Ndikumana Sijaja Coastal kuuza uso mjue!

COASTAL Union ya Tanga imesajili kipa mzoefu, Justin Ndikumana (30) aliyecheza nchi mbalimbali, jambo litakaloisaidia timu hiyo kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ulinzi ili kumaliza mzunguko wa pili kishujaa.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Ndikumana anafunguka namna alivyokuwa anaifuatilia Ligi Kuu Bara na kupata mwanga kujua linachezwa soka la aina gani, jambo lililompa urahisi wa kutopata changamoto ya kuzoea mikimiki, akieleza ligi hiyo ni tafu.

Ukiachana na hilo, anatamani washambuliaji watambue uwepo wake na awe na muendelezo wa kuchukua tuzo kama alivyokuwa anazinyakua alikotoka ambapo 2018/19 akiwa  Sofapaka ya Kenya  alikuwa kipa namba mbili bora nyuma ya Faruk Shikhalo.

"Nilichukua tuzo mbalimbali kama kipa bora wa mwezi machi 2019 nikiwa na Sofapaka, kitu ninachotamani kiwe na muendelezo, licha ya kutambua kwamba kuna ushindani mkubwa kwenye ligi ya Tanzania," anasema.

Ligi kuu bara
Anasema alikuwa anaifuatilia Ligi Kuu Bara kupitia vyombo mbalimbali vya hapa nchini, hilo limemsaidia  kufanya kazi kwa urahisi baada ya kujiunga na Coastal Union ya Tanga.

Wachezaji kutoka Burundi  ambao ni chanzo  cha kuifuatilia Ligi Kuu waliondoka na wanaocheza sasa anaowataja  ni Amissi Tambwe (Singida Big Stars), Laudit Mavugo, Gilbert Kaze, Emery Nimubona waliichezea Simba na Said  Ntibazonkiza 'Saido' (Simba).

"Ligi ya Tanzania ina ushindani mkali na ina mwamko mkubwa wa mashabiki ambapo mchezaji akifanya vizuri anakuwa na jina kubwa, kitu kinachowapa morali wachezaji kujituma bila kuchoka, tofauti na nchi nyingine ambapo hakuna sapoti kama inayopatikana Tanzania.

"Pia Coastal Union nilikuwa naifuatilia kwa ukaribu kwani imemsajili Mburundi mwenzangu Francis Mustapha, hivyo baada ya kujiunga nao sikuwa na ugeni sana, kwani nimekutana na watu tofauti utadhani nimezaliwa mkoa huo."

Kilichomshangaza zaidi baada ya kutua Coastal Union ni mapokezi makubwa ya mashabiki, jambo ambalo hakuzoea kuliona kwenye vyombo vya habari vinavyoonyesha Simba na Yanga ndizo timu pekee zenye wafuasi wengi "Nimeshangaa sana kuona timu yangu mpya ina mashabiki wa kutosha na ina presha kubwa."

Mastaa walitokea Burundi, Kenya
Anaeleza kwa miaka ya hivi karibuni wapo mastaa wa Ligi kuu Bara ambao majina yao yanatajwa zaidi Kenya na Burundi kutokana na bidii yao ya kazi na kuwafanya wachezaji wengine kutamani kuja kucheza Tanzania.

Mastaa  hao ni Fiston Mayele (Yanga), Meddie Kagere (Singid Big Stars), Said  Ntibazonkiza 'Saido' (Simba), Jonas Mkude (Simba), Feisal Salum 'Fei Toto' (Yanga), Joash Onyango (Simba), Clatous Chama (Simba) na John Bocco (Simba), kwamba hata timu alizopitia zilikuwa zinawafuatilia zaidi na kutaka kujua vyombo vya habari vinasema nini juu yao.

Nje na mastaa hao alikuwa anamkubali  ni Juma Kaseja kabla ya  kustafu uwanjani na  sasa amegeukia ukocha wa makipa wa Kagera Sugar, anasema akiwa golini alisimama kama mwalimu wa wenzake kufanya kazi kwa umakini.

"Kwa mara ya kwanza kukutana na Kaseja na nilimwambia namna ninavyopenda utendaji wake, nikiwa na timu ya taifa ya Burundi tulicheza dhidi Stars Uwanja wa Benjamin Mkapa walitushinda kwa penalti, kiukweli nilijisikia faraja kucheza naye."

"Kitu kinachomtangaza mchezaji ni muendelezo wa kiwango chake,Kaseja nilimsikia kwa muda mrefu akiitwa Tanzania One na aliitendea haki, alikuwa mahili wa kudaka penalti, ilikuwa ngumu kumfunga mtu na mtu akiwa karibu, makipa chipukizi warudi kwenye video zake wajifunze jambo kutoka kwake."
Anasisitiza wachezaji wengi wanaocheza Tanzania wanaonekana vipaji vyao kwa ukubwa kutokana na sapoti ya vyombo vya habari namna vinavyojua kuutangaza mchezo wa soka "Gazeti lenu la Mwanaspoti ni mojawapo ya yale  yanayofuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, kwa namna linavyoripoti habari zake nyingi ni za uhakika."

Angechemka soka
 Anasema kama malengo yake kwenye soka yasingefanikiwa angekuwa anafanya shughuli mbalimbali nchini kwao Burundi kama vile biashara mbalimbali kwani hakuwahi kufikilia kufanya kazi nyingine na uwanjani.

"Soka limenikutanisha na watu tofauti, limenipa elimu ya kujua kuishi na watu, nimetembea nchi mbalimba ikiwemo Tanzania,  hivyo isingekuwa kazi hiyo ningefanya biashara, kama ilivyo kwa wanaume wengine waliopo Burundi ambao wanajishugulisha na vitu tofauti ili mladi kuendesha maisha yao.

"Najivunia kazi ya soka kwani limefanya niwajengee wazazi wangu wanaishi sehemu salama, namiliki vitu vingi sana ambavyo siwezi kuviweka wazi na ingekuwa vigumu sana kufanya mambo makubwa nje na soka, hivyo kazi ninayoiheshimu sana."

Familia ya soka
Amezaliwa katika  familia yao  ya soka kuanzia baba yake mzazi ambaye hakucheza levo za juu kama wao "Kaka zangu wana vipaji vikubwa wanacheza nafasi za ulinzi, hivyo haikuwa kazi kwangu kufanya kazi hii nikajikuta napenda na ndio maana nimefika hapa nilipo.

"Ndugu zangu wapo waliotangulia mbele ya haki, wadogo zangu wawili wanaocheza Ligi Kuu ya Burundi ni Ndikuriyo Patient yupo timu ya  Bumamuru FC , Ndikumana Mohamed Alain anachezea  Les Messagers FC, huwa tukikutana wakati wa mapumziko tunaelimishana namna ya kuwa bora zaidi,"anasema.

Anakijua kiswahili
Anasema amezaliwa uswahilini  Bujumbura mtaa wa Buyenzi ambako wanazungumza Kiswahili kama Tanzania, jambo ambalo linampa urahisi wa mawasiliano na kila mtu baada ya kujiunga na Coastal Union, akisisitiza akiamua kutembea mitaa mbalimbali ya Tanga hakuna litakalomsumbua.

"Historia yangu nina miaka 30, nimecheza timu ya taifa ya Burundi, pia katika timu ya kituo cha  Inyange F.C, ya Daraja la Kwanza Prince Louis F.C, Vital'o F.C ambapo nilichukuwa taji la Ligi Kuu mwaka 2012, Kombe la Cecafa Kagame cup 2013 huko Sudani.

"Nikanunuliwa  na timu ya O.C Muungano ya  Bukavu ya Daraja la Kwanza, ikaninunua Saint Eloi Lupopo ya Lubumbashi huku nilikutana  na David Molinga, Heritier Makambo na Pascal Kitenge, ikaninunua  Sofapaka F.C ya  Kenya ambako nilikuwa mchezaji bora March 2019, kisha  kipa bora namba mbili nyuma ya Faruk Shikalo 2018/2019 baada ya hapo nikajiunga Bandari."

Kujiunga Coastal Union
Anasema 2020 akiwa Bandari FC ya Kenya ilikwenda kucheza mechi ya kirafiki na Coastal Union mkoani Tanga, ambapo viongozi wa wagosi wa kaya walipenda kipaji chake, tangu pale wakaanza kumfuatilia.

"Baada ya mechi ile ya kirafiki, viongozi wa Coastal Union walianza kufuatilia kazi zangu wakati mwingine wananipongeza kwa kucheza vizuri, tukawa na mawasiliano ya karibu hadi ulipofika muda wa kujiunga nao ambao wanahitaji kuona huduma yangu inaifaa timu.

"Natarajia kufanya ushindani kuanzia kwenye timu yangu hadi wapinzania, nilikotoka nilikuwa nachukua tuzo mbalimbali, hivyo natamani niwe na muendelezo kwa kuchukua kwenye ligi ya Tanzania, ingawa najua kuna makipa wazuri wanaoshindana kwa klinishiti."

Anasema anatambua Ligi Kuu ina washambuliaji wazuri na makini ambao wanamfanya muda mwingi atafute mbinu za kukabiliana nao ili awe kipa anayewanyima mabao.

"Japokuwa wanaongoza wanatoka Yanga ambako ni Mayele mwenye mabao 15, Simba ni Moses Phiri mabao 10 pia ina viungo wazuri wanaofunga na kutengeneza pasi  za mwisho Chama na Saido, nimewajua kirahisi kutokana na umarufu wao ila wapo wengi wazuri bado sijawajua kwa majina," anasema.
Mbali na hilo, anasema akikaa golini anapenda kuwasiliana kwa maneno na vitendo na mabeki wake ili kunyumbulika kufanya majukumu na kuzipa mianya inayotokea kwa bahati mbaya.

"Ni kweli kila mchezaji anapaswa kukaa kwenye majukumu yake, lakini haizuii mwingine anapoponyokwa basi awepo anaweza kunyumbulika kwa mawasiliano ili mladi tu kufanya timu kuwa salama," anasema.