Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWAMEJA: Siri ya ushindi kila timu iko hapa

MWAMEJA: Siri ya ushindi kila timu iko hapa

KATIKA mfululizo wa mahojiano na kipa wa zamani wa Simba, Momammed Mwameja kazungumzia mambo mbalimbali akigusia safari yake Uingereza ilivyofeli kumpa alichokifuata, lakini pia Simba ilivyokuwa inapambana kuweka mambo sawa. Leo anakupa siri ya ushindi kwa kila timu akianza na michuano ya Afcon.


MECHI NA TIMU YA GEORGE WEAH

Mwameja anasema Ali Bushiri ndiye aliyekuwa mfano wake wa kuigwa na ndiye alimhamasisha kupambana kwenye timu ya taifa baada ya kumueleza kwamba wao tayari umri umesogea hivyo akaze ili awe mbadala.

“Ni kweli nilipambana. Nakumbuka kuna mechi tulikwenda kucheza na Liberia wakati huo George Weah akiwa anacheza AC Milan. Japo nilikaa benchi, lakini ile mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu Afcon ilikuwa ngumu sana kwetu nje ya uwanja,” anasema.

Wakati ule Liberia ilikuwa na vita na mechi yao ilichezwa kwenye uwanja wa Samuel Doe mmoja wa wababe katika kivita enzi hizo. “Weah alikuja na kuomba mapigano yasitishwe. Aliwaomba mashabiki kujitokeza na yeye mwenyewe atakuwepo uwanjani. Alikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi na kweli silaha ziliwekwa chini sababu ya mechi.

“Ila mtaani kabla ya mechi tulikuwa tunasikia milio ya risasi. Kuna muda mnapita maiti barabarani. Ilikuwa inatisha sana. Baada ya mechi mashabiki walikimbia kwa hofu, sisi tulitoka kwa eskoti uwanjani na kurudi hotelini ambako baadaye tulikwenda Ivory Coast na kurudi nyumbani.”

Anasema katika mechi hiyo walitoka sare, japo hakumbuki vyema mechi nyingine, lakini walikosa pointi moja kufuzu Afcon kwa kutocheza mechi ya marudiano Sudan.


UONGOZI WA MPIRA

Licha ya baadhi ya wadau wa soka kumshawishi Mwameja kujitosa kwenye uongozi wa soka nchini, kipa huyo anasema hajawahi kufikiria hilo.

“Nimepata mawazo mengi ya watu, ila niko mpirani kwa miaka 29 nikiwa nje ya familia kwa muda mrefu. Hivyo nimeona sasa uwe muda wa kuwa na familia ambayo nilipoamua kustaafu ilifurahi sana,” anasema kipa huyo.

Anasema vitu ambavyo anavichukia ni kuwa kocha wa mpira Tanzania - kazi anayodai makocha wazawa wanadharaulika.

“Yale ya msingi wakiyahitaji hawapati kama ilivyo kwa wageni. Pili, timu inapofanya vizuri nafasi yake ni ndogo, anasifiwa hadi mganga lakini yeye haguswi. Sasa pale inapofanya vibaya wa kwanza ni yeye.

“Japo makocha wetu ni wazuri sana, sisi fainali Caf tumecheza hatukuwa na kocha kutoka nje - wote walikuwa wazawa lakini wanacheleweshwa na kutopata sapoti ya kutosha kwenye klabu zetu,” anasema.

Anasema walicheza fainali Caf wakinolewa na Abdallah Kibaden na Salum Madadi ambao leo hii ni miongoni mwa makocha wake watano bora nchini.

“Kibadeni ni kocha ambaye akikuambia kitu ukakifanyia kazi unapata matokeo chanya. Ma-dadi pia namkubali sana hata Charles Boniface Mkwasa ni makocha bora ambao kama nchi tunashindwa kuwatumia kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha kwenye mipango yao, ila kama wakitimiziwa kile wanachokihitaji kwenye mipango yao, hata baadhi ya makocha wetu wa kigeni tunaowaleta hawafui dafu kwa hawa wazawa,” anasema.


SOKA NCHINI

Mwameja anasema kwa viwango vya klabu soka la Tanzania limepanda na pia kuonyeshwa laivu kumeongeza hamasa.

“Waamuzi wetu wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara, lakini hata wale wa nje pia wanafanya makosa japo wenzetu wanasaidiwa na baadhi ya vitendea kazi, wetu bado wanashindwa kwenda na kasi ya mpira. Ile kasi inawaacha, lakini wana mazuri yao ingawa wanapaswa kuwa makini. Waongeze kasi ili wawe bora zaidi.

“Kwa wachezaji wa kigeni wamekuja kuleta mabadiliko na kutupa chalenji. Wanatuamsha ili tusijisahau, japo huwa najisikia vibaya nikiona tuzo ya kipa bora, beki bora au mshambuliaji bora zinachukuliwa na mtu wa nje. Inaumiza waje kutuamsha na kutusaidia wasitufanye kubweteka,” anasema.


USHIRIKINA SIO SIMBA NA YANGA TU

Licha ya klabu kongwe za Simba na Yanga kutajwa zaidi kwenye ushirikina, Mwameja anasema mambo hayo kwenye mpira yapo sana na sio kwenye klabu hizo tu.

“Klabu nyingi nilizopita sio Simba tu, nyingi nilizopita mambo hayo nimeyakuta, nimeyaishi na bila kufanya hivyo mchezaji unaitwa msaliti. Yanaenda na saikolojia, yanakufanya kukuongezea morali na kuna baadhi ya wachezaji bila hayo mambo hawasikii raha.

“Sio Simba na Yanga tu, klabu nyingi zinafanya. Nilikotoka nimeyakuta yapo na huwezi kuyakataa, nimeyaishi na kuyaacha baada ya kuondoka, ila hayasaidii - sema ndiyo hayaepukiki kwenye mpira wetu japo ukiwa na nidhamu, ukimsikiliza kocha na bidii utafanikiwa zaidi kuliko hayo mambo,” anasema Mwameja.

Anasema kwenye klabu za mpira sio jambo la mtu mmoja au wawili ni la watu wengi na wengine ni wanachama au wapenzi ambao wana watu wanaoamini wakiwapeleka kwenye timu zitafanya vizuri. “Huyo mpenzi au mwanachama anawafuata viongozi na viongozi wanaridhia wanampeleke kambini kwa wachezaji. Vitu hivyo vinafanyika mnaweza kupewa vitu mvae kwenye jezi na mambo kama hayo.”


KUVUNJIKA BEGA

Kabla ya kutua Simba, Mwameja anasimulia namna ambavyo aliumia bega na kufifisha ndoto za kucheza soka 1989 tukio ambalo lilimfanya ajute baada ya kukosa huduma mu-himu.

“Ilikuwa ni kwenye mechi yetu ya mwisho ya msimu kati ya Coastal na African Sports niligongana na mchezaji wa Sports nikavunjika bega,” anasema Mwameja.

“Nilikaa nje ya uwanja mwaka mzima. Nilijuta sababu sikupata huduma muhimu hata ndoto yangu ya mpira iliyeyuka. Daktari wa Coastal anaitwa Mganga alikuwa msaada mkubwa kwangu hadi nikapona. Alinitia moyo na kuniambia majeraha kama yangu watu wanapata na kupona hivyo hata mimi nitapona,” anasema.

Mwameja anasema kipindi hicho aliamua kuachana na mpira, japo kuna mzungu mmoja alikuwa Coastal Union alimtafuta akamsihi kurudi uwanjani.

“Nilimwambia naona giza kwenye ndoto zangu akasema hapana rudi mpirani nakuona bado una nafasi ya kufanya kikubwa zaidi, ishi kwenye ndoto zako. Yale maneno yalinifariji nikaona kumbe naweza kurudi, kikubwa ilikuwa ni matibabu kwa wakati na ubora, niliyapata nikawa sawa na nikarudi Coastal.”


SOKA LAMPA MKE

Mwameja anasema katika soka, jambo kubwa alilopata ni mchumba ambaye alikuja kuwa mkewewe na wanaishi wote mpaka sasa.

“Unapokuwa hujaoa na ni maarufu kuna vitu unapitia. Binafsi kusafiri na timu kumesababisha nipate mke mwema japo alikuwa haji mpirani ila katika safari zangu za mpira nikamuona tukapendana na nikaja kumuoa,” anasema.

“Hicho ndicho kitu najivunia katika miaka 29 kwenye soka, kumefanya nipate mke mwema ni Mtanzania na nilimpata hapahapa Tanzania.”


BILA SINDANO HAKUCHEZA

Katika maisha yake ya soka Simba, Mwameja anaeleza namna alivyoishi kwa kuchomwa sindano za ganzi ili acheze kipindi cha miezi sita.

“Sikuweza kufanya chochote bila sindano japo nilifanya hivyo kwa mapenzi ya timu yangu, lakini maumivu niliyopitia baada ya ganzi kuisha hayakuwa yanaelezeka,” anasema Mwameja.

Anasema alipata maumivu ya goti, lakini hakwenda kutibiwa kwa wakati baada ya wachezaji wenzake kumuomba aendelee kuitumikia timu.

“Nilishindwa kukataa kwa kuamini wachezaji wenzangu wameona umuhimu wangu, nikajikuta naishi kwa kuchoma sindano za ganzi kwa miezi sita mfululizo ili niendelee kucheza japo viongozi waliniahidi kunipeleka kwenye matibabu Ujerumani wakati wa mapumziko ya ligi.

“Waliniambia wewe cheza tu sisi tutakutibia. Kuna muda ulifika natolewa nyuzi ili nicheze. Simba nimepitia vipindi vya raha na shida. Kuna muda unagombana na mwenzako nyumbani baada ya ganzi kuisha maumivu unayopata hulali, yote sababu ya Simba.”

Anasema baadaye Simba walimpeleka Ujerumani kwenye matibabu ambako alikaa wiki tatu na kurejea nchini ambapo alitakiwa kupumzika kwa miezi miwili na kurudi tena uwanjani.

Anasema mpira umehamisha mkoa aliozaliwa - Tanga na kuwa na makazi ya kudumu Dar es Salaam, lakini pia umempa marafiki wengi tofauti na maadui.


KUHUJUMU TIMU

Akizungumzia maneno yanayoibuka kuwa timu huhujumiwa na yanavyowatesa wachezaji, Mwameja anasema: “Haya mambo huwezi kuyakataa - yapo, wakati mwingine mpira unakuchagulia hadi marafiki, usiongee na kiongozi au mchezaji wa Yanga kisa tu wewe ni Simba. Wachezaji ilifika wakati kama mna ugomvi sababu tu ya Simba na Yanga kwa kuhofia kuambiwa umeihujumu timu, kila mmoja anaangalia klabu yake, lakini baadaye mnakuwa marafiki.”

Katika safari ya miaka 29 ya Mwameja kwenye soka anaeleza namna alivyoitwa kwenye timu ya taifa kwa mara ya kwanza akitokea timu ya Coastal Union.

“Nilikuwa mchezaji wa akiba nilipopata nafasi nikaitendea haki. Wakati ule timu za Ligi Kuu zilikuwa na watu wenye ubora na vipaji katika nafasi tofauti tofauti.

“Ukienda Pamba, Tukuyu, Coastal, Lipuli na timu nyingine kila moja ilikuwa na watu, (Taifa) Stars ilikuwa inapata wachezaji wa nafasi tofauti kutoka timu tofauti tofauti wote wako kwenye viwango, Stars ilisheheni,” anasema mkongwe huyo.


USHINDI TIMU UKO HAPA

Mwameja anaamini kuwa kipa katika timu yake ni mhimili mkuu kwa ajili ya mafanikio na timu ikiwa na kipa mzuri na mabeki wazuri nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa inakuwepo.

“Sio Tanzania tu kote duniani, timu ikiwa na kipa mzuri na beki imara ina nafasi kubwa ya ubingwa kwa kuwa sio rahisi kufungwa, hivyo ikitokea mkapata bao moja ni rahisi kumaliza mechi kwa ushindi huohuo, tofauti na timu yenye washambuliaji wazuri halafu ina kipa mbovu na beki mbovu,” anasema Mwameja.

Anasema alichojifunza kwenye safari yake ya soka ni kuwa kama wangepata viongozi wa mpira wenye maono wakati ule basi leo hii Tanzania ingekuwa na nyota wengi wa soka ambao wamecheza kwa mafanikio katika timu mbalimbali nje ya nchi. “Wakati ule tulikuwa na uwezo na vipaji, lakini viongozi wengi walituzuia kwenda kutafuta maisha mengine ya soka nje ya nchi.

“Zamani ukiwa staa timu haikubali kirahisi kukutoa kwenda kwenye majaribio au kukuuza nje ya nchi. Mimi ukiachana na sekeseke langu la Uingereza, lakini nimewahi kurudishiwa uwanja wa ndege mara mbili.

“Awali nilikuwa naenda Afrika Kusini na safari nyingine ilikuwa ya Swaziland. Ilipigwa simu tu nikaambiwa bwana umeambiwa usiondoke na klabu yako au unaweza kuambiwa waziri amekataa usiende na ndiyo imeisha hivyo,” anasema.

Mwanasoka huyo anasema kama ingekuwa wakati wao ndiyo wanakutana na mazingira ya soka ya sasa, bila shaka Tanzania ingekuwa na kina Mbwana Samatta wengi.

Anasema hivi sasa viongozi wa soka na nchi wameweka mazingira mazuri kwa wachezaji, ingawa wanapaswa kuwa wabunifu zaidi na mashabiki pia wakosoe au kusifia panapostahili.

Anasema sio vizuri mtu anapomchukia mchezaji kila analofanya uwanjani alione ni baya au kwa kuwa anampenda mchezaji fulani kila anachofanya hata kama si kizuri basi amsifie.