MTU WA PWANI: Misri, Morocco zimeliumbua soka la Afrika

Muktasari:

  • Kutolewa mapema kwa Misri na Morocco kungeweza kuwa jambo la kushangaza, lakini sidhani kama kuna ambaye aliamini timu hizo zingeweza kufuzu hatua inayofuata ya 16 Bora.

KUNA kipi kipya na cha kushangaza ambacho kinafanywa na timu za Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Russia? Bila shaka hakuna.

Kutolewa mapema kwa Misri na Morocco kungeweza kuwa jambo la kushangaza, lakini sidhani kama kuna ambaye aliamini timu hizo zingeweza kufuzu hatua inayofuata ya 16 Bora.

Pengine timu hizo zingefuzu hatua inayofuata ndio ingekuwa habari ya kushangaza kwa sababu namna zilivyocheza mechi zao za kwanza ilitosha kuonesha kuwa zitacheza mechi mbili zinazofuata kukamilisha ratiba tu.

Pamoja na kujitahidi kucheza vizuri dhidi ya Uruguay, Misri ilipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo kama wangezitumia vizuri chache tu kati ya hizo, wangeweza kufunga mabao ambayo yangewapa ushindi na kuwaweka kwenye nafasi nzuri kuelekea mechi inayofuata.

Kocha mpya wa Azam FC, Hans Pluijm, aliwahi kusema siku moja kuwa timu ambayo haifungi mabao, haiwezi kuwa bingwa. Soka lisingetenda haki kama Misri inayoshindwa kufunga bao angalau hata moja licha ya kutengeneza zaidi ya nafasi 10, ingefuzu hatua ya 16 bora mbele ya Russia na Uruguay ambazo zinafunga mabao kwa kutumia nafasi chache zilizotengeneza.

Kwa bahati mbaya mechi ya pili walikutana na wenyeji ambao walitoka kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Saudi Arabia.

Hii inamaanisha kuwa Misri waliingia uwanjani wakiwa na presha kubwa kuliko wenyeji ambao walikuwa sawa kisaikolojia baada ya kupata ushindi mkubwa kwenye mechi ya kwanza.

Ni kama ilivyotokea kwa Morocco. Walicheza vizuri dhidi ya Iran, wakatengeneza nafasi, lakini wakashindwa kufunga. Mbaya zaidi walifanya uzembe dakika za jioni uliowagharimu na kupoteza mchezo huo.

Haikushangaza kuona wakifungwa na Ureno na kuaga fainali hizo.

Hadithi ilikuwa ile ile ya kucheza vizuri lakini walishindwa kutumia nafasi walizotengeneza.

Soka ni kama kilimo tu. Huwezi kulima matikitiki ukavuna matango.

Timu inayoshindwa kufunga mabao dhidi ya Iran, nini kitakushangaza iwapo ukisikia imepoteza mbele ya Ureno yenye Cristiano Ronaldo au Hispania yenye Sergio Ramos na Andres Iniesta?

Wakati Misri na Morocco zikiaga mapema, wawakilishi wengine wawili, Tunisia na Nigeria wako chumba cha wagonjwa mahututi na wanakaribia kuungana na wenzao kurudi nyumbani.

Kitendo cha kupoteza mechi zao za kwanza kinazifanya kwenda kwenye mechi zinazofuata zikiwa na presha kubwa kama ilivyotokea kwa Morocco na Misri jambo ambalo likawa sababu ya kupoteza mechi hizo na kujikuta zikiaga mashindano hayo.

Kimsingi kuna tatizo sugu na la kudumu kwa Bara la Afrika ambalo linachangia timu zetu kugeuka wasindikizaji kwenye Kombe la Dunia awamu zote na kunaonekana hakuna hatua za dhati zinazochukuliwa kukabiliana nalo.

Wakati mwingine unajiuliza, inakuwaje kwenye ngazi ya klabu? Mbona wachezaji wanafanya vizuri zaidi tena kwa jitihada binafsi?

Pengine unaweza kusema kuwa Mohamed Salah anafunga anasaidiwa na Firmino au Sadio Mane lakini wakati mwingine anafanya yale mambo ya binafsi, lakini inashangaza huku wachezaji wa Afrika hawayaonyeshi kwenye timu za Afrika.

Nina wasiwasi mwingine na hawa wachezaji, wakati mwingine nawaza kuwa inawezekana hawapambani. Wanahofia kuumia na kuja kubakia benchi kwa muda mrefu na kupata changamoto za kupata namba ya kudumu kwenye klabu.

Tatizo hili ama lipo kwenye maandalizi ya timu zetu kabla na wakati wa mashindano hayo ama lipo kwenye namna tunavyopata wawakilishi wa kwenda kushiriki kwenye Kombe la Dunia.

Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa soka la Afrika limekuwa likikabliwa na changamoto nyingi kama rushwa, upangaji matokeo na hujuma kwa timu hasa pale zinapokwenda ugenini, lakini mara kwa mara Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limekuwa likikanusha tuhuma hizi kwa nguvu zote.

Mataifa makubwa yanayofanya vizuri kisoka kama hayo ya Kaskazini mwa Afrika na yale ya Magharibi, ndio yamekuwa yakilalamikiwa mara kwa mara kwa kuwepo na fitina kwa timu ngeni iwe za taifa au za klabu pindi zinapokwenda kucheza mechi za kimashindano, lakini zimekuwa hazifanyiwi kazi na CAF.

Matokeo yake tunapata wawakilishi ambao hawakustahili ambao mwisho wa siku wanakwenda kwenye Kombe la Dunia kushiriki na kujikuta wakidhalilika kwa kutolewa mapema kama hiki tunachokiona kwa sasa.

Kufanya vibaya kwa timu za Afrika kwenye Kombe la Dunia, hakupaswi kuwa jambo la kushangaza wala kushtusha, bali ni matokeo ya mbegu ambayo imepandwa na Bara la Afrika lenyewe.