Inashtua! Vifo hivi katika ngumi iwe darasa
Muktasari:
- Pia kule Ghana hivi karibuni alifariki dunia bondia mmoja, Ernest Akushey aliyefariki dunia siku 11 baada ya pambano ikielezwa kwamba kifo chake kilitokana na kipigo.
KWA miezi mitatu sasa upo mjadala mpana katika nchi mbalimbali na mashirikisho ya kimataifa ya mchezo wa ngumi juu ya usalama wa mabondia. Hali hiyo imekolezwa na vifo vya mabondia wawili. Mmoja aliaga dunia katika ulingo na mwingine hospitali katika mapambano tofauti yaliyofanyika Japan Agosti 2, mwaka huu.
Pia kule Ghana hivi karibuni alifariki dunia bondia mmoja, Ernest Akushey aliyefariki dunia siku 11 baada ya pambano ikielezwa kwamba kifo chake kilitokana na kipigo.
Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha masumbwi na mielekea ambayo ni miongoni mwa michezo hatari mara nyingi imezua mijadala juu ya athari zake na zipo nchi zilizopiga marufuku kwa muda au moja kwa moja. Hii imekwenda sambamba na kuweka sheria kali na tahadhari nyingi za kuepusha maafa kwa mabondia.
Serikali ya Cuba ilipiga marufuku ngumi za kulipwa 1961, lakini ikaruhusu Aprili 2022, na kuwaruhusu mabondia wa kulipwa kushiriki katika mapambano ya ndani na nje ya nchi. Mwaka 1981 Norway ilipiga marufuku na kukifunga Chama cha Ngumi za Kulipwa Norway, lakini ikaondoa zuio 2014 na kuweka vizuizi vingi ili kuhakikisha usalama wa mabondia.
Afghanistan ilipiga marufuku masumbwi na mieleka mwezi Agosti, mwaka jana, kwa maelezo kwamba michezo hiyo ni ya kibabe. Majimbo kadhaa ya Canada yamepiga marufuku ngumi za kulipwa na zile za riadha zimewekewa masharti kibao. Sweden nayo mara nyingi imekuwa ikipiga marufuku na kuondoa; mara ya mwisho ilikuwa 1970 na amri hiyo iliondolewa 2006.
Vifo vya mabondia wawili wa Japan vimesababisha Kamisheni ya Ngumi Japan kufanya uchunguzi ambao kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamisheni hiyo, Hagiwara Minoru na katibu mkuu Tsuyoshi Yasukochi utatakiwa kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuhakikisha usalama wa mabondia na hasa hatari zinazosababisha vifo.
Miongoni mwa hatua za mwisho zilizochukuliwa ni kupunguza urefu wa mapambano kutoka raundi 12 na kuwa 10. Vilevile mabondia watalazimika kupitia uchunguzi mzito wa uzito na afya karibu kila sehemu ya kiungo cha mwili ikiwamo uoni wa macho na uwezo wa kuhimili vishindo vya mchezo wa masumbwi.
Jingine linalozingatiwa ni kuongeza ukali wa adhabu kwa mabondia na waamuzi endapo watafumbia macho sheria na kanuni za mchezo. Hivi sasa nchi nyingi zinazingatia kupunguza urefu wa mashindano na hata muda wa mzunguko mmoja upunguze kutoka dakika tatu hadi mbili na sekunde 45 au dakika mbili na sekunde 30.
Hivi sasa, bondia akianguka mara tatu ulingoni mwamuzi hutakiwa kusimamisha mchezo na kumpa aliyemuangusha ushindi. Hili linazingatiwa na upo ushauri wa kwamba mara mbili inatosha. Suala la mabondia kujinyima chakula kwa muda ili kupunguza uzito nalo linaangaliwa kwa vile limeonekana kuchangia kudhoofisha afya ya baadhi yao.
Japokuwa hakuna takwimu sahihi, inakisiwa mabondia 2,000 wameshafariki dunia ndani ya ulingo au ndani ya wiki moja baada ya kukumbana na vipigo katika mashindano. Kifo cha kwanza ndani ya ulingo kurekodiwa ni cha bondia wa Mmarekani Andy Bowen katika karne ya 19 alipochapwa vibaya na kuangushwa chini katika mzunguko wa 18. Wakati ule kulikuwa hakuna ushindi wa alama na pambano lilikuwa linaendelea mpaka mmoja wao asalimu amri.
Tangu 2000 kumetokea vifo 33, sita kati ya hivyo nchini Marekani. Miongoni mwa vifo vya mabondia ndani ya ulingo vilivyoleta mshtuko mkubwa ni kile cha 2012 cha msichana wa miaka 18 nchini Mexico, Jeanette Zacarias Zapata ambaye alianguka na kufa hospitalini baada ya siku tano kufuatia kusukumiwa makonde mazito na Marie-Pier Houle wa Canada.
Kilichosikitisha ni kwamba uchunguzi ulionyesha alikuwa na matatizo ya uti wa mgongo aliyoyapata katika pambano la miezi minne kabla, lakini vyeti vyake vya vipimo vya afya vilighushiwa ili aweze kupigana na kujipatia pesa. Novemba 2021, kulitokea kifo ndani ya ulingo cha bondia kijana wa miaka 24 wa Zimbabwe, Taurai Zimunya, baada ya kupata majeraha ya kichwa.
Zimunya aliangushwa katika raundi ya tatu ya pambano la raundi sita alipozichapa na Tinashe Majoni ambaye pia ni raia wa Zimbabwe. Katikati ya pambano hilo mwamuzi alilaumiwa kwa kumuachia Majoni kuendelea kumpiga mwenzake kichwani licha ya kwamba alikuwa ameonyesha ishara za kusalimu amri, huku akijilinda kuonyesha hataki kuendelea na mchezo.
Ni kawaida kila mtu anayekwenda kuangalia masumbwi hutarajia kuona wanaochapana wakitoana jasho kwa kutwangana makonde mazito na kuonyesha ubora wa kuyakwepa. Lakini wakati mwingine utesaji huwa mkubwa hata kuwafanya watazamaji kumuonea huruma bondia aliyeelemewa.
Lakini, yapo mashindano ya mchezo huo ambayo badala ya kuwafurahisha mashabiki yamewahi kuwaudhi kwa vile yalichukua muda mfupi. Pia yapo ambayo mabondia walitwangana makonde kwa muda mrefu na hata kufikia wakati mashabiki wakitaka pambano limalizike kwa kuwaonea huruma mabondia kwamba wameteseka vya kutosha.
Pambano la masumbwi ambalo limeweka rekodi kwa kuchukua muda mrefu kwenye historia ni lile lililofanyika katika mji wa New Orleans, Marekani, Aprili 6, 1893 kati ya Andy Bowen na Jack Burke. Mabondia hao walipigana kwa saa saba na dakika 19. Pambano hilo lililoanza saa tatu usiku lilimalizika kwa mabondia hao kutoka sare kwa vile wote wawili walikuwa wamechoka na hawakuweza kuendelea kupigana.
Mchezo unaosemekana kuwa wa muda mfupi katika historia ni wa Mike Collins alipomuangusha Pat Brownson kwa konde la kwanza alilomrushia sekunde nne baada ya pambano kuanza katika Jiji la Minneapolis, Marekani, Novemba 4, 1947. Kwa ujumla vifo vya mabondia na juhudi zinazofanyika hivi sasa ni zinafaaa kutumika ili kuhakikisha usalama wa mabondia na kuwa darasa kwao na viongozi wa mchezo huo.