Mutale ilikuwa lazima aage Simba
Muktasari:
- Japo Simba haijanuaga rasmi mchezaji huyo, kijiwe kimenasa habari za uhakika haitoendelea naye baada ya kumtoa kwa mkopo msimu uliopita.
NI wazi Simba haitoendelea na Joshua Mutale hivyo katika msimu ujao, mchezaji huyo wa Zambia hatokuwa katika kikosi chao.
Japo Simba haijanuaga rasmi mchezaji huyo, kijiwe kimenasa habari za uhakika haitoendelea naye baada ya kumtoa kwa mkopo msimu uliopita.
Kimsingi Simba imechelewa tu kumpa mkono wa kwaheri Joshua Mutale lakini hakupaswa hata kuwepo msimu uliopita.
Wakati hapa kijiweni tulipokuwa tunasema kwamba sio aina ya mchezaji ambaye anaweza kuisaidia Simba, wapo mashabiki waliooga maji ya bendera waliona kama tunamchukia.
Lakini kiuhalisia Mutale ni mchezaji machachari na sio hatari na ndio maana ndani ya muda mfupi wamekuja watu ambao wamelithibitisha hilo.
Libasse Gueye ndani ya miezi sita tu aliyoichezea Simba, tayari amehusika na idadi kubwa ya mabao kuzidi ile ambayo Mutale amechangia katika muda wote alioichezea Simba.
Pia ndani ya uwanja, Gueye ana yale machachari ambayo Mutale alikuwa anajifichia.
Na hii sio kwa Gueye tu bali pia hata kwa Anicet Oura aliyeongezwa katika dirisha dogo.
Ukiwatazama hao wawili wanavyocheza, huoni ni wapi Mutale angetoboa.