MZEE WA UPUPU: Ile ndizi ya Mwesigwa inazidi kunukia

Wednesday April 07 2021
MWESIGWA pic

NI rasmi sasa harakati za kuwania mkataba wa haki za matangazo ya kuonesha Ligi Kuu ya Tanzania zimefunguliwa rasmi kwa tangazo la TFF lililotoka Ijumaa ya Aprili 2, 2021.

TFF imetangaza zabuni hiyo kuvialika vituo vyenye uwezo wa kifedha na teknolojia kuwania haki ya matangazo ya luninga na redio kuanzia msimu ujao.

Itakumbukwa kwamba kwa sasa haki za matangazo ya luninga zinamilikiwa na Azam TV waliosaini mkataba wa miaka 5 tangu msimu wa 2016/17.

Hata hivyo, mkataba wa kwanza wa Azam TV na TFF TFF ajili ya haki za kuonesha ligi kuu ulisainiwa mwaka 2013 ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka, kwa miaka mitatu.

Hii ilikuwa na maana kwamba kila klabu ingepata shilingi milioni 100, jambo ambalo lilikuwa habari njema kwa vilabu vyote vya ligi kuu kasoro Yanga tu.

Mwenyekiti wa Yanga wa wakati huo, Yusuph Manji, aliupinga sana mkataba huo akisema pamoja na mambo mengine, una thamani dogo kwa kulinganisha na thamani halisi ya ligi.

Advertisement

Wakati huo ligi ilikuwa na timu 14, na timu 13 zilizobaki zikaitisha kikao kujadili suala hilo kuona endapo kulikuwa na mkataba mwingine wowote wenye thamani kubwa zaidi ya ule.

Bahati mbaya ni kwamba hakukuwa na mkataba mwingine hivyo wakakubaliana kuukubali uliokuwepo na hatimaye kutoa tamko la pamoja kwamba wameridhia mkataba huo na watachukua pesa yao ya mgao.

Katibu Mkuu wa TFF wa wakati huo, Selestine Mwesigwa, alitumia mkasa wa mtoto muuza ndizi.

Alisema kuna mtoto mmoja wa kijijini alitumwa na mama yake kuuza ndizi barabarani. Kwa bahati mbaya hakupata hata mteja mmoja tangu asubuhi hadi mchana wa jua kali.

Masikini mtoto wa watu njaa ikaanza kumuuma na hakuwa na hela ya kununua chakula wala maji ya kunywa...akachukua ndizi moja akaimenya na kuila.

Ghafla wakatokea wateja wengi na kununua ndizi zote zilizobaki hadi mwenyewe akashangaa.

Kumbe kitendo cha yule mtoto kuimenya ile ndizi mbovu moja kulifanya harufu yake kusambaa kila sehemu na kuwatamanisha hata wale ambao hawakuwa na mpango wa kula ndizi...ndiyo maana wakaja kununua.

Mwesigwa akasema kitendo cha wao kuuza haki za matangazo ya TV kwa Azam TV ilikuwa ni sawa na kuimenya ndizi moja na kuila, harufu yake itasambaa na kuvutia wengine wengi.

Na kweli, baada ya kumalizika kwa mkataba wa 2013 ambao ulikuwa wa miaka 3, mkataba mpya wa 2016 uliwaniwa na vituo vitatu vikubwa kiasi cha kuipandisha thamani ligi hadi kufikia shilingi bilioni 23 kwa miaka mitano, ambao ndiyo unaisha

msimu huu.

Wakati TFF imetangaza zabuni hii, mtu mmoja ampigie simu Mwesigwa na kumwambia ile ndizi imezidi kunukia.

Kutoka bilioni 4.5 kwa miaka mitatu mwaka 2013, kuja shilingi bilioni 23 kwa miaka mitano 2016, ndizi inazidi kunukia na sasa tutatajie zaidi ya bilioni 30 katika mkataba mpya.

Huu ni muda sahihi kwa TFF kutengeneza mazingira ya kuvuna pesa nyingi kadri inavyowezekana kupitia haki za matangazo.

Mojawapo ya mbinu ya kuvikamua vituo vya luninga ni kugawa zabuni katika vifurushi kama wanavyofanya England.

EPL ambayo ndiyo ligi tajiri zaidi duniani, wamezigawa mechi zao kwenye vifurushi vikuu 7.


Kifurushi A

Hiki kina mechi 32 na mechi zake huchezwa saa tisa na nusu alasiri Jumamosi tu.


Kifurushi B

Hiki nacho kina mechi 32, na zote ni Jumamosi. Lakini tofauti yake na kifurushi A ni muda wa mchezo...hiki mechi zake huchezwa saa mbili na nusu usiku.


Kifurushi C

Hiki nacho kina mechi 32, lakini zimegawanywa mara mbili.

Mechi 24 huchezwa saa 11 alasiri Jumapili, na mechi 8 huchezwa saa 4:45 usiku, Jumamosi.


Kifurushi D

Hiki kina mechi 32 zinazoanza saa 1:30 usiku, Jumamosi.


Kifurushi E

Hiki kina mechi 32 zilizogawanywa mara mbili. Mechi 24 za saa 5:00 usiku Jumatatu au Ijumaa saa 4:30/saa 5:00 usiku, na mechi 8 ni za saa 11:00 jioni Jumapili.


Kifurushi F

Hiki kina mechi 20 ambazo ni maalumu kwa ajili ya siku za sikukuu na mechi za katikati ya juma.


Kifurushi G

Hiki kina mechi 20 na zote ni kwa ajili ya mechi za katikati ya juma tu.

Vituo vinavyotaka kununua haki, vinatakiwa vinunue kwa vifurushi, siyo kwa pamoja na kituo kimoja hakiruhusiwi

kununua vifurushi vyote.

Zaidi ya vifurushi hivi, pia kuna haki ya kuonesha vipande vya mechi (highlights) ambayo huuzwa peke yake yake.

Tuachane na utamaduni wa vituo vya luninga kuonesha vipande vya mechi bila malipo yoyote.

Haki za matangazo ya redio pia huuzwa peke yake.

Hii ina maana kwamba ukijipanga sawasawa, haki za matangazo huweza kuipatia ligi husika pesa nyingi ambazo zitaifanya ligi hiyo kuwa na pesa nyingi.

Baada ya kujihakikishia pesa nyingi, kinachofuata sasa ni mgawanyo wa hizo pesa kwa vilabu.

England ambao nimewatolea mfano hapo, wana faida moja ambayo sisi hatuna, katika mgawanyo wa pesa.

Wao, ligi yao wameuiza mara mbili. Kwanza kwa ajili vituo vya ndani, halafu kwa vituo vya nje.

Mapato wanayoyaingiza kutokana na mauzo kwenye vituo vya ndani, hugawanywa sawa kwa vilabu vyote.

Mapato wanayoyaongiza kutokana na mauzo kwenye vituo vya nje, hugawanywa kutokana na mvuto wa vilabu kimataifa.

Sisi hatuna faida ya mauzo ya nje ya nchi yetu, hivyo tutengeneze mgawanyo kulingana na utaratibu wa mazingira yetu.

Ichukuliwe nusu ya pesa igawanywe sawa kwa vilabu vyote, halafu nusu iliyobaki igawanywe kulingana na msimamo wa mwisho kwenye ligi.

Hii itaongeza ushindani hadi mwisho wa msimu na kuondoa utamaduni wa timu kupunguza jitihada mwishoni mwa msimu baada ya kujihakikishia kutoshuka daraja.

Mwenye namba ya Mwesigwa, naomba anipe nimpigie nimkumbushe kuhusu mkasa wa ile ndizi.

Advertisement