Mwamba Sergio Ramos anasepa, wa kuziba pengo nani?

SERGIO Ramos hajasaini mkataba mpya. Mkataba wake na Real Madrid aliyoichezea kwa miaka 15 akitumika katika zaidi ya mechi 468, tangu mwaka 2005, alipojiunga nayo akitokea Sevilla, unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Kwa umri wake wa miaka 34, kwa mafanikio aliyopata akiwa na Real Madrid, ni dhahiri kuwa, hata kama ataamua kuongeza mkataba, haitokuwa zaidi ya mwaka mmoja au miwili. Maana yake ni kwamba Mhispania huyu anakaribia kuondoka Santiago Bernabeu.

Muda wa kuondoka utakapofika, Ramos ataacha pengo kubwa Real Madrid. Hata kama Los Blancos watapata nahodha mwingine. Hata kama atapatikana beki mwingine, itakuwa ngumu kumpata Sergio Ramos mwingine. Ila hawa watano wanaweza kuziba pengo lake.


5. Diego Carlos

Beki huyu wa Sevilla ana nguvu, kasi na akili. Diego Carlos amekuwa nguzo kuu katika safu ya ulinzi ya Andalusians kwa misimu miwili. Mbrazil huyu ndio chanzo cha ubabe wa Sevilla tangu alipotua akitokea Nantes, mwaka 2019.

Carlos ni mzuri hewani, ni mzuri akiwa na mpira miguuni pia. Tofauti yake na Sergio Ramos ni kuwa ni nadra sana kumkuta Diego Carlos akifanya rafu za kizembe. Huwa ni makini na ‘tackles’ zake ni za kijanja sana. Sio beki wa kupigwa kadi kizembe.

Diego Carlos, ndio kwanza ana miaka 27, maana yake ni kwamba bado ana muda mrefu wa kucheza soka. Mkataba na Sevilla uko hadi 2024. Hii itamaanisha kuwa itabidi Real Madrid itumie fedha nyingi kumsajili licha ya Sevilla kupitia wakati mgumu kiuchumi.


4. Pau Torres

Huyu amehusishwa na Real Madrid kwa muda sasa. Pau Torres mwenye umri wa miaka 23, ni nguzo kuu kwenye safu ya ulinzi ya Villarreal. Tayari yupo timu ya taifa ya Hispania. Alicheza sambamba na Ramos kwenye michuano ya mwaka huu ya UEFA Nations League.Kama kuna mtu anayeweza kuvaa vizuri viatu vya Ramos basi ni Mhispania huyu. Akiwa ni mchezaji anayetumia mguu wa kushoto, Torres ataweza kurudisha utulivu kwenye beki ya Real Madrid. ametulia akiwa na mpira mguuni na anapenda kupiga pasi ndefu.

Pau Torres ni mrefu na fundi wa kushambulia kwa kushtukiza. Mkataba wake na Villarreal unamalizika mwaka 2024. Mtihani mkubwa kwa Real Madrid, ni dau la beki huyu. Ili kumpata lazima Fiorentino Perez awe tayari kutoa Euro 50 milioni.


3. Dayot Upamecano

Beki wa RB Leipzig, Dayot Upamecano, ana-mezewa mate na klabu nyingi za Ulaya. Chelsea, Manchester United, Manchester City, Liverpool na Arsenal zote zinamuhitaji. Hii inatokana na ufanisi mkubwa aliouonyesha na kiwango kikubwa alichokuwa nacho msimu uliopita.

Aliisaidia klabu hii kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Upamecano ni mmoja wa mabeki wababe zaidi duniani. Ana nguvu, kasi na akili pia. Uwezo wake wa kufikiria ni mkubwa. Upamecano ni fundi wa kuanzisha mashambulizi.

RB Leipzig inamtegemea sana, katika kushambulia hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi za uhakika. Akiwa na miaka 22, bado ana umri mrefu wa kucheza soka. Mfaransa huyu hawezi kupatikana kirahisi, lazima Los Blancos wajiandae kuvunja benki.


2. Jules Kounde

Jules Kounde ni beki mwingine wa kati wa Sevilla kwenye listi hii ya mabeki wanaopigiwa upatu kuvaa viatu vikubwa vya Sergio Ramos. Kwa mujibu wa Defensa Central, Mfaramsa huyu mwenye umri wa miaka 22, ndio chaguo la Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane.

Haikumchukua muda mrefu kutangaza ufalme wake katika kikosi cha Sevilla baada ya kujiunga nayo akitokea Bordeaux mwaka 2019. Manchester City, walipobisha hodi kutaka sajili yake mwaka jana, Sevilla waliweka ngumu, na kusisitiza kuwa haendi kokote.

Kingine ni kwamba dau la beki huyu ni Euro 90 milioni, fedha ambazo City walishindwa kutoa. Hata hivyo, hali mbaya ya kiuchumi inayokabili Sevilla kwa sasa inaweza ikaharakisha uhamisho wake kama Real Madrid wataamua kuingia sokoni kuitaka saini yake.


1. David Alaba

Viatu vya Sergio Ramos vinahitaji mtu aliyekomaa na mwenye uzoefu. Kwenye orodha hii nzima mtu huyo ni beki wa Bayern Munich, David Alaba. Alaba, huenda akajiunga na Los Blancos, mwanzoni mwa msimu ujao baada ya kandarasi yake na Bayern kumalizika.

Licha ya kuwa sehemu ya kikosi cha mafanikio cha Bayern Munich katika kampeni yao msimu uliopita, ambapo walitwaa mataji matatu, ikiwamo ubingwa wa Ulaya, Alaba mpaka kufikia sasa hana uhakika kama ataendelea na maisha pale Allianz Arena.

Alaba, anakaribia kumaliza mkataba wake, na huenda ndoa yake na Bavarian ikaisha muda wowote. Kwa mujibu wa mtandao wa Marca, tayari ameshakubali kutua Santiago Bernabeu, kilichobaki ni kusaini tu. ujio wake utabusti kiwango cha kikosi cha Zinedine Zidane.

Alaba anaweza kucheza kama beki wa kati. Anaweza kutumika kama beki wa kushoto. Kwa ufupi, Los Blancos wakimchukua, watakuwa wamepata beki kiraka. Alaba ana kasi, akili nyingi, ubabe na uwezo wa kusaidia katika kujenga mashambulizi.

Imeandikwa na FADHILI ATHUMANI