika hasa kwa Simba na Yanga na kwenye Ligi Kuu Bara. Kama Simba na Yanga wataamini na kujituma na kufuata maelekezo ya walimu wao, sioni sababu kubwa sana ya kuwafanya wasisonge mbele. Michezo ya kwanza ilipita na wanatakiwa kuiweka nyuma ya akili yao huku wakifanyia kazi udhaifu wao na kutumia mianya waliyoiona kwa wapinzani wao ili waweze kupata ushindi katika michezo yao ya usiku wa leo.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU ZIBARIKI SIMBA NA YANGA.

Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.