Prime
MUSONDA: Tatizo lilikuwa Mayele, ila nataka kucheza hapa!
Muktasari:
- Ndio, Yanga ni Prince Dube aliyesajiliwa msimu huu, lakini pia kuna Clement Mzize ambaye pamoja na Musonda ni wazoefu ndani ya timu hiyo kwani walikuwepo zaidi ya msimu mmoja, mbali na nyota wengine wanaoisaidia Yanga kufanya mambo makubwa katika ligi ya ndani na kimataifa.
KIKOSI cha Yanga kina washambuliaji ambao ni tishio kwa mabeki wa timu pinzani, lakini mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa wakichanganywa na namba za Mzambia Kennedy Musonda.
Ndio, Yanga ni Prince Dube aliyesajiliwa msimu huu, lakini pia kuna Clement Mzize ambaye pamoja na Musonda ni wazoefu ndani ya timu hiyo kwani walikuwepo zaidi ya msimu mmoja, mbali na nyota wengine wanaoisaidia Yanga kufanya mambo makubwa katika ligi ya ndani na kimataifa.
Hata hivyo, Musonda amekuwa na maisha flani yasiyoeleweka, kwani kuna wakati anakuwa anawaka kisha ghafla anazimika, lakini Mwanaspoti lilimsaka nyota huyo wa timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo) kufanya mahojiano naye kujua ukweli wa hali hiyo, naye akazungumza mengi.
Pia ameweka bayana namna straika wa zamani wa timu hiyo, Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri alivyochangia kiasi kikubwa kumtibulia mbali na kuweka msimamo wake timu gani anayotamani kuichezea kama ataondoka nchini. Endelea naye...!
AIPOTEZEA MAZEMBE
Musonda alisajiliwa Yanga katika dirisha dogo la usajili la misimu miwili iliyopita, ikiwa na maana Januari hii anatimiza misimu kamili akiwa na kikosi hicho.
Nyota huyo anakiri kwama imekuwa misimu yenye milima na mabonde, kwani kila msimu amekuwa akipata mzuka wa kikosi hicho kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa ni mara mbili sasa pamoja na Kombe la Shirikisho pia mara mbili sawa na Ngao ya Jamii.
Musonda ambaye amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi hicho kutokana na mabao muhimu ambayo amekuwa akiyafunga kuibeba Yanga tangu alipojiunga nayo anafichua safari nzima ya kuibukia Yanga iliyomtambulisha Januari 13, 2023 na miezi michache kubeba ubingwa wa ligi na Kombe la Shirikisho kisha kufika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.Anasema wakati Yanga inamsajili alikuwa na ofa mbili mezani ikiwamo ya TP Mazembe na nyingine ya mabingwa hao wa soka Tanzania, lakini aliamua kukubali kuja kufanya kazi Tanzania na kufafanua sababu iliyomfanya achukue hatua hiyo.
“Nafikiri kwangu niliipenda Yanga. Niliamua hivyo baada ya kuona mpango wa mradi wa timu. Haikuwa na maana kwamba ulitumika ushawishi mkubwa wa fedha, lakini kitu muhimu ilikuwa kuvutiwa na namna mambo yalivyokuwa yamepangiliwa kama klabu baada ya kuzungumza kwa kirefu na rais wa klabu, Hersi (Said) nikaona nije kufanya kazi hapa,” anasema.
“Hadi sasa naona kwamba sikufanya uamuzi mbaya kuchagua kuja kufanya kazi hapa. Yale ambayo niliyaona yapo na kitu muhimu ni kuendelea kupambana na changamoto za kawaida ambazo mchezaji mwingine yeyote angekutana nazo.”
KWANINI CHIPOLOPOLO
Mashabiki wa Yanga wanachanganyikiwa wanapomuona Musonda hafungi sana akiwa klabuni kwao, lakini anafunga sana akienda timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ na hapa anawapa majibu.
“Labda nikuulize wewe na mashabiki ni mara ngapi wameniona nacheza kama mshambuliaji wa kati hapa Yanga? Nilipofika hapa nilimkuta Mayele (Fiston) ambaye alikuwa anacheza kama mshambuliaji wa mwisho. Kwa muda wote mimi nikawa napewa nafasi nyingine pembeni, lakini nikienda timu ya Taifa nitacheza kama mshambuliaji wa mwisho,” anasema Musonda.
“Unapocheza mbali na uso wa goli kuna ugumu sana kuweza kufanya ambacho unacho. Mimi ni mshambuliaji halisi ndio maana unaona nikipewa nafasi ya kucheza nafasi ya mshambuliaji huwa nafunga, lakini nikitakiwa kucheza mbali lazima mambo yatakuwa magumu. Lakini, mimi ni mchezaji siwezi kukataa kocha akitaka nicheze eneo gani kwa kuwa tunatafuta mafanikio ya timu.
“Naomba mashabiki waelewe mimi ni mshambuliaji wa kati halisi. Nikicheza hapo watayaona mabao, lakini naweza kucheza sehemu zingine kama kutokea pembeni ikitegemea na mpango wa kocha anataka tucheze vipi dhidi ya timu ipi.”
UBINGWA MSIMU HUU
Nyota huyo anapoulizwa kwa namna anavyoiona Ligi Kuu Bara ilivyo na upinzani, anafikiri Yanga inaweza kutetea tena ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo na wa wa tatu mfululizo kwake tangu atue katika timu hiyo, naye anajibua:
“Bila shaka inawezekana kwanini isiwezekane? Kila kitu kinawezekana hatutakiwi kuruhusu mechi mbaya tulizopitia ziamue juu ya msimu wetu mzima. Ligi bado iko wazi sana. Tunatakiwa kuendelea kubadilika kurudi njia ya ushindi kama ambavyo tunafanya.
“Nafahamu ushindani ni mkubwa, lakini tuna timu imara na benchi zuri la ufundi. Uongozi ni uleule na mashabiki wetu ni walewale. Kwa hiyo tunatakiwa kuendelea kushirikiana kupigania malengo yetu kwa pamoja. Tuna tofauti ya pointi moja dhidi ya timu inayoongoza ligi na mechi bado zipo nyingi, nani anajua kipi kitatokea. Mimi naamini tutachukua tena huu ubingwa.”
USHINDANI WA LIGI ANAUONAJE?
Kuhusu ushindani katika Ligi Kuu Bara inayotajwa kuwa ya sita Afrika, mchezaji huyo anasema kuna mengi yanayoifanya iwe hivyo.
“Nafikiri ligi inaendelea kukua. Naona udhamini unazidi kuongezeka. Unaona namna kuna usimamizi mzuri licha ya makosa ya waamuzi. Mechi nyingi zinaonyeshwa moja kwa moja ambazo zinasaidia hata waamuzi kuona tabia za wachezaji,” anasema.
“Kwa upande wangu naona kuna maendeleo makubwa, hata ushindani wa timu unazidi kukua. Sio rahisi kuona mnapata ushindi kwenye mechi, inatakiwa muonyeshe ubora ili mpate matokeo. Kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa wako hapa na wanaendelea kuja. Hii yote inaonyesha ukomavu wa ligi.”
RAMOVIC KOCHA WA AINA GANI?
Musonda yuko ndani ya Yanga akitumika chini ya kocha wa tatu akianzia kwa Nasredine Nabi, Miguel Gamondi na sasa Sead Ramovic, na hapa anaeleza ubora wa kocha huyo mpya Mjerumani.
“(Ramovic) ni kocha mzuri sina tatizo naye lolote. Anataka sana kuona mchezaji wake anajitoa zaidi. Anataka kuona wachezaji wake wako fiti muda wote. Aisi kama wachezaji jukumu letu ni kufanya kile anachotaka ili tupate mafanikio. Sisi ndio silaha kwa kocha, jukumu letu ni kufuata programu zake.”
MTU WA FAMILIA
Ukiacha Musonda unayemuona uwanjani, nje ya soka mshambuliaji huyo ni mtu wa familia, ataonekana na watoto wake na mkewe kidogo pamoja na marafiki, lakini hapa anaeleza maisha yake yapoje.
“Nimekuwa hivyo na huhama na huo utaratibu tangu nikiwa kwa wazazi wangu. Wazazi walikuwa watu wanaopenda kuona tunakaa kama familia pamoja. Sio kwamba haya ninayoyafanya yalikuja tu kwa bahati mbaya, hii ni kama asili yetu,” anasema.
“Hata watoto wangu baadaye watakuja kufanya kama hivi kwa kuwa sasa wanaishi kwenye maisha hayohayo. Hiki ni kitu cha kawaida na wala siigizi, lakini nafurahi kuona watu wanafurahia hilo.”
TOFAUTI LIGI ZAMBIA NA TANZANIA
Kuhusu ligi za mataifa hayo mawili, Musonda ana jambo la kuzizungumzia.
“Ligi ya Tanzania ina wadhamini wengi na kuna hela ya kutosha. Inatangazwa pia kwa kuwa mechi nyingi zinaonyeshwa. Kwa sasa pia kuna wachezaji wengi wazuri, lakini ligi ya Zambia nayo pia ni ya ushindani,” anasema mchezaji huyo.
“Ligi ya Zambia hata timu kubwa zinaweza kupoteza mechi zaidi ya moja tofauti na hapa Tanzania. Hizi timu kubwa za hapa zinaweza kumaliza msimu zikiwa zimepoteza mechi moja au mbili, lakini kule ni zaidi kwa kuwa ushindani ni mkubwa. Mwisho naweza kusema ligi ya hapa ina mvuto mkubwa kwa kuwa klabu zina mashabiki wengi na watu wa hapa wanapenda sana klabu zao kulinganisha na Zambia.”
MALENGO MSIMU HUU
Kila mchezaji ana malengo na kwa Musonda msimu huu ana jambo lake.
“Malengo yangu ya kwanza nataka msimu huu niongeze muda wa kucheza kulinganisha na misimu iliyopita na baada ya hapo nataka nimthibitishie kocha mpya kuwa naweza kucheza eneo ambalo nahitaji kucheza ili sasa nifunge mabao ya kutosha, ndio maana nipo hapa kama mshambuliaji,” anasema.
KUCHEZA NA CHAMA YANGA
Musonda na Clatous Chama wote ni nyota wa kimataifa wa Zambia na kabla ya Chama kutua Jangwani alikipiga Simba alikopata mafanikio makubwa. Kutokana na hayo, Musonda katika mahojiano haya akatia neno kucheza pamoja na Mzambia mwenzake katika kikosi cha Yanga.
“(Kucheza na Chama) haikuwa habari mpya kwa kuwa tulikuwa tunakutana sana tukiwa timu ya taifa lakini aliposajiliwa hapa (Yanga) ilikuwa ni kama mwendelezo wa kucheza kwetu pamoja. Hata alipokuwa Simba kuna nyakati baada ya majukumu yetu tulikuwa tunaonana na kuzungumza kama familia, hivi sasa tupo naye hapa tunafanya mazoezi pamoja,” anasema.
Anaongeza kuwa, :”Chama ameanza vizuri Yanga. Huyu ni mchezaji ambaye analeta kitu tofauti kwenye soka, anahitaji muda kidogo. Alikuja hapa akakuta tukiwa na kocha mwingine na sasa ndani ya muda mfupi kaja mwingine. Haya yote yanatokea ndani ya muda mfupi akiwa ameingia kwenye timu. Huyu ni mchezaji mkubwa akijipata sawasawa itakuwa safi zaidi kwa timu yetu.”
MABAO YAKE MATAMU
Akizungumzia mabao aliyowahi kufunga, mchezaji huyo anasema: “Bao nililofunga kwenye fainali ya Azam (FA) kule Tanga lilikuwa muhimu sana. Kama utakumbuka tulikuwa tunakwenda kucheza fainali dhidi ya timu ngumu na washambuliaji wenzangu karibu wengi walikuwa wameondoka nchini kwenda timu ya Taifa.
“Nakumbuka kocha wakati huo (Nasreddine Nabi) alinifuata na kuniambia kwamba nimebebe matumaini yote ya timu kwenye mchezo ule na klabu inalitaka kombe, na bahati nzuri nikafunga bao pekee lililotupa ubingwa.
Lilikuwa ni tukio ambalo nitalikumbuka sana ukizingatia kwamba wakati huo tangu nimefika (Tanzania) nilikuwa sipati nafasi ya kucheza kama mshambuliaji wa kati.
“Bao lingine ni lile nililowafunga Simba kwenye mchezo wa watani wa jadi. Hizi mechi nyingi nilizofunga nilikuwa nacheza kama mshambuliaji wa kati na hata hii ya Simba nilicheza hapo, na kufunga bao zuri la kichwa, lakini kitu kitamu ni kwamba nilifunga bao kwenye mechi ambayo iliweka rekodi kubwa baina hizi klabu mbili kubwa hapa Tanzania.”
AUCHO MWANA SANA
Musonda anao marafiki wengi ndani na nje ya kikosi cha Yanga, lakini Khalid Aucho ni mwana sana kwake.
“Rafiki yangu mkubwa ni Khalid Aucho, ingawa naishi vizuri na kila mmoja. Ila mtu ambaye tunaelewana sana ni huyu unajua napenda sana ushirikiano wetu. Huyu mtu ni kaka pia ambaye ukikosea atakuambia hapa umekosea au fanyia kazi hili. Haya yametufanya kuwa pamoja na kuendelea kushirikiana. Tunashinda pamoja tukiangalia filamu na hata kufanya mazoezi.”
Kama straika anapenda kipi akiwa uwanjani?
Musonda anajibu: “Nafasi nayocheza ni wazi. Napenda sana krosi ije kichwani au mguuni, lakini pia nafasi ili niweze kufanya uamuzi wa kufunga. Kwenye soka kuna wakati unatakiwa kujiandaa na mambo yanayoweza kutokea kwa mshtuko ili uyafanye kwenda sawa.”
NI KWELI NUSURA AACHWE?
Wakati Yanga inaanza maandalizi ya msimu huu Musonda alikuwa mmoja wa wachezaji waliochelewa kujiunga na timu, jambo ambalo lilizua uvumi kwamba pengine ataachwa, lakini mwenyewe anafafanua.
“Hapana haikuwa hivyo labda niwaeleze. Kama mtakumbuka ligi ya msimu uliopita ilipokwisha wengine tulikwenda kujiunga na timu za taifa. Kule tulitumia kama wiki mbili na nusu na baada ya majukumu hayo kumalizika niliomba ruhusa ili nipumzike na uongozi ukakubali, ndio maana nilichelewa kurejea nchini,” anasema.
BILA SOKA
Kama isingekuwa soka Musonda angekuwa huyu.
“Nilitamani sana kuwa mhandisi wa mambo ya majengo. Ilikuwa kwenye ndoto yangu kwa miaka mingi, lakini soka ikaniteka na kunileta huku ambako nipo sasa. Ndio maisha yalivyo hakuna namna.
Akizungumzia Kiswahili anasema lugha hiyo upande wake inapanda, lakini changamoto ni hii, wakati wote wa mahojiano haya Musonda alikuwa anaulizwa maswali kwa Kiingereza na anajibu kwa lugha hiyohiyo, lakini akaeleza namna anavyojifunza Kiswahili huku akifunguka baadhi ya wachezaji wenzake wanavyomzingua kwa kumfundisha pia maneno flani ya kitaa.
“Najifunza Kiswahili. Kidogokidogo nazungumza na marafiki, lakini hawa wenzangu kuna muda wananifundisha maneno mabaya. Kuna siku waliniambia ni maneno mazuri, nikaenda kumwambia mtu akaniambia mbona unatukana? Nikashtuka nikaomba radhi, lakini alielewa na kucheka. Sio mbaya naendelea kujifunza.
“Kwa sasa najua, siwezi kutukana tena unajua huyu Farid (Mussa) ni matatizo sana ndio mtu anayeweza kufanya mambo ya namna hii,” anasema Musonda huku akicheka saaanaa.
SIMBA, YANGA FRESHI
Akizungumzia timu hizo, mchezaji huyo anasema: “Napenda sana namna ushindani wa Simba na Yanga ndani ya Tanzania, lakini pia kimataifa. Unajua ubora wao kimataifa ndio kitu bora kinachowavutia makocha na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali. Hii itasaidia kuitangaza zaidi Tanzania.
INONGA, BACCA
Musonda amecheza na wachezaji wengi hapa nchini, lakini upande wa mabeki anawataja beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca na Henock Inonga aliyekuwa Simba. “Tangu nilipofika hapa Tanzania nimekutana na mabeki wengi, lakini beki ambaye alinipa wakati mgumu mwanzoni alikuwa Henock Inonga.
“Alikuwa beki mzuri sana na mshindani, lakini baadaye nilijua namna ya kupambana naye. Mwingine ni beki wangu hapa Yanga, Bacca. Huyu ni beki aliyekamilika sana,” anasema. akizungumzia nafasi ya Yanga kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezaji huyo anasema ipo.
“Kila kitu kinawezekana. Huu ni mchezo wa soka, kitu muhimu hapa tunatakiwa kushinda mechi zetu zilizosalia na kwa sasa inawezekana,” anasema.
“Unajua tumebadilika tumeanza kurudi kwenye ubora wetu baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza na kupata sare mechi moja. Hapa ndani ya timu yetu kila mmoja akili yake ipo huko, tushinde na kwenda robo fainali.”