Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NETZER; Fundi wa Kijerumani asiyeishiwa mbwembwe, lakini nyavu zilimjua

KIJIWE Pict

Muktasari:

  • Mmojawao ni kiungo wa zamani wa Ujerumani, Gunter Netzer aliyeng’ara Ulaya wakati Ujerumani Magharibi ilipokuwa na wachezaji waliosifika kama Franz Beckenbauer, Gerd Muller, Hans-Georg Schwarzenbeck, Paul Breitner na kipa Sepp Maier.

WAPO wachezaji nyota wa kandanda hata wakistaafu au kuwa na umri mkubwa unaowapa tabu kuzungumza au kutembea bado hujiona kuwa wana mchango mkubwa katika mchezo huo. Baadhi yao haupiti muda mrefu bila kutoa ushauri au kulaumu uamuzi wa utaratibu mpya wa mchezo, hatua inayochukuliwa na klabu au timu ya taifa.

Mmojawao ni kiungo wa zamani wa Ujerumani, Gunter Netzer aliyeng’ara Ulaya wakati Ujerumani Magharibi ilipokuwa na wachezaji waliosifika kama Franz Beckenbauer, Gerd Muller, Hans-Georg Schwarzenbeck, Paul Breitner na kipa Sepp Maier.

Mapema Septemba, mwaka huu, Netzer aliilaumu Bayern Munich kwa kumchagua Uli Hoeness kuwa rais wa heshima wa klabu hiyo akidai ataichafua kwa sababu anapenda marafiki zake kuliko maendeleo ya mchezo wa kandanda.

Mara nyingi siku hizi mkongwe huyo huondoka Uswisi anakoishi na kwenda Ujerumani kuangalia michezo ya Bundesliga akiwa amefuatana na binti yake. Baadhi ya nyakati ikicheza klabu yake ya zamani ya Borussia Monchengladbach huhisi zipo dosari katika mchezo au ikiwa imeelemewa huenda kwenye chumba cha wachezaji wakati wa mapumziko. Awapo huko hutumia muda kutoa ushauri kutokana na uzoefu wake alipokuwa akisakata kabumbu, na huwaambia wachezaji kuwa hawawezi kufunga mabao na  wahakikishe nyavu zao hazitikiswi.

Mbali ya kuwa mchezaji mzuri, Netzer, aliyekuwa akicheza katikati kama kiungo alikuwa na mambo ya ziada yanayofanya asisahaulike. Mashabiki walimpenda kwa mengi. Mojawapo ni kuwa mtu mwenye umbo refu (futi 6 na inchi 3), nywele ndefu na miguu mirefu kuliko ya wachezaji wote wa Ujerumani wa wakati ule.

KIJI 01

Vyombo vya habari vilikuwa vikieleza kuwa umbile la Netzer halikutofautiana na twiga, na nguvu za mapaja zilimsaidia kupiga mashuti makali ya masafa marefu. Jingine lililompa umaarufu ni kwamba alikuwa mpole alipokuwa nje ya uwanja, lakini mwingi wa hasira ndani ya uwanja hasa alipohisi mwamuzi hakuitendea haki timu yake. Mara kadhaa alifungiwa kwa kuwachapa vibao wachezaji au kuwatukana waamuzi.

Siku zote kocha wake alipomaliza kutoa nasaha za mwisho kwa wachezaji kabla ya kuingia uwanjani, alimalizia kwa kumwambia Netzer: “Punguza hasira, utatuponza.” Naye alijibu kwa mkatao, “waambie wasinifanyie upumbavu.” Wajerumani wanamkumbuka kwa mambo aliyoyafanya siku ilipochezwa fainali ya 1973 ya Kombe la Ujerumani kati ya Borussia Monchengladbach na FC Koln. Siku ile, Netzer alikuwa anaumwa na alikwenda uwanjani akiwa amevaa suti na kukaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba.

KIJI 02

Timu hizo mbili zilikwenda muda wa ziada baada ya kumaliza dakika 90 za mchezo bila kufungana. Netzer aliondoka kwenye benchi na waliomuona walihisi alikuwa hajisikii vizuri na alikwenda kujisaidia au alikasirishwa na kuamua kwenda nyumbani. Lakini dakika tano baadaye alichomoza akiwa amevaa jezi na kumwambia kocha amtoe mchezaji mmoja ili aingie uwanjani.

Kocha alimshangaa na kumkatalia, lakini alipotishia kuwa atakuwa mchezaji wa 12 kama angelizuiwa, angeacha kuichezea tena klabu hiyo. Kocha alikubaliana naye na aliingia uwanjani huku akishangiliwa na mashabiki wa klabu yake. Haikuchukua zaidi ya dakika mbili baada ya kupewa mpira kufanya kile ambacho wenzake walikishindwa kwa dakika 90 kwani aliipiga chenga safu ya ulinzi ya FC Koln na kuachia fataki hadi wavuni.

KIJI 03

Mpira ulipowekwa katikati ili mchezo uanze, Netzer aliwapigia saluti wachezaji wenzake na watazamaji kisha akatoka nje. Bao hilo lilitosha kuiwezesha klabu yake kuchukua kombe. Gunter Theodor Netzer alizaliwa Septemba 14, 1944 katika mji wa Monchengladbach, Ujerumani. Alijiunga na Monchengladbach 1952 akiwa na miaka minane na kuhamia klabu nyingine ya mji huo, Borussia Monchengladbach 1963 akiwa na miaka 19.

Alianza kuwa mchezaji wa kulipwa na kucheza Bundesliga 1965–66 na mwaka huohuo aliitwa kujiunga na kikosi cha timu ya Ujerumani Magharibi ambayo aliichezea michezo 37 ya kimataifa kuanzia 1965 hadi 1975 na kuifungia mabao saba. Alikuwemo katika kikosi cha Ujerumani kilichobeba Kombe la Ulaya 1972, na alicheza kwa muda mfupi (dakika 21) wakati Ujerumani Magharibi ilipopambana na Ujerumani Mashariki, na anakumbukwa kwa namna alivyotawala mchezo katikati.

KIJI 04

Alipokuwa na timu ya taifa aliendelea kuichezea Borussia mpaka 1973 na kuteremka nayo uwanjani katika michezo 230 na kuifungia mabao 82. Alichaguliwa mchezaji bora wa mwaka wa Kandanda wa Ujerumani 1972 na 1973. Mwaka 1973, mchezaji wa kiungo maarufu wa Uholanzi, Johan Cruyff aliposajiliwa na Barcelona, Real Madrid nayo iliona lazima ipate mchezaji wa kiungo mzuri atakayemkaba Cruyff. Kwa hivyo, kocha wa Real, Santiago Bernabeu alimsajili Netzer na Paul Breitner, na usajili huu ulielezwa kama wa mchezo wa kuigiza kwa vile Netzer ni mrefu na Breitner mfupi sana.

Netzer aliichezea Real hadi 1976 na kuisaidia kuwa bingwa 1975 na 1976, na kuchukua Kombe la Hispania 1974 na 1975. Mwaka 1976 alikwenda Uswisi kujiunga na Grasshopper Zurich na kustaafu 1977. Baada ya kustaafu aliingia katika fani ya habari na mawasiliano na kuchapisha gazeti la Klabu ya Hamburger SV. Baadaye alikuwa kocha wa klabu hiyo na kubaki nayo kwa miaka minane iliyoshuhudia mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuchukua ubingwa wa 1979, 1982 na 1983 chini ya uongozi wake.

Hivi sasa Hamburger SV huelezwa kuwa klabu ambayo haijapata mafanikio makubwa katika nusu karne iliyopita kama ilivyokuwa chini ya uongozi wa Netzer. Mpaka hivi karibuni Netzer alijihusisha zaidi na matangazo ya biashara, utangazaji na kufanya uchambuzi wa kandanda katika runinga na alikuwa mmoja wa watangazaji maarufu wa soka wa Ulaya.

KIJI 05

Vilevile alikuwa na safu za kuchambua kandanda katika magazeti ya michezo kama Sport-Bild na Blick, na anaendesha biashara ya vifaa vya michezo. Pia alifungua kampuni ya matangazo ya biashara yenye makao makuu katika jiji la Zurich, Uswisi, ambako ndiko anakoishi. Mwaka 2003, Netzer alimkosoa kocha wa Ujerumani, Rudi Voller pale Ujerumani ilipotoka suluhu na Iceland na maelezo yake kuungwa mkono na karibu vyombo vyote vya habari vya Ujerumani. Mbali na tuzo za kucheza vizuri kandanda, Netzer pia alipewa tuzo za utangazaji na uchambuzi mzuri wa soka.

Mojawapo wa nukuu zake maarufu ni: “Rafiki mkubwa na adui namba moja wa kipa ni nguzo tatu za goli  mbili pembeni na mwamba. Ni rafiki zinapozuia mpira usiingie wavuni na adui zinapokubali kugongwa na kuuruhusu kutingisha wavu.”

Baada ya kufanyika mashindano ya fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini 2010, Netzer alitangaza kuiacha kampuni ya matangazo ya ARD aliyoitumikia kwa miaka 13 kwa maelezo kwamba alichoka kutumwa. Vilevile hatasahaulika kwa vituko vyake ndani na nje ya uwanja na atakumbukwa zaidi kwa kuvua suti akiwa mgonjwa, amekaa katika benchi la wachezaji wa akiba, akavaa jezi na kuingia uwanjani kisha kufunga bao la haraka lililoipatia klabu yake ushindi na kubeba kombe 1973.