MZUKA WA GOLF: Leverian, huyu ndiye mpishi wa watu maarufu kwenye gofu

HAKUNA jambo linaloshindikana mbele ya uthubutu, nidhamu, kujituma na kujiamini. Hivyo ndivyo anaeleza mchezaji wa kulipwa wa gofu, Geofrey Leverian mwenye mafanikio makubwa yaliyotokana na kutodharau mwanzo wa hatua zake katika mchezo huo.

Leverian anasema alianza kama caddy, lakini imani yake ilimtuma kuja kuwa mchezaji mkubwa wa kuigwa ndani na nje ya nchi, hivyo hakuangalia mazingira ya wakati huo na hakuyaruhusu kumkatisha tamaa.

“Jambo kubwa lililonipa mafanikio nilipenda kujifunza kwa bidii na kuthubutu kufanya. Ndio maana wale waliokuwa wananizunguka walinipa moyo wa kuzifikia ndoto zangu,” anasema.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Leverian anawashauri vijana namna wanavyopaswa kuzitazama fursa kisha wajue kuzipambania, huku wakijua kwamba hakuna kitu kinachokuja kirahisi, badala yake yanahitajika mapambano.

“Fursa haziwezi kuwafuata nyumbani mfano wakisoma kuna mambo ya caddy kwanini wasiende huko ambako watakutana na watu wengi kutoka sekta mbalimbali, maana hata mimi nilikuwa caddy na sasa ni mchezaji wa kulipwa,” anasema.


MAFANIKIO ALIYOPATA

Leverian anasema maisha yake yanaendeshwa na mchezo huo ambapo amefanikiwa kujenga nyumba nne, huku tatu zikiwa Dar es Salaam na moja mkoani Morogoro.

“Ukiachana na nyumba nina bodaboda tano, duka la vinywaji vya jumla, lakini pia nina gari aina ya Jeep ambalo nilipewa na Mjerumani mmoja. Nilikuwa namfundisha akaniambia nikijua hadi kufikia hatua ya kucheza mashindano nitakupa zawadi ya gari, baada ya kuanza kucheza mashindano akanipatia gari hilo, ikabidi niifundishe familia yake nzima,” anasema.

“Nimepata zawadi nyingi nyingine siwezi kutaja kila kitu hapa. Pia mchezo huo unanifanya nisomeshe watoto wangu shule nzuri, hivyo una maana kubwa kwenye maisha yangu.”

Kutokana na kazi yake ya ukocha inamfanya kualikwa kwenye mataifa mbalimbali kama Afrika Kusini, Marekani, Kenya na wachezaji ambao amewahi kuwafundisha kutoka nchi hizo, lakini kutokana na ratiba zake anasema imekuwa ngumu kusafiri mara kwa mara.

“Nawafundisha watu mbalimbali wa ndani na nje kwa siku wanaweza kuwa watano hadi sita, kila mtu kwa muda wake anaona ana nafasi ya kucheza na ada yao kwa saa moja ni Sh20, 000 na kitaalamu anayeanza anapaswa kucheza saa mbili, ila siyo lazima hiyo ni sababu inayofanya nikose muda wa kusafiri,” anasema.

“Mbali na kufundisha bado ni mchezaji wa kulipwa. Kuna wakati mwingine nakuwa najiandaa na mashindano, hivyo muda wangu nakuwa naupangilia vizuri ili kufanya kila kitu kwa wakati na kiweze kwenda vizuri.”


MATAJI ANAYOMILIKI

Leverian ambaye alianzia kufanya kazi ya caddy kwa kumbebea kaka yake aliyemtaja kwa jina la Godfrey Leverian, bingwa wa mashindano ya Morogoro Open yaliyofanyika Oktoba, anasema ndiye sababu ya kumfanya ajiunge na mchezo huo.

“Asilimia 98 ya mapro walianzia kwenye caddy ndio maana wanaujua sana huo mchezo, kwani muda mwingi walikuwa wanashinda uwanjani. Ilikuwa rahisi kwao kuzijua sheria na mbinu za mchezo, ndivyo ilivyotokea kwangu,” anasema nyota huyo wa gofu.

“Wakati nambebea begi kaka yangu, kuna wakati alikuwa ananifundisha jinsi ya kucheza na mwaka 2001 nikaanza rasmi kucheza. 2004 nikashiriki  mashindano ya Arusha Open niliibuka mshindi namba moja wa glosi kwa maana ya mtu niliyehesabiwa mipigo ya mpira bila kupunguza wala kuongeza.”


MALINZI KAMBEBA

Leverian Anasema baada ya kuanza kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Dioniz Malinzi alisaidia kumuendeleza zaidi.

“Mwaka 2006, Malinzi alituchukua vijana wanne na kutupeleka kwenda kusomea mchezo huo kwenye chuo cha gofu, kilichopo Afrika Kusini kwa miezi mitano. Kiukweli binafsi nilirejea na maarifa makubwa ambayo yananisaidia hadi sasa.

“Malinzi alikuwa mhimili mkubwa katika gofu. Aliwasaidia vijana wengi na kuzifanikisha ndoto zao. Kwenye kipindi chake aliupigania mchezo wa gofu kuona wanapatikana Watanzania wenye ushindani dhidi ya nchi nyingine na ndiye aliyemleta kocha mzungu wa timu ya taifa alikuwa anaitwa Charles Fallah kwa sasa ni marehemu,” anasema kocha na mchezaji huyo.


GOFU YAMKUTANISHA NA VIGOGO

Kocha huyo anasema isingekuwa gofu asingeweza kupata nafasi ya kukutana na wakuu wa nchi, mawaziri, wabunge, wamiliki wa kampuni na watu kutoka sekta mbalimbali.

“Kwenye kazi yangu ya kufundisha nimekutana na watu hao wazito, mabalozi, wakati mwingine napata nafasi ya kuisemea jamii. Yapo mambo yanayotekelezwa kwa kuwa nilisema, ingawa hivyo vitu siwezi kuviweka wazi,” anasema.

Pia anafundisha timu ya gofu ya Tanzania ya wabunge ambao kila mwaka wanakuwa na mashindano yao, yakizikutanisha nchi kama Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda.

Wabunge anaowafundisha anawataja kuwa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye; Mbungewa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangalla; Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro; wabunge wa viti maalumu, Grace Tendega na Neema Mgaya.

“Tunatoka familia za chini lakini huu mchezo umefanya kila jambo liwe jepesi, kwani kuna muda ambao mtapiga stori. Ukiona kuna nafasi ya kuisemea jamii unasema sehemu fulani kuna changamoto na baadhi zimetatuliwa,” anasema.


AMPA TANO BAKARI MACHUMU

Leverian anasema kitendo cha mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Bakari Machumu kuwa mstari wa mbele kuhakikisha gofu unakuwa mchezo unaowafikia watu kupitia gazeti la Mwanaspoti ikienda na kaulimbiu ya ‘Mzuka wa Gofu’ kinatoa moyo wa kuendelea kuwafundisha vijana ambao watalibeba taifa kwenye mashindano mbalimbali.

Mbali na hilo, anasema Machumu ni mwanafunzi wake aliyemfundisha na ameelewa kucheza mchezo huo katika kipindi kifupi, na alipofikia anaweza kushiriki mashindano ya gofu ya ndani na nje ya nchi.

“Kwa kawaida mwanafunzi anapaswa kufundishwa siku 10 kabla ya kuanza kucheza uwanjani yeye katumia siku sita na siku ya saba tukaingia uwanjani,” anasema Leverian.

“Kwa sasa Machumu ni mchezaji anayeweza kucheza mashindano ya ndani na nje ya nchi. Ana handcup 24 na anazidi kuzipunguza. Naamini akiendelea kuna siku anaweza akafikisha 10 hata 0.

“Kwangu niliona fahari kumfundisha mtu wa aina yake, kwani nilipata fursa ya kumwambia magazeti anayoyasimamia yaendelee kumulika mchezo wa gofu ambao unatoa ajira kwa watu wote, maana ni mchezo ambao haubagui umri na kweli amekuwa akifanya jambo hilo kwa umahiri mkubwa.”


KAULI YA MACHUMU

Kwa upande wake, Machumu anasema bado ni mapema kuona anaujua sana mchezo huo, badala yake anahitaji kujua zaidi mbinu, kanuni na utulivu akikiri kwamba kwa muda aliocheza ameona ni mchezo wa kipekee unaoondoa msongo wa mawazo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia) akiwa na mkurugezi mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu katika viwanja vya gofu Lugalo.

“Wakati mwingine inakuwa ni mawazo ya kazi. Sasa unapoenda viwanja vya gofu nadhani kwa ajili ya miti, nyasi inasaidia kuifanya akili iwe vizuri zaidi unakutana na watu tofauti wa kuzungumza nao vitu mbalimbali.” anasema.

 Anasema lengo la kuisapoti gofu na kuanzisha Mzuka wa Gofu kupitia gazeti hili ni ili kuondoa hofu kwa jamii kutokana na maneno inayosikia kuhusu mchezo huo.

“Hata mimi kabla ya kuanza kuucheza nilikuwa na mtazamo tofauti, ila kwa sasa niwaambie vijana mchezo huo ni ajira. Pia kwenye Klabu ya Lugalo nimeona watoto wanafanya vizuri sana, hilo linaonyesha miaka inayokuja gofu itakuwa juu sana,” alisema.

“Pia nishukuru vyama vya michezo hiyo kwa maana ya TGUna TGLU kwa kushirikiana na Mwananchi kupitia gazeti la Mwanaspoti. Naamini huko mbele tutafanya makubwa zaidi na tayari tumeanza kuona matokeo ya mapokeo ya jamii.”


Imeandaliwa na Olipa Assa, Nevumba Abubakar, Brown Msyani, Imani Makongoro na Oliver Albert