Nani atawarithi hawa Simba?

NI misimu sita sasa Simba imekuwa katika pata shika nguo kuchanika ya wingu la makocha ambao wanaingia na kushindwa kudumu.

Ndani ya miaka hiyo makocha wanane wamekalia benchi kuu la timu hiyo licha ya wengine kufanya vizuri lakini waliondolewa na kuletwa wapya ambao nao maji yalifuata mkondo.

Wengi wanasema na kujiuliza iweje makocha hao wote wenye CV nzuri wanashindwa kudumu Simba wakitupia lawama kwa viongozi kutokana na timu ambazo machoka hao huenda wanapoondoka Simba.

Mwanaspoti linakukumbusha makocha wakali waliopita Simba hivi karibuni na kuacha alama na wengine hawakuambulia chochote.


PIERRE RECHANTRE (JAN 2018-JUNi 2018)

Aliipa Simba ubingwa msimu 2017/2018 ikiwa ni miaka mitano tangu ilipoutwaa na ufalme huo iliuacha kwa watani zao Yanga ambao walitwaa mara nne na Azam FC mara moja.

Msimu huo Aprili 29 aliweka historia ya kumfunga mtani wake Yanga bao 1-0 ushindi ulionogesha zaidi ubingwa wao.

Mbali na hilo kocha huyo kuipa Simba taji la Ngao ya Jamii ambalo pia lilikuwa likishikiliwa na mtani wake hakudumu kikosini.


PATRICK AUSSEUMS (JULai 2018-NOVEMba 2019)

Walimuita uchebe, raia wa Ubelgij kocha aliyependwa zaidi na wachezaji wa klabu hiyo kutokana na namna ambavyo alikuwa akiishi nao.

Ubora wa kocha huyo uliifanya Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiondosha Nkana Red Devils ya Zambia. Furaha ambayo itaendelea kuwepo mioyoni mwa Wanasimba sambamba na wachezaji Clatous Chama na Hassan Dilunga aliyetengeneza pasi safi ya bao liliipeleka mbele Simba.

Mbali na hilo aliipeleka hatua hiyo tena 2019 baada ya kuifunga As Vita ya Congo mabao 2-1.

Mbali na hilo Ausseums aliipa timu hiyo taji la Ligi Kuu mara ya pili mfululizo sambamba na Ngao ya Jamii matokeo yaliyowaacha hoi watani zao Yanga.  Alipotoka Simba aliitumikia Black Leopards na kwenda tena AFC Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.


SVEN VANDEBROECK (DESEMBA 2019-JAN 2021)

Mbelgij huyu aliyepewa jina la utani ‘Kishingo’ alisifika zaidi kwa ukali wake kwa wachezaji ambao uliifanya timu kuwa na nidhamu ya hali ya juu ndani na hata nje ya dimba.

Aliacha alama baada ya kunyakua mataji yote matatu yaliyoshindaniwa msimu huo la Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azam sambamba na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baada ya Simba kumuona wa kazi gani FAR Rabat ya Morocco ikamnasa, Abha, Wydad na sasa CR Belouizdad.


DIDIER GOMES (JAN 2021-OKTOBA 2021)

Kocha aliyeonekana kupendwa na wachezaji hadi mashabiki, lakini muda wake ulikuwa mfupi Msimbazi.

Gomes raia wa Ufaransa alidumu Simba kwa miezi 10 tu na kuwafanya mabosi kumfungashia virago baada ya kushindwa kuivusha Simba hatua ya makundi baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Jwaneng Galaxy wakiwa na mtaji wa mabao 2-0  walioupata ugenini yeye akiwa jukwaani kutokana na leseni yake kutompa haki ya kukaa benchi na kusaidiwa majukumu na Thiery Hitimana.

Lakini aliipa Simba ubingwa wa michuano mipya ya Super Cup ambayo ilifanyika hapa nchini.

Alipotoka Simba alikuwa kocha mkuu timu ya Taifa ya Maurtania, klabu ya Al Wehdat, Al Ain FC, Al Taraji na sasa ni kocha  wa Timu ya Taifa ya Botswana.


PABLo FRANCO (NOVEMBA 2021-MEI 2022)

Raia wa Hispania hakumaliza mwaka katika kikosi hicho (miezi saba tu) licha ya matumaini makubwa ambayo Simba ilikuwa nayo juu yake lakini uvumilivu haukuwa upande wao na kumpa mkono wa kwaheri.

Kwa sasa Pablo anakinoa kikosi cha Amazulu FC kinachoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini inayoshika nafasi ya 11 katika timu 16 zinazoshiriki.


ZORAN MAC (JUNE 2022-SEPTEMBA 2022)

Kocha aliyedumu kwa muda mfupi sana ndani ya kikosi hicho miezi miwili tu ilimfanya kufungasha virago vyake.

Ilisemekana kocha huyo alipojiunga na Simba alikuwa na ofa nyingine katika timu za nje na mara tu baada ya kukubaliana akaielewa ofa yao akaona isiwe tabu wakakaa mezani na kukubaliana.

Katika timu hizo ilipofika ofa nzuri Al Ittihad akaenda kujiunga nayo lakini hakudumu mwaka jana alijiuzulu na sasa hana timu.


ROBERTO OLIVEIRA (JAN 2023-NOVEMBA 2023)

Katika michezo 18 aliyosimami Simba ameshinda 15 sare miwili na kupoteza mmoja dhidi ya Yanga.

Huenda angefungwa hata bao 1-0 mabosi wangeendelea kumvumilia kukinoa kikosi hicho ila  idadi kubwa ya mabao 5-1 ndiyo iliyowachanganya mabosi na kuona isiwe tabu ni bora awapishe.