NINAVYOJUA : Tuelekeze akili zetu sasa kwenye mechi ya Uganda

Muktasari:

  • Inawezekana kocha Emmanuel Amunike akawa pekee na Watanzania wachache ambao mawazo yao yapo kwenye mchezo huo huku wengi wakiwa wanaishi kwa matukio tu ikifika wakati huo ndipo wataanza kuzungumzia kuhusu mchezo huo unatarajiwa kufanyika mwezi wa tatu.

KUNA mambo mengi kwa sasa yanaendelea nchini yanayohusu soka ambayo tayari yameshatuhamisha kutoka kwenye kuuwaza mchezo wa mwisho wa kufuzu kwenda hapo Misri kwenye fainali za AFCON mwaka huu.

Inawezekana kocha Emmanuel Amunike akawa pekee na Watanzania wachache ambao mawazo yao yapo kwenye mchezo huo huku wengi wakiwa wanaishi kwa matukio tu ikifika wakati huo ndipo wataanza kuzungumzia kuhusu mchezo huo unatarajiwa kufanyika mwezi wa tatu.
Kuna michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo kwa kiasi inaweza kuwa imehamisha mawazo ya wengi, lakini pia kuna maandalizi ya fainali za Afcon kwa vijana chini ya miaka 17 fainali zitakazofanyika nchini mwaka huu mwezi wa nne na kwa kiasi maandalizi haya yamechukua sehemu kubwa ya mawazo ya Watanzania.

Sikushangaa nilipomuona Mkurugenzi wetu wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania, Ammy Ninje akizunguka nchini kuangalia namna ya kupata wachezaji bora wenye maumbile mazuri kama nilivyowahi andika huko nyuma juu ya uchaguzi za wachezaji wanaunda vikosi vya vijana kutozingatia hili la maumbo.

Ni dhahiri Mkurugenzi wetu ametilia maanani zaidi namna ya ujenzi wa timu hizi za vijana. Kwa mana hii inaonyesha jinsi watu wengi tulivyosahau kufuatilia maandalizi ya mchezo huo na kutengeneza mikakati yake kuelekea mchezo huu.

Kuna michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika kwa upande wa klabu nayo yamechukua akili zetu kabisa, michuano hii ambayo klabu ya Simba inashiriki kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2003, imeshatuchukua akili na kila kitu huku tukisahau kuzungumzia hata kidogo kuhusu mchezo huo wa mwisho kwenye kundi letu dhidi ya Uganda.

Lakini haya yote si mageni kwetu labda hili la maandalizi ya Afcon 2019 kwa vijana chini ya miaka 17 na sisi tukiwa ni wenyeji wa michuano hiyo. Ukiacha hilo, haya ya Ligi Kuu na michezo inayoendelea ni kawaida tu na hili la Simba si geni kwetu kwa kuwa Simba imeshashiriki na itaendelea kushiriki na ukizingatia njia ya kufikia hatua hiyo waliopo Simba si ngumu sana kwa upande wa klabu ni namna ya kujipanga tu.

Unapozungumzia ushiriki wa nchi kwenye michuano hii ya Afrika ikizihusisha nchi, unazungumzia michuano mikubwa kabisa Afrika na dunia kwa ujumla , hii michuano sisi kama nchi tumeshiriki mara moja tu huku wenzetu wakiifanya michuano hii kama sehemu ya maisha yao ya kawaida wakishiriki kila uchwao huku sisi tukiendelea kuitizama tu.

Hatutakiwi kulala kipindi hiki ambacho michezo hiyo ya mwisho ikiwa inakaribia, sioni jinsi gani tunavyojitayarisha kimawazo kabla ya kufikia muda huo sidhani kama kuna kitu kinafanyika labda kwa kuwa siijui akili ya Amunike.

Binafsi kwenye hili najaribu kutafakari jinsi tulivyo shindwa kufanya vizuri dhidi Lethoto kwenye michezo yetu miwili na ule dhidi ya Cape Verde nikiona kabisa ndiko tunakokwenda kushindwa, sijui kama kocha Amunike alishagundua na kuona afuatilie hili la viwango vya wachezaji wanavyocheza sasa kwenye Ligi Kuu na michezo mingine ya kimataifa kama inavyoshiriki Simba na hapo awali Mtibwa.

Sipendi kuona kocha mkuu anaonyesha kukariri kwenye chaguzi za wachezaji wake bila kuzingatia mabadiliko yao uwanjani na Ubora wanaoendelea kuuonyesha.
Itakuwa dhambi kubwa iwapo Amunike atakuwa yupo akiangalia viwango vya wachezaji lakini mwisho wa siku kwenye chaguzi zake za kikosi kitakachoitwa na mwisho kinachokuja kucheza siku ya mwisho hivi ndivyo vitakavyomuangusha Amunike.

Niangalia sana jinsi alivyoshindwa kutengeneza vizuri eneo la ulinzi kwa kutokuwa na msimamo hasa baada ya kuwa amewachagua wachezaji, kwenye eneo la kulia bila shaka anamfuatilia sana Hassan Kessy na hilo halina ubishi huku mbadala wa Kessy kwa sasa akiwa hajulikani inaweza kuwa kwa mara ya kwanza tukamuona kijana mdogo wa Yanga, Paul Godfrey au kiasi kina Salum Kimenya ambaye kwangu huwa siuoni ubora wake zaidi ya kupiga krosi bado, kwenye kunyang`anya mipira sijui labda uzoefu kiasi, lakini yupo nyuma sana kwa kasi ya uchezaji.

Upande wa Kushoto huku aliko Gadiel Michael namuona akipungua ubora kila uchwao, Gadiel huyu si yule wa mwanzo ndivyo hivyo namuona Mohamed Hussein wa Simba akisogelea nafasi hii na si kwa sababu ya ubora tofauti lakini mwenzake huyu anamzidi mwenzake kwa kuwa anacheza kila mara. Kwa maana hii tunamtarajia Kocha Amunike na wasaidizi wake wawe wameshachekecha akili zao na kuja na mbinu mbadala kuelekea mchezo huo wa mwisho.