Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stewart Fundi wa mbio aliyekitisa riadha miaka ileee

Muktasari:

  • Haikuwa rahisi kutabiri nani angefika mwanzo kwenye utepe na kila walipopambana wacheza kamari walihangaika kutabiri ili kujipatia pochi iliyonona. Wakati ule Tanzania ilikuwa na wanariadha wake mashuhuri katika kundi hilo ambao nao waliitikisa dunia kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Ibrahim Juma, Juma Ikangaa na wengineo.

KATI ya miaka ya 1950 na mwanzoni wa miaka ya 1980 palikuwepo na kundi la wanariadha maarufu wa mbio za masafa ya kati na marefu ambao kila walipokutana katika mashindano ya kimataifa ilikuwa vuta nikuvute.

Haikuwa rahisi kutabiri nani angefika mwanzo kwenye utepe na kila walipopambana wacheza kamari walihangaika kutabiri ili kujipatia pochi iliyonona. Wakati ule Tanzania ilikuwa na wanariadha wake mashuhuri katika kundi hilo ambao nao waliitikisa dunia kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Ibrahim Juma, Juma Ikangaa na wengineo.

Scotland ilijivunia mwanariadha mmoja ambaye mpaka leo anatajwa kwa heshima kubwa kama mwanariadha nchini humo aliyetia fora na hajafikiwa kiwango chake mpaka leo huko kwao.

Huyu ni Ian Stewart aliyeshinda mashindano mengi ya kimataifa na ambaye sasa akiwa na miaka 76 anaendesha biashara yake ya duka kubwa la michezo nchini kwao Scotland na mara chache husikika akizungumzia riadha. Stewart alinyakua medali za dhahabu za mbio za mita 5,000 za Ulaya (1969), Jumuiya ya Madola (1970) na mbio za nyika za dunia (1975).

Vilevile aliweka rekodi ya Ulaya ya mita 5,000 mwaka 1970 kwa kutumia dakika 13 na sekunde 22:8. Aliwashinda Ron Clarke wa Australia aliyekuwa bingwa wa Olimpiki wa mbio zile, Kipchoge Keino wa Kenya na Mskochi mwenzake Ian McCafferty.

Stewart aliweka rekodi ya Uingereza ya mita 1,500 kwa kukimbia kwa dakika 3 na sekunde 39.12 (1969), mita 2,000 kwa dakika 5 na sekunde 2.98 (1975) na maili 2 kwa dakika 8 na sekunde 22.0 (1972). Baadaye alishinda medali ya shaba ya mita 5,000 katika michezo ya Olimpiki ya 1972 iliyofanyika Munich, Ujerumani Magharibi. Medali ya dhahabu ya mbio hizo ilichukuliwa na Lasse Viren wa Finland na ya fedha ilibebwa na Mohamed Gammoudi (Morocco).

Stewart alizaliwa katika mji mdogo wa Handsworth, Birmingham, Uingereza, Januari, 15, 1949 akiwa ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita ya John na Mary Stewart. Alipenda kukimbia tangu akiwa mdogo pamoja na kaka yake, Peter ambaye tayari alikuwa anashiriki mashindano ya shule na manispaa.

Alijiunga na kituo cha michezo cha Birchfield Harriers ambacho kaka yake tayari alikuwa mwanachama na haikumchukua muda mrefu alitambulika kuwa mwanariadha mzuri. Alikuwa bingwa katika mashindano ya vijana wa Midlands 1966 na alitokea wa pili katika mbio za nyika za taifa za vijana zilizofanyika katika mji wa Norwich, 1967.

Stewart, baada ya kusoma katika gazeti juu ya mafanikio ya mwanariadha maarufu wa mbio za maili moja wa Marekani wa zama zile, Jim Ryan, aliamua kumuiga kwa kukimbia maili 16 kila Jumapili asubuhi na 10 baadaye jioni katika Uwanja wa Perry Barr. Mazoezi hayo magumu yalimsaidia na amekuwa akisema ndiyo yaliyomwezesha kupata mafanikio katika riadha.

Mwaka 1969, akiwa na miaka 20, alishinda mashindano yake ya kwanza ya kimataifa kwa kumaliza wa kwanza katika mbio za mita 3,000 za ndani zilizofanyika Yugoslavia. Miezi mitatu baadaye alikimbia katika Uwanja wa Reading pamoja na kaka yake Peter na kuweka historia ya ndugu wawili wa kwanza duniani kukimbia maili moja kwa chini ya dakika nne. Hata hivyo mshindi wa mbio zile alikuwa Ian McCafferty.

Akiizungumzia siku ile ya historia, Stewart alisema baada ya kustaafu: “Nilifurahi na nilisikitika. Nilifurahi kwa kuweka historia, lakini nilisikitika kwa kuwa mtovu wa nidhamu kwa kumtangulia kaka yangu Peter, kwani yeye ndiye aliyestahili kuwa mbele kwa kuwa alizaliwa wa kwanza. Peter pia ndiye aliyenihimiza kuwa mwanariadha.”

Wiki tatu baadaye Ian Stewart alionyesha umahiri kwa kushinda mbio za mita 5,000 mjini Athens, Ugiriki kwa staili ya aina yake. Aliongoza wenzake kwa mita 3,000 za kwanza na baadaye aliamua kupunguza mwendo na kuwa karibu na mwisho - zaidi ya mita 20 alipokuwepo mtu wa mbele. Wanariadha wenzake na watazamaji waliamini alikuwa amechoka kwa vile alitumia nguvu nyingi mbio zilipoanza.

Lakini, zikiwa zimebakia mita 1,000 za mwisho aliongeza kasi kidogo kidogo na kuwarudisha nyuma yake mwanariadha mmoja baada ya mwingine. Zikiwa zimebaki mita 300 za mwisho alichukua tena uongozi hadi kwenye utepe kwa kuchomoka kwa kasi kama vile ndio kwanza aliingia uwanjani. Alitumia dakika 13 na sekunde 44.8.

Alipostaafu mwishoni mwa 1979 Stewart alijihusisha na kuendeleza riadha nchini kwao Scotland na baadaye alikuwa mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Raidha ambayo mwenyekiti wake alikuwa mmoja wa wanariadha mashuhuri wa Uingereza, Sebastian Coe aliyekuja baada ya Ian Stewart kustaafu. Vilevile alikuwa mtangazaji wa michezo wa vituo vya televisheni.

Mara nyingi Stewart amesikika akisema wanamichezo wengi wa siku hizi wakishapata mafanikio na kuwa maarufu kwao na nje huvimba vichwa na kujiona ni wao tu. Bahati mbaya badala ya kuendelea kujituma zaidi ili wafanye vizuri huporomoka haraka kutokana na kutumbukia katika dimbwi la starehe na anasa na kuwa na muda mfupi wa kufanya mazoezi.

Miaka 17 iliyopita jina la Ian Stewart liliingizwa katika ukumbi wa wanamichezo maarufu wa Scotland. Mpaka sasa hufanya mazoezi ya kukimbia mara tatu kwa wiki pamoja na wanariadha wa zamani aliokimbia nao katika mashindano ya nyumbani na nje miaka ya nyuma.