MWAMBUSI KAONDOKA NA ALAMA ZAKE YANGA SC

Muktasari:

BEKI Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wakati anatoka Klabu ya LA Galaxy inayocheza Ligi Kuu Marekani, lengo lake la kujiunga na Yanga mwaka jana lilikuwa ni kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, lakini alijikuta hesabu zake zinakwenda ndivyo - sivyo hadi alipotokea mkombozi wake, Juma Mwambusi.

BEKI Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wakati anatoka Klabu ya LA Galaxy inayocheza Ligi Kuu Marekani, lengo lake la kujiunga na Yanga mwaka jana lilikuwa ni kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, lakini alijikuta hesabu zake zinakwenda ndivyo - sivyo hadi alipotokea mkombozi wake, Juma Mwambusi.

Ninja alikwenda kucheza LA Galaxy kwa mkopo akitokea MFK Vyaskov ya Jamhuri ya Czech iliyomsajili kutokea Yanga mwaka 2019. Baada ya kumaliza muda wa kukaa Marekani, alivunja mkataba wa miaka mitatu uliokuwa umebakia na kurejea Yanga.

Tangu msimu huu (2020/21) uanze, Ninja chini ya kocha Zlatko Krmpotic na Cedrick Kaze waliofutwa kazi Yanga, kwa nyakati tofauti hakuwa na nafasi hata ya kukaa benchi na alikuwa kati ya wachezaji waliokuwa wanapigiwa hesabu ya kuondolewa kupitia dirisha dogo.Hata hivyo, kilichombakiza ni baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Baada ya uongozi wa Yanga kumtimua Kaze, Mwambusi alipewa majukumu ya kukaimu na alifanikiwa kuwarejesha kwenye mstari baadhi ya mastaa ambao walianza kupotea kiana kwenye ramani ya kuwa wachezaji muhimu Yanga.

Mwanaspoti linakuchambulia mastaa ambao Mwambusi amewainua upya na wanaonyesha uwezo wa kuisadia Yanga katika mechi ambazo wamecheza chini yake, akiwemo Ninja ambaye usajili wake ulitikisa kutokana na kutoka nje kurejea ligi ya ndani.


NINJA

Chini ya Mwambusi, beki huyo amecheza dakika 270 - kwa maana ya mechi tatu dhidi ya KMC (sare ya bao 1-1), Biashara United (waliyoshinda bao 1-0) na Gwambina FC (mabao 3-1), ambapo alianza dakika ya kwanza hadi ya 90. Baada ya kuja kocha mpya, Nasreddin Nabi naye kumpa dakika 90 dhidi ya Azam FC, hivyo amecheza dakika 360, ambapo huduma yake ilikuwa na manufaa ya kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao.

ADEYUN SALEH

Beki namba tatu, Adeyun Saleh, hakuwa na nafasi kubwa chini ya makocha waliotimuliwa. Baada ya Mwambusi kukaimu nafasi hiyo alimwamini na kumuanzisha mechi tatu zilizochezwa chini yake kabla ya Nabi kukabidhiwa majukumu hayo, ambapo naye alimuanzisha dhidi ya Azam FC.


DICKSON JOB

Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu alianza kukitumikia kikosi hicho chini ya Mwambusi. Alikaa benchi dhidi ya KMC, akianza dhidi ya Gwambina na Biashara United ambapo mashabiki wameuona mchango wake kama mchezaji anayetumia akili zaidi licha ya umbo lake kuwa dogo tofauti na wanavyoonekana Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto na Ninja.


SAIDi NTIBAZONKIZA

Alianza mechi mbili dhidi ya KMC na Biashara United, na kuingizwa kipindi cha pili dhidi ya Gwambina ambapo baada ya kufunga bao la tatu Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Saido alionekana kukasirika na kutoka nje. Jambo hilo lilizua sintofahamu kidogo baina yake na kocha Mwambusi.

Sio kwamba hakucheza kabisa chini ya Kaze, alicheza mechi chache (dakika 280), ambapo alifunga mabao matatu na kuasisti nne za mabao. Kocha huyo alikiongoza kikosi hicho katika mechi 18.


CARLOS CARLINHOS

Carlos alikuwa haanzi mara kwa mara chini ya Kaze, lakini baada ya Mwambusi kupokea majukumu alikosekana dhidi ya KMC, lakini mechi dhidi ya Biashara United, Gwambina alianza na ya Azam FC ambayo kocha alikuwa Nabi. Anatumia akili kubwa kumeneji mipira na namna ya kutoa pasi makini. Ukiachana na hilo ni mtaalamu wa kupiga kwa vipimo mipira ya faulo.


ALAMA ZA MWAMBUSI

Katika mechi tatu ambazo Mwambusi alikiongoza kikosi hicho alishinda mechi mbili dhidi ya Biashara United (bao 1-0), Gwambina FC (mabao 3-1) na sare dhidi ya KMC (bao 1-1). Hivyo alivuna pointi saba na mabao matano.