NDO HIVYO... KenGold inaanza upyaaa, mjipange!

Muktasari:
- Ken Gold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, haikuwa na mwanzo mzuri baada ya kushinda mechi moja, sare tatu na kupoteza michezo 12 katika michezo 16 iliyocheza ikiburuza mkia kwa kuvuna pointi sita.
TUNARUDI UPYAAA. Ni kauli ya vigogo wa KenGold wakitambia kikosi walichokisajili katika dirisha dogo lililofungwa juzi kwa kushusha mastaa wapya ambao wanaamini wataibeba timu katika ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara.
Ken Gold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, haikuwa na mwanzo mzuri baada ya kushinda mechi moja, sare tatu na kupoteza michezo 12 katika michezo 16 iliyocheza ikiburuza mkia kwa kuvuna pointi sita.
Hata hivyo, ni kama mabosi wa klabu hiyo wameshtuka kwa kulitumia dirisha dogo la usajili kuongeza wachezaji 24 ikiwatema wengine 11 ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wanarejea upya katika duru la pili.
Ken Gold ilianza msimu ikiwa chini ya kocha Fikiri Elias aliyeongoza takribani mechi saba na kuamua kutimka kikosini kufuatia matokeo ambayo hayakuwa mazuri, kisha wachimba dhahabu hao wa Chunya wakampa kwa muda kocha aliyeipandisha daraja hadi Ligi Kuu, Jumanne Challe kabla ya kumleta Omary Kapilima aliyeiongoza kushinda mechi moja tu, lakini yeye na msaidizi wake, (Challe) wakashindwa kuitoa mkiani hadi duru la kwanza lilipomalizika.

USAJILI HUU HAPA
Katika dirisha dogo KenGold imeonekana kuwa makini kujisuka upya kabla ya duru la pili kuanza mapema Februari baada ya michuano ya CHAN 2024 kusogezwa mbele hadi Agosti mwaka huu.
Timu hiyo imeongeza wachezaji wapya 24 wakiwamo nyota waliowahi kutamba na timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, huku pia ikivuka mipaka ya Tanzania kwenda kuvuta silaha mpya za maana.
Wachezaji waliosaini na wanaotarajia kuiongoza timu hiyo ni kipa Mohamed Yusuph aliyetokea Dodoma Jiji, Bernard Morrison ‘BM3’ aliyetamba na Simba na Yanga, Obrey Chirwa, Zawadi Mauya na Emmanuel Asante.
Wamo pia Mubashid Seidu (Ghana), Kyala Lassa (Zambia), Elnest Kwofie (Ghana), Kelvin Yondan, Mathias Juvilian, Nassir Bofu, Abdul Abdulai, Thompson Unachi (Nigeria) na Maulid Mbegu.

Wengine ni Sele Bwenzi, Joseph Ambokege, Ahmed Chambela, Sadala Lipangile, Sandale Komanje, Rogers Gabriel, Fredrick Kalubunga na Erick Kabamba aliyetokea Vipers FC.
Pamoja na kunasa saini hizo, lakini ilikwaa kisiki kwa baadhi ya mastaa waliokuwa katika hesabu zake wakiwa ni Thadeo Lwanga, Luis Miquisone na Saido Ntibazonkiza ambao walishindwana kimaslahi.
Licha ya usajili huo wa wachezaji, lakini pia inamshusha kocha mpya, Vladslav Heric kutoka Serbia anayetarajiwa kutambulishwa muda wowote kabla ya ligi kuanza.
Taarifa zilizopatikana kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa tayari kocha huyo yupo katika moja ya hoteli kubwa jijini Mbeya akisubiri muda wowote kuvaa uzi wa KenGold.
Kuja kwa kocha huyo inaelezwa ni kutaka kufanya mabadiliko kikosini ili kuendana na hali ya wachezaji wa mataifa tofauti, ambapo Mserbia huyo atasaidiana na Kapilima na Challe kwenye benchi.

KAPILIMA ACHEKELEA
Kocha wa sasa wa timu hiyo, Omary Kapilima anasema usajili walioufanya wanaenda kusahihisha makosa yaliyotokea mapema ili kurudisha morali na heshima.
Amekiri duru la pili litakuwa gumu kutokana na ushindani ulivyo kwa kila timu, lakini kutokana na maandalizi waliyonayo watafanya vizuri kwenye ligi.
“Ndio maana tumeamua kuingia kambini mapema kujiandaa na mzunguko wa pili, wachezaji wanaonyesha ari na morali. Kila mmoja yupo tayari kwa ajili ya ligi,” anasema beki huyo wa zamani wa Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar.
“Tunajua kazi haitakuwa nyepesi kwakuwa hatupo sehemu salama hivyo tunahitaji kuona mechi 10 za mwanzo tunapambana kutafuta ushindi ili kujitoa mkiani,” anaongeza Kapilima.
Nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars, anasemaa usajili wote umekidhi mahitaji ya timu na kwamba wapo tayari kuanza upya akieleza kuwa mashabiki wawe na matarajio makubwa na timu hiyo.
Kuhusu kushuka daraja, kocha huyo anasema ni mapema sana kutabiri matokeo hayo, akieleza kuwa bado wana mechi 14 za kuamua hatma yao akieleza kuwa lazima kieleweke.
Anaongeza kuwa baada ya kutokea mabadiliko ya ratiba kwa sasa wanaendelea kujifua zaidi kujiandaa na ligi hiyo na kutamba kuwa KenGold mpya inakuja.
“Tunaendelea na mazoezi na tuko tayari kwa ligi, bado ni mapema sana kututabiria kwakuwa mechi 14 tulizonazo zinaweza kuwa na mabadiliko makubwa,” anasema Kampilima.
WACHEZAJI NAO
Kipa wa timu hiyo, Castor Mhagama anasema baada ya kutokuwa na mwenendo mbaya mzunguko wa kwanza, raundi ya pili inaenda kuwa ya tofauti kutokana na maandalizi waliyonayo.
Anasema pamoja na kipindi kigumu walichopitia, lakini hawajakata tamaa wala kupoteza morali, akieleza kuwa matarajio yao ni kuona wanaondoka kutoka katika nafasi za chini.
“Bado tuna ari na morali, tunatarajia raundi ya pili itaanza kwa mafanikio makubwa na kuziba zile nafasi tulizopoteza mzunguko wa pili kwakuwa tumeanza maandalizi makubwa,” anasema kipa huyo.
Straika wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kikosini humo, Joshua Ibrahim anasema pamoja na kiwango binafsi alichonacho, lakini kiu yake ni kuona timu inafanya vizuri pia.
Anasema matokeo waliyopata raundi ya kwanza hayakuwa mazuri kwao, akieleza kuwa mkakati wao ni kuona wanabadili upepo na kuinusuru timu kubaki salama Ligi Kuu.
“Tumepitia magumu lakini tunaenda kuanza upya, kimsingi kila mmoja atimize wajibu kuhakikisha tunasalia Ligi Kuu na lolote linawezekana kwakuwa uwezo na nia tunayo,” anasema Ibrahim.

USIKIE UONGOZI
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha anasema kwa sasa kazi inaenda kuanza upya kufuatia usajili na maandalizi ya ndani na nje ya uwanja waliyofanya akieleza kuwa burudani ipo KenGold.
Anasema walikubali matokeo yaliyotokea katika mzunguko wa kwanza na sasa wanarudi kivingine kuhakikisha timu inafanya vizuri kutokana na uwekezaji walioufanya.
“Tulikubali matokeo yaliyotokea mzunguko wa kwanza ndio maana tumeamua kuingia sokoni kuboresha kikosi ili kubadili mwelekeo, tunaamini kwa kilichofanyika tutavuna matunda,”
“Mashabiki waje sasa kupata burudani, tumeamua kuingia sokoni kujenga timu mpya ili tuanze ligi upyaa, tunaamini tutabaki salama Ligi Kuu kwakuwa maandalizi tumefanya,” anasema Mkocha.