NIONAVYO: Afcon 2027 inagonga hodi, mlango uko wazi?

New Content Item (1)
New Content Item (1)

NI wiki chache zimepita tangu kutamatika kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) yaliyofanyika Ivory Coast.

Mnyonge mnyongeni, sikwenda Ivory Coast lakini nilifuatilia kwa karibu mashindano hayo na Ivory Coast walikuwa ni wenyeji wenye mafanikio.

Shuhuda za walikokuwa kule na zaidi wenye mashindano yao, yaani Shirikisho la Soka Afrika (Caf) walisifia namna wenyeji walivyofanya kazi nzuri. Rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe alifika hatua ya kumwambia Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Giani Infantino, sasa Ivory Coast ina uwezo wa kuandaa Fainali za Kombe la Dunia. Sifa zote hizo haziwezi kuwa zinatoka hewani bali watu wamefanya kazi kwelikweli.

Watu walijipanga hasa. Mashindano ya Afcon 2025 yanatarajiwa kufanyika Morocco, nyumbani kwa wababe pekee wa Afrika waliofika nusu fainali za Kombe la Dunia 2022.

Ufalme wa Morocco una uzoefu wa kuandaa mashindano na matukio makubwa kwa jumla hivyo kwao haya wanayamudu. Ikumbukwe pia Morocco ilikuwa mtahiniwa wa kuandaa Kombe la Dunia 2026 ambako ilizidiwa kidogo na maombi ya pamoja ya Marekani ya Kaskazini, yaani Canada, Mexico na Marekani (USA).

Afrika Mashariki kupitia maombi ya pamoja ya Kenya, Tanzania na Uganda imepewa uenyeji wa Afcon 2027. Hii ni mara ya kwanza Afrika kwa mataifa kuomba kuandaa mashindano kwa pamoja (joint bid). Maombi ya pamoja yatakuwa yalisukumwa na ukweli, Afrika Mashariki imekuwa ikipata ugumu wa kuandaa mashindano makubwa ya Caf na Fifa kutokana na sababu nyingi ikiwemo fedha, miundombinu mbalimbali na uzoefu wa kuandaa.

Kwa miaka ya karibuni, mashindano ya soka ya Afrika kwa timu za taifa, hapa Afrika Mashariki yalifanyika Tanzania, nayo ni Afcon ya vijana (U17) ya mwaka 2019. Kwa kuja pamoja mataifa hayo matatu, yamefanikiwa kuwa wenyeji.

Nadhani ni wakati mwafaka kwa mataifa haya kuanza kujiangalia kabla hata ya vumbi la Ivory Coast kutulia. Najiuliza sana tena na tena. Tuko tayari kufanya walichofanya Ivory Coast kama nchi na mabingwa wa soka wa Afrika?

Kuandaa mashindano kwa pamoja kunaweza kuwa rahisi na vigumu pia. Ni sawa na ndugu watatu ambao kila mtu ana mji wake kupewa uenyeji wa mgeni mmoja kwa pamoja. Kuna mtihani kupanga atapata staftahi wapi, chakula cha mchana wapi na cha jioni kwa nani. Mgeni atalala kwa nani, ataoga kwa nani. Kuna mtihani kupanga nani atalipia gharama za chakula, nani atakwenda kununua chakula. Mgeni ataanzia kwa nani na ataondokea kwa nani. Nani atampokea mgeni na nani atamsindikiza kwenda stendi, bandarini au uwanja wa ndege. Unaweza kuona ndugu hawa wamegawana mzigo wa majukumu lakini wanatakiwa kutumia akili sana na mawasiliano ya mapema ili kupangiana jinsi ya kutekeleza majukumu bila kukwama wala migongano pindi mgeni atakapowasili.

Huo ndio mtihani wa kuandaa mashindano na zaidi mashindano ya pamoja. Maombi ya pamoja yana nguvu ya ushawishi lakini maandalizi ya pamoja yanahitaji weledi na busara kuliko hata uenyeji wa taifa moja.

Nimekuwa nikikumbana na maswali mengi kuhusu maandalizi ya Umoja Afcon 2027, lakini kwa kuwa sina habari za jikoni niliishia kuwatia moyo watu wenye wasiwasi.

Baada ya maswali kuzidi nilimtafuta Mtanzania mmoja mwenye uzoefu na masuala ya uandaaji matukio na akanieleza jinsi ambavyo angefanya kama yeye angejikuta anahusika na maandalizi ya mshindano haya makubwa na ambayo kwa mara ya mwisho yalifanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki mwaka 1976, Ethiopia.

Ukibebwa nawe ubebeke. Afrika Mashariki inatakiwa kutambua ukweli, walipata nafasi hiyo kama si kwa huruma basi ni kwa lengo la kueneza maendeleo ya soka na kama si hilo ni kwa malengo ya siasa za soka yaani kupata kura za ukanda huu. Afrika Mashariki wakishajua ubavu wao ulikuwa mdogo kulinganisha na mataifa waliyoshindana nao kuwa wenyeji basi watahakikisha hawalali ili waliodharau wapatwe na aibu. Kufanikisha hilo si jambo la mzaa.

‘Kamwe muda haumsubiri mtu’ ananiambia mkongwe huyu wa utawala wa soka. Anasema muda hauko upande wetu hasa ukizingatia wenyeji hawa wa Afcon hawana uzoefu mkubwa sana wa kuandaa matukio ya kiwango cha juu. Ilitakiwa hadidu za rejea ziwe zimeorodheshwa tayari huku kila mdau kwenye kamati ya maandalizi ya ndani (Local Organising Committee/LOC) akijulishwa wajibu wake. Kamati ya kitaifa ingefanya kazi kwa karibu na kamati ya pamoja (Afrika Mashariki) ili CAF wanapokuja na kamati ya mashindano haya kamati za ndani za kitaifa na ile ya pamoja ziwe zimekwisha kupiga hatua kubwa. Kamati ya pamoja inatakiwa kuungaanisha mawazo ya kamati tatu za kitaifa na kuangalia wapi pamekaa sawa na wapi bado. Mfano masuala kama ya nchi na uwanja utakaokuwa mwenyeji wa ufunguzi wa mashindano, robo fainali, nusu fainali na fainali.

Miundombinu ya viwanja ni muhimu sana kwa mashindano haya kwa jumla. Sikubahatika kuona nyaraka za kuomba uenyeji lakini ni muhimu kuhakikisha kuna viwanja ambavyo viko kwenye matumizi tayari vinavyoweza kutumika kama mbadala endapo (hili hatuliombei) viwanja vilivyo kwenye makabrasha vitashindwa kukamilika kwa wakati.

Imewahi kutokea huko nyuma ambako mashindano yalilazimika kuchelewa au kuhamishiwa nchi nyingine baada ya wenyeji kuchemsha.

Usafiri na hoteli kwa timu na menejimenti ya mashindano ni muhimu sana. Pia mashabiki, wapenzi na hata watalii wangependa kujua namna  usafiri uwe wa ndege, barabarani, reli na hata meli utakavyokuwa. Watu wapate uhakika wa sehemu nzuri ya kulala katika miji wenyeji.

Menejimenti ya mashindano kitaifa (ingekuwepo) inatakiwa kuwasiliana na wizara na idara za kiserikali zinazohusika kwa wakati mfano idara ya uhamiaji kuhakikisha wageni wana uhakika wa viza za kuingia katika nchi husika. Idara za usalama ni wadau muhimu sana kama ilivyo idara zinazohusika na forodha kama. Kwa jumla ziko wizara na idara nyingi za serikali zinazohusika katika zoezi zima la kufanikisha uenyeji wa mashindano makubwa. Majukumu mengi ya kiserikali yanahitaji mawasiliano ya mapema sana kwani kuna mlolongo wa itifaki unaotakiwa kufuatwa kwa mfano kuondoa ushuru kwenye vifaa vya kimichezo na vinginevyo vitakavyoingia katika mataifa haya, kuondoa viza, utaratibu wa chanjo na masuala mengine ya kiafya. Serikali kamwe haziwezi kushtukizwa.

Mafanikio ya maandalizi ya Afcon 2023 yaliyofanyika katika miji mitano ya Ivory Coast ni changamoto kwa Afrika Mashariki. Kuunganisha watu, fedha na raslimali nyingine kuelekea Afcon si jambo rahisi japo linawezekana. “Tunataka kufanya mashindano yatakayoacha kumbukumbu katika vichwa vya mashabiki na athari chanya katika miundombinu ya michezo, hoteli na huduma nyingine,” alinukuliwa akisema Mwenyekiti wa Kamati ya ndani ya maandalizi ya Afcon, Ivory Coast (COCAN), Francois Albert Amichia.

Afrika Mashariki hii yenye viwanja visivyozidi vitatu vyenye hadhi ya Fifa inatakiwa kukimbia pale ambapo wengine wanatembea.

Kupata uenyeji wa mashindano makubwa ni jambo ambalo kila nchi inalitaka. Ni jambo ambalo mataifa hutumia ushawishi wote na wakati mwingine kampeni chafu kuhakikisha wanapata. Kuandaa mashindano yenye mafanikio ni jambo jingine kabisa. Nionavyo mimi, gari la maandalizi ya Afcon Afrika Mashariki 2027 halijashika kasi inayotakiwa. Nini kitaamua? Kuona thamani ya kila nukta ya muda mfupi uliobaki, kukusanya fedha za maandalizi, kuhakikisha miundombinu ya mpira na mingineyo kama hoteli iko sawa lakini zaidi ya yote kuwa na kamati mahiri za maandalizi (Local Organising Commitees) kitaifa na ile ya Afrika Mashariki. Maajabu tunayotarajia yatategemea lini zinaundwa hizi kamati, nani wanaunda hizi kamati na mazingira na ushirikiano watakaopewa na mashirikisho ya soka ya TFF, FKF, FUFA, pia serikali na umma wa mataifa hayo matatu.

La mwisho japo si kwa umuhimu, ni mataifa ya Afrika Mashariki kuhakikisha yanaandaa timu zao za taifa kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo. Kwa kuwa wenyeji, The Cranes, Harambee Stars na Taifa Stars hawataangaika na mtoano.

Hata hivyo, ukiondoa Uganda iliyowahi kufika fainali miaka 46 iliyopita, Tanzania na Kenya wamekuwa wakiishia hatua ya makundi ya Afcon. Hakuna jambo baya kama mwenyeji wa mashindano kuondolewa mapema. Bila mwenyeji mashindanoni, nguvu ya umma nyuma ya mafanikio ya mashindano haiwezi kupatikana. Itakuwa sawa na kumwandalia mgeni karamu nzuri, ukamwacha mezani anakula halafu wewe ukaenda kuchungulia dirishani anavyokula na kufurahia karamu uliyoiandaa wewe. Hili ni jukumu la watu wa ufundi na ni jukumu linalohitaji muda kulifanikisha. Bahati mbaya muda hauko upande wetu.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka  Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kwa simu yake hapo juu.