Mwenda afunguka kilichotaka kumuondoa Simba

Muktasari:
- Mengi yalikuwa yakizungumzwa mitaani kwamba wawili hao walikuwa hawazungumzi wala kupeana mikono chanzo kikitajwa kuwa ni uhasama wa kuwania namba hiyo ambayo Kapombe amejihakikishia kikosini kwa miaka mingi tangu aliposajiliwa na Simba Julai 1, 2017 akitokea Azam FC.
STORI kubwa iliyozunguka maisha ya beki wa kulia, Israel Mwenda, katika klabu yae ya zamani ya Simba, ni uhusiano wake na mmiliki wa nafasi anayoicheza katika kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi, Shomary Kapombe.
Mengi yalikuwa yakizungumzwa mitaani kwamba wawili hao walikuwa hawazungumzi wala kupeana mikono chanzo kikitajwa kuwa ni uhasama wa kuwania namba hiyo ambayo Kapombe amejihakikishia kikosini kwa miaka mingi tangu aliposajiliwa na Simba Julai 1, 2017 akitokea Azam FC.
Kutokana na Kapombe kuelekea katika miaka yake ya mwisho ya kupiga soka la kiwango cha juu, wengi walitabiri mrithi wake angekuwa ni Mwenda, staa mwenye umri mdogo na kipaji kikubwa.
Lakini uvumi wa wawili hao kila mmoja kumwangalia mwenzake kwa jicho la wasiwasi, ulitajwa kuwa chanzo cha Mwenda kuomba kuondoka katika klabu hiyo, muda mfupi tu baada ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Simba.
Stori za mitaani zilidai kwamba Mwenda alisaini mkataba mpya baada ya kuahidiwa kwamba Kapombe atatemwa katika lile panga kubwa lililopita Msimbazi katika dirisha kubwa la uhamisho la kuingia msimu huu ambao Wekundu wa Msimbazi wamekuja na kikosi chenye nyota wengi wapya.

Ikadaiwa kwamba Mwenda alikuja kushtuka baadaye aliposikia Kapombe anaongezwa mkataba na akabaki, hivyo naye dakika za mwisho akaamua kuondoka katika kambi ya timu hiyo iliyokuwa ikijiandaa kuanza msimu huu wa 2024-25 na hivyo akalazimisha kuuzwa kwa Singida Black Stars, ambako ametumika kwa miezi sita tu kabla ya kutua Yanga katika dirisha dogo la uhamisho lililofungwa jana usiku..
Mwanaspoti imempata Mwenda ambaye kwa mdomo wake amefunguka kila kitu:
KILICHOMTOA SIMBA
Mwenda analiambia Mwanaspoti kuwa, mipango yake ilikuwa kucheza nje ya Bongo kwa muda mrefu kama ilivyo kwa wengine ila dili hilo lilimjia wakati mbaya.
Anasema kuwa, alitaka kuachana na Simba kama dau la timu hiyo lingepanda na alikuwa tayari kuvunja mkataba, jambo ambalo lilikuwa gumu kidogo.
“Kipindi naomba kuondoka Simba nilipata ofa ya nje ya nchi, lakini kilichokwamisha ni dau dogo, maana hiyo ofa niliipata nikiwa nimeongeza mkataba Simba, waliposhindwa kuongeza hela basi nikabaki.
“Kweli nina mpango wa kucheza nje na Bongo na lazima uwaze kwenda huko na hiyo ipo ila kutimiza ni wewe mchezaji kwa kufanya vizuri.

KUHUSU SIMBA
“Sijui kitu gani sitasahau au kukikumbuka Simba kwa sababu maisha yangu naishi tu sinaga hayo mambo ya kumbukumbu au kujutia.
“Sijawahi kutofautiana na mchezaji yeyote kama inavyoelezwa mitandaoni, ila ugomvi wa kawaida kazini kwa kila mtu upo.”
SAFARI YANGA ILIANZA HIVI
Israel ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea Simba lakini mwanzoni mwa msimu huu akatimkia Singida Black Stars, ghafla dirisha dogo ameibukia Yanga
Anaeleza jinsi safari hiyo ilivyokuwa, huku akiweka wazi kuwa ni mambo ya kawaida kwa mchezaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Nilipokea taarifa kutoka kwa wakala wangu, aliniambia nahitajika kwenda Yanga na mimi nikasema hakuna shida kwa sababu natamani kucheza timu kubwa na ukipata nafasi kama hiyo huwezi kusema uiache kwani ni wengi wanaitamani.
“Kwa hiyo nilikubaliana nayo kwani walifanya kila kitu ambacho wakala wangu aliwaambia. Basi nikasema sawa niko tayari kujiunga na Yanga.
“Nilipokuwa nachezea timu nyingine nilitamani sana kuchezea klabu kubwa kama Simba na Yanga, hatimaye ndoto imeatimia,” anasema Mwenda aliyewahi kuichezea Alliance Football Club ya Mwanza (2019/20 hadi 2020/21) ambapo alikuwa nahodha na baadaye kujiunga na KMC FC ya Dar es Salaam kwa msimu wa 2020/21.

TOFAUTI SIMBA, YANGA
Katika ligi ya Tanzania hizi ndio timu vigogo, huku rekodi zikionyesha katika msimamo wote wamecheza mechi 16 huku Simba ikiwa kileleni ikiizidi Yanga kwa alama moja tu.
Hapa Mwenda anaeleza utofauti wa timu hizi ulipo upande wa maisha na ushindani kwa ujumla.
“Nadhani kwenye utofauti katika hizi timu mbili haziachani sana kimaisha ila ushindani wake ni mkubwa sana, kama mchezaji utakuwa na kiwango cha chini muda wowote unaweza ukatolewa.
“Hizi timu zina mahitaji makubwa sana kwa mchezaji na unatakiwa uwe tayari kufanya vizuri ili uweze kusaidia timu, hivyo ni wewe kuwa fiti na kufanya vizuri ukipata nafasi.”
MATARAJIO
Mwenda anaweka wazi kuwa, anajipanga kufanya makubwa kila atakapopewa nafasi.
“Nitafanya kazi yangu ya kuhakikisha naisaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea, ikiwamo kushinda ubingwa kwenye mashindano yote tunayoshiriki.”

ALICHOMWAMBIA RAMOVIC
Mwenda anatua Yanga wakati ambao kocha wa kikosi hicho akiwa mpya kabisa Sead Ramovic na anasema alipata nafasi ya kuzungumza wakiwa wawili tu.
“Kocha alinielezea anachokihitaji na siwezi kusema, kwa sababu hiyo ni siri, nikisema niyatoe hapa nitawapa mbinu wapinzani, ila ni kocha mzuri sana ingawa nimefanya naye kazi kwa muda mfupi.”
WA KWANZA KIKOSINI
Mwenda ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakiunda kikosi cha vijana cha Serengeti Boys na moja kati ya timu ambayo ina wachezaji wengi kutoka huko ni Yanga. “Nilipofika kikosini watu wa kwanza kukutana nao walikuwa washikaji zangu wa Serengeti Boys, Kibwana Shomari, Dickson Job, Nickson Kibabage, Aboutwaleeb Mshery na wengine na hao ndio marafiki zangu wa tangu utotoni.
“Ni kweli nilikuwa natamani kucheza nao, unajua mtu ukikaa naye miaka zaidi ya mitatu unakuwa umeshafahamu udhaifu wake na mazuri yake pia kwa hiyo ni rahisi kufanya kazi.”

ANACHEZA NAFASI 4
“Nacheza kama beki wa kulia na kushoto, namba sita na winga ila aina ya winga ni sawa tu na beki ila utofauti ni kuzuia lakini ukicheza hiyo nyingine huzuii sana.”
USHINDANI
Nafasi anayoichezea yuko pamoja na Muivory Coast, Yao Kouassi, ambaye amefanyiwa upasuaji, na Kibwana Shomari, anaeleza alivyojipanga na ushindani wa namba.
“Ushindani kweli upo na hiyo ni kitu kizuri kwa timu kwa sababu kwenye nafasi moja ushindani ukiwa mkubwa ni vizuri kwa upande wa timu sio wachezaji.
“Unapofanya vizuri halafu ukapewa namba ukitoka anaingia mwingine ambaye anakwenda kufanya vizuri zaidi, kwa hiyo kwa upande wa timu inakuwa freshi, maana yake ukicheza vizuri timu itapata matokeo.”
ANACHOJIVUNIA
“Najivunia sana kupata nafasi ya kucheza Simba na Yanga ndani ya muda mfupi, unajua ni wachezaji wachache wanaweza kuweka rekodi hiyo kwa umri wangu.
“Kuna mtu anatamani acheze Yanga, mwingine Simba, Lakini mimi nimepata nafasi ya kucheza zote mbili hilo tu ni jambo la kushukuru sana na ninajivunia kwa historia hiyo.”
JAMBO GUMU ZAIDI
“Nashukuru Mungu sijapata changamoto ngumu zaidi kwani hii ni kazi niliyoichagua chochote nilichokutana nacho kwangu naona ni sehemu ya kazi. Sijawahi kujutia maana soka ndio kazi niliyochagua.”
MGUU MDOGO ZAIDI
“Wengi wanasema navaa kiatu kidogo zaidi kuliko wote hapa kambini lakini sio kweli kabisa, Kibabage anavaa sawa na mimi, Nkane na Kibwana pia.”
WINGA MSUMBUFU ZAIDI
“Nakumbuka kuna mechi moja hivi kipindi niko Alliance tulicheza dhidi ya Kagera Sugar, Erick Mwijage ile siku ndio ilikuwa mara ya kwanza ndio tumepanda Ligi Kuu alinikimbiza.
“Hapo mwanzo sikuwa na uzoefu wa ligi, hivyo kwangu Mwijage ndio winga aliyenisumbua na huo ndio mchezo mgumu zaidi kwa sababu nililala hoi.”