Prime
Chamou amenikumbusha Bacca, usitanie nafasi

Muktasari:
- Mchezaji anajua kwa hiki alichoumia basi anaweza kukaa nje hata miezi sita. Wachezaji wanaijua miili yao. Mara nyingi wanakuwa wamekaa katika mpira kwa muda mrefu kujua moja kwa moja aina ya majeraha ama kwa kupitia uzoefu wa mwili wake mwenyewe au kupitia kwa wachezaji wenzake mbalimbali aliowahi kucheza nao au kusikia majeraha yao.
WAKATI mwingine tunaona wachezaji walioumia wakiondoka uwanjani huku wakilia. Machozi yao hayatokani na maumivu tu. Machozi yao yanatokana na ukweli kwamba wanakuwa wamegundua watakaa nje kwa muda mrefu kwa aina ya majeraha ambayo wameyapata. Wakati mwingine wachezaji wanakuwa kama madaktari.
Mchezaji anajua kwa hiki alichoumia basi anaweza kukaa nje hata miezi sita. Wachezaji wanaijua miili yao. Mara nyingi wanakuwa wamekaa katika mpira kwa muda mrefu kujua moja kwa moja aina ya majeraha ama kwa kupitia uzoefu wa mwili wake mwenyewe au kupitia kwa wachezaji wenzake mbalimbali aliowahi kucheza nao au kusikia majeraha yao.
Hii inawafanya wachezaji kulia wakiwa katika machela wakitolewa nje ya uwanja. Kuna mambo mawili ambayo yanawatoa machozi. Jambo la kwanza ni kuikosa kazi ambayo wanafuraia kuifanya. Wachezaji wana bahati ya kufanya kazi wanayoipenda na hapo hapo wanalipwa mamilioni ya pesa. Kukaa benchi ni kitu kinachowaumiza.
Kingine ambacho kinawaumiza ni ushindani wa nafasi yenyewe. Anaingia mtu mwingine anaifanya kazi yako kwa ufasaha zaidi na kisha anaitwaa namba yenyewe. Kuanzia Ulaya hadi Tanzania mifano ya namna hii ni mingi. Hiki ndicho kilichomtokea Che Malone Fondoh. Huu ni mfano halisi.

Aliumia kwa muda mrefu na nafasi yake akaichukua Karaboue Chamou. Mwanzoni Chamou hakuaminika kwa Wanasimba lakini sasa gari limewaka.
Wachezaji huwa wanalia kama ambavyo Che Malone alipaswa kulia wakati anapata majeraha. Na sasa Chamou anacheza vema na patna wake Che Malone Mtanzania mwenzetu, Abdulrazak Hamza. Uzuri ni kwamba wote ni warefu. Uzuri zaidi ni kwamba Chamou hajafanya makosa tangu alipokabidhiwa nafasi ya Che Malone.
Rekodi zake na timu pia hazimuangushi. Historia itaendelea tu kutukumbusha kwamba wakati Mnyama Simba akitinga fainali za michuano ya Shirikisho barani Afrika ukuta wake ulikuwa unaundwa na Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein Tshabalala, Abdulrazak Hamza na Karaboue Chamou. Huu ndio ukweli halisi.

Kilichotokea kwa Chamou kinanikumbusha Ibrahim Bacca alivyofanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza cha Yanga. Ilishaeleweka kwamba walinzi wawili wa kati wa kwanza wa Yanga walikuwa Bakari Mwamnyeto na Dickson Job. Mioyo ya mashabiki wa Yanga ilikuwa imetulia hapo. Hata haikueleweka kwa nini Rais wao, Hersi Said alikwenda Zanzibar kumchukua Bacca.
Siku moja Mwamnyeto aliumia na Bacca akaonyesha ambacho amejaaliwa nacho. Bahati nzuri kwa Mwamnyeto ni kwamba kocha wa wakati huo wa Yanga aliamua kuwachezesha walinzi wote watatu kwa pamoja katika mfumo wake. Lakini licha ya hivyo makocha waliokuja baadaye wanapoamua kuchezesha mabeki wawili wa kati lazima Bacca na Job waanze.
Wakati mwingine kilichohitajika kwa mchezaji kama Chamou ni kucheza mfululizo. Mechi zake za mwanzo hakuonekana kuwa na makali. Huwa inatokea. Haujui mchezaji alikotoka. Labda hakufanya mazoezi kwa muda mrefu. Labda alikuwa ameumia. Labda alikuwa hajazoea aina ya mpira wetu. Huwa inatokea. Anapopata nafasi ya kufanya mazoezi kwa muda na kisha kuanza kucheza mfululizo basi gari linawaka.

Na sasa Che Malone amerudi uwanjani. Kocha atamuweka nje Chamou au atabadili mfumo wake wa uchezaji na kuweza kuwapanga wote kama ilivyotokea kwa Bacca, Job na Mwamunyeto? Hilo ni swali moja. Lakini Che Malone ana mtihani mwingine ambao unamkabili. Tayari mashabiki wa Simba walikuwa wananong'ona kuhusu makosa aliyokuwa anayafanya katika mechi za kimataifa.

Rafiki yangu mmoja wa ndani ya Simba alininong'oneza kwamba hata kuelekea katika pambano la Machi 8 dhidi ya mtani ambalo halikuchezwa kulikuwa na uwezekano wa Che Malone kutopangwa kwa sababu baadhi ya viongozi walikosa imani naye kufuatia makosa ya mara kwa mara aliyokuwa anayafanya.
Kwa kocha Fadlu Davids nadhani anaweza kufuata mfumo wa makocha wengi wakubwa duniani ambao huwa wanajisemea 'hauwezi kuibadili timu inayoshinda'. Akifanya hivyo basi nafasi ya Che Malone itaanza kuwa finyu, hasa tukikubaliana na ukweli kwamba licha ya kwamba Che Malone ni beki mzuri lakini sidhani amefikia umuhimu wa kuwa nguzo kubwa kama ilivyokuwa kwa kina Pascal Wawa na Joash Onyango enzi zao.

Kitu kingine ambacho kinawaumiza wachezaji wetu ambao hawapati nafasi ni ukweli kwamba kuna michuano michache katika mpira wetu. Kule kwa wenzetu chukulia timu kubwa kama za England huwa zinacheza mechi nyingi za Ligi. Mechi 38. Halafu hapo hapo kuna michuano ya FA, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Carabao. Sisi tuna mechi chache za Ligi halafu Ligi ya Mabingwa na FA ambayo nayo ina mechi chache.
Wakati mwingine kocha hahitaji kikosi kipana kama wachezaji wake wanakuwa fiti. Labda bahati kwa Che Malone ni kwamba mpira wetu una viporo vingi ambavyo baadaye vinaliwa mfululizo kama tunavyoona namna ambavyo Simba imekabiliwa na mechi nyingi mfululizo kwa sasa kwa ajili ya kumaliza Ligi salama.
Uzoefu pia unaonyesha kwa mpira wetu wakati mwingine inakuwa nadra kuwa na walinzi watatu wa kati huku mzawa akiwa lazima acheze na walinzi wawili wa kigeni wakiwania namba. Tumezoea kuona wageni wakibadilishana nafasi zaidi katika maeneo mengine kama ya kiungo na ushambuliaji lakini linapokuja suala la mlinzi wa kati mmoja anaweza kutolewa kafara kwa ajili ya kupisha mchezaji mwingine wa kigeni ambaye atakuwa anacheza eneo la kiungo au ushambuliaji.

Tuone kuanzia sasa mpaka mwisho wa msimu nini kinaweza kutokea lakini kwa kadri ninavyofahamu hata Karaboue mwenyewe angekuwa anaendelea kukaa benchini basi si ajabu mwishoni mwa msimu angeweza kujikuta yuko uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akielekea kwao kusaka timu mpya.
Kule kwa watani iliwahi kumtokea jirani yetu wa Uganda, Gift Fred. Alikuwa mlinzi mzuri lakini kwa kukaa sana benchini ilikuwa wazi kwamba Yanga wangeizawadia nafasi hiyo ya mchezaji wa kigeni kwenda kwa mchezaji wa nafasi nyingine. Ndio maana alipoondoka Gift hakuja tena mlinzi wa kati wa kigeni katika nafasi yake. Hivi ndivyo wakubwa wanavyofanya kazi.
Hata pale eneo la katikati la Simba nahisi mwishoni mwa msimu wanaweza kuamua kumtema Augustine Okajepha kwa sababu Yusuf Kagoma amekuja kuwashangaza wengi. Hauwezi kuwa na mgeni anayekaa benchini halafu ndani kuna mgeni na mzawa, Kagoma na Fabrice Ngoma ambao wanafanya vizuri. Sana sana anaweza kuletwa mchezaji mwingine wa kigeni kwa ajili ya kutoa changamoto kwa Kagoma na Ngoma kitu ambacho ni dhahiri kinaonekana kumshinda Okajepha.