Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtibwa ilivyoduwaza, vita mpya imeanza Champioship

CHAMPIONSHIP Pict
CHAMPIONSHIP Pict

Muktasari:

  • Wakati ligi hiyo yenye ushindani mkubwa ikitamatika na kila timu kuvuna ilichopanda kutokana na ilichokifanya tangu mwanzo mwa msimu, yapo mambo mengi yaliyojitokeza ambayo huenda unayajua au huyatambui, ila Mwanaspoti linakuelezea kwa kina.

LIGI ya Championship imefikia tamati kwa msimu wa 2024-2025 baada ya kivumbi cha jasho na damu kuvuja kwa wachezaji wa timu 16, zilizokuwa zinapigania nafasi mbalimbali hususani ile ya lengo mama ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Wakati ligi hiyo yenye ushindani mkubwa ikitamatika na kila timu kuvuna ilichopanda kutokana na ilichokifanya tangu mwanzo mwa msimu, yapo mambo mengi yaliyojitokeza ambayo huenda unayajua au huyatambui, ila Mwanaspoti linakuelezea kwa kina.

CHAMP 01

MTIBWA SUGAR YAWEKA REKODI

Mtibwa ilikuwa ni timu ya kwanza msimu huu kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao huku ikiwa na mechi mbili mkononi kutokana na kuonyesha soka safi tangu mwanzo, ikiwa imerejea tena katika hekaheka za michuano hiyo baada ya kushuka msimu uliopita.

Timu hiyo ya Morogoro imekuwa mabingwa baada ya kukusanya pointi 71, ikifuatiwa na Mbeya City ya Mbeya iliyorejea tena baada ya kusoka katika Ligi ya Championship tangu iliposhuka msimu wa 2022-2023, ikimaliza ya pili na pointi zake 68.

Ukiachana na hilo, ila Mtibwa Sugar imeweka rekodi mbili za kibabe na kikosi hicho kimekuwa ni timu ya kwanza katika Ligi ya Championship kumaliza na pointi nyingi, huku ya pili ni kucheza mechi za nyumbani bila kupoteza wala kutoa sare.

Ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kiluvya United Mei 11, 2025, umeifanya timu hiyo kucheza mechi zake 15, kati ya 30 kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro na imeshinda zote ikiwa ni rekodi mpya, huku ikifunga mabao 38 na kuruhusu sita.

Pia, pointi 71 ilizovuna ni rekodi, kwani tangu msimu wa 2021-2022, hakuna timu yoyote iliyofikisha kama hizo na 2021-2022, ilikuwa ni Ihefu iliyomaliza kinara na pointi 66, huku ule wa 2022-2023, JKT Tanzania ilikusanya pointi 63.

CHAMP 02

Msimu uliopita wa 2023-2024, KenGold ya Mbeya iliyoshuka daraja msimu huu ikitoka Ligi Kuu Bara, ilimaliza na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji iliyokuwa na pointi 67, iliyorejea baada ya kusota takribani kwa miaka 23 tangu iliposhuka 2001.


STAND, GEITA VITA INAENDELEA

Wakati timu mbili zilizomaliza nafasi ya kwanza na pili zikipanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja, vita kwa sasa imebaki kwa Stand United iliyomaliza ya tatu na pointi 61 na Geita Gold iliyoshika nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi zake 56.

Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019, katika mechi mbili za msimu huu haijaifunga Geita Gold, kwa sababu ya kwanza kukutana ilichapwa ugenini mabao 3-1, Januari 12, 2025, huku marudiano zilipokutana zilitoka sare ya 1-1, Mei 11, 2025.

CHAMP 03

Timu hizo zitakutana katika mechi ya 'Play-Off' (mtoano) na mechi ya kwanza itapigwa Mei 24 na marudiano ikipigwa Mei 28 na mshindi wa jumla atakutana na atakayepoteza kutoka Ligi Kuu Bara kwa atakayemaliza kwenye nafasi ya 13 na 14.


BIASHARA, COSMO BASI TENA

Biashara United ilikuwa timu ya kwanza kushuka daraja ikiwa na mechi mbili mkononi, baada ya kuburuza mkiani na pointi 16, ikiungana na mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1967, Cosmopolitan iliyomaliza nafasi ya 15, kutokana na kukusanya pointi 20.

Wakati Biashara United na Cosmopolitan zikishuka daraja moja kwa moja kwenda kucheza First League, tayari wageni wapya watakaochukua nafasi hizo wameshapatikana ambao ni Hausung ya Njombe na Gunners ya mkoani Dodoma zilizokata tiketi hiyo.

Hausung ilikuwa timu ya kwanza kupanda kutoka kundi A, ikikusanya pointi 25, baada ya kushinda mechi saba, sare minne na kupoteza mitatu, huku Gunners kutoka kundi B, ikiwa na pointi 35, baada ya kushinda 11, sare miwili na kupoteza mmoja.

CHAMP 04

KAZI IPO HUKU!

Mechi nyingine za mtoano zitakazovuta hisia za mashabiki ni zile zitakazozikutanisha timu zilizomaliza nafasi ya 11, 12, 13 na 14 kusaka tiketi ya kubakia kwa msimu ujao katika ligi hiyo zitakapopambana zenyewe kisha kukutana na za First League.

Kiluvya United iliyomaliza ya 11 na pointi 24, itacheza na Transit Camp iliyoshika nafasi ya 14 na pointi 21, huku kwa upande wa Green Warriors iliyohitimisha msimu nafasi ya 12 na pointi 23, itacheza na African Sports ya 13 na pointi 22.

Timu mbili zitakazoshinda zitabaki katika Ligi ya Championship msimu ujao na nyingine mbili zitakazopoteza zitakuwa na kibarua cha kujitetea, wakati zitakapocheza tena mechi za mtoano na zile za kutoka First League kusaka tiketi ya kubaki.


REKODI YA HAT-TRICK

Msimu huu zimefungwa 'Hat-Trick' sita, akianza mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mechi baina ya timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda kwa mabao 4-0, Desemba 13, 2024.

Andrew Simchimba wa Geita Gold akafunga pia wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akifunga katika ushindi wa 5-0, mbele ya Biashara United, Februari 23, 2025.

Nyota mwingine ni William Thobias wa Mbeya City aliyefunga pia wakati kikosi hicho kilichorejea Ligi Kuu Bara sambamba na Mtibwa Sugar, kilipoichapa Kiluvya United mabao 4-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Machi 17, 2025.

Emmanuel Manyanda wa Stand United akaifungia pia timu hiyo iliyo katika nafasi ya 'Play-Off' ya kusaka kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, wakati kikosi hicho cha 'Chama la Wana', kilipoichapa Green Warriors mabao 5-1, Aprili 20, 2025.

Mchezaji wa mwisho kufunga 'Hat-Trick', alikuwa ni mshambuliaji wa African Sports, Frank Edmund aliyefunga katika mechi ya Mei 11, 2025, wakati kikosi hicho kilipoichapa Transit Camp kwa mabao 3-2, ikiwa ni rekodi tofauti na msimu uliopita.

Msimu uliopita, zilifungwa 'Hat-Trick' tano na nyota wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa alifunga mbili, huku Kika Salum wa Pan Africans FC, Abdulaziz Shahame (TMA FC) na Oscar Mwajanga aliyekuwa Mbeya Kwanza wakifunga moja.

CHAMP 05

UFUNGAJI BORA

Moja ya sehemu pia iliyokuwa na mvuto msimu huu ni katika vita ya ufungaji bora na nyota watatu wamefunga idadi sawa ya mabao 18, ambao ni Andrew Simchimba wa Geita Gold, Raizin Hafidh (Mtibwa Sugar) na Abdulaziz Shahame (TMA FC).

Tangu msimu wa 2017-2018, hakuna wachezaji watatu walioamaliza kwa idadi sawa ya mabao katika Championship, ingawa kwa msimu huu imekuwa ni rekodi mpya kwa nyota hao, hali inayoonyesha wazi ushindani miongoni mwao ulikuwa ni mkubwa zaidi.

Hata hivyo, utata wa bao moja alilonyimwa Andrew Simchimba katika mchezo wa Geita Gold ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Cosmopolitan, Novemba 24, 2024, ikiwa atapewa ataibuka kidedea kwa kufikisha 19 na kuwashinda wenzake wote.

Katika mechi hiyo ndio iliyoleta utata zaidi wa kunyimwa bao na kamishina aliandika kimakosa aliyefunga mabao yote kwa upande wa kikosi cha Geita Gold alikuwa ni Frank Ikobela, japo nyota huyo na Simchimba kila mmoja wao alifunga moja.

Hivi karibuni, Mwanaspoti lilimuuliza Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda kuhusiana na utata wa bao hilo ambapo aliweka wazi wataangalia tena upya ripoti ya mechi iliyoletwa, kisha wakijiridhisha nyota huyo atapewa haki yake.

"Kama ripoti iliyoletwa iliandikwa kimakosa huwa tunairekebisha kwa sababu ni mambo ya kawaida, hatuko tayari kumnyima mtu haki yake, tutaipitia tena upya na ikigundulika tutamuongezea bao lake moja na wala hilo halina tatizo," anasema.

Licha ya kasi na ushindani mkubwa kwa nyota hao, ila wameshindwa kuifikia au kuivunja rekodi ya msimu uliopita wa 2023-2024, ya aliyekuwa mshambuliaji wa KenGold, Edgar William aliyeipandisha Ligi Kuu Bara huku akitupia kambani mabao 21.

Nyota huyo anayeichezea Fountain Gate msimu huu, mabao hayo 21 aliyofunga, yanamfanya kushikilia rekodi ya mshambuliaji aliyefunga mengi zaidi katika Ligi ya Championship, kwani tangu msimu wa 2017-2018, hakuna aliyefunga idadi kama hiyo.


WASIKIE HAWA

Rais wa Bigman FC, Ahmed Waziri Gao, anasema umekuwa msimu bora kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo tangu mwanzoni, huku akijigamba na mafanikio makubwa waliyoyapata na sasa wanajipanga upya kwa ajili ya msimu ujao kuendeleza ushindani.

"Ni kweli hatujapanda Ligi Kuu Bara lakini malengo yetu makubwa yalikuwa ni kubaki kwanza Championship, tunashukuru kwa hilo tumefanikisha, kwa sasa tumeshajua tunapaswa kufanya nini na tunaweka mikakati ya kuongeza ushindani," anasema Gao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar anasema haikuwa rahisi kwa timu hiyo kurejea tena Ligi Kuu Bara, ingawa moja ya jambo kubwa walilofanikiwa kama uongozi ni kuhakikisha wanaendeleza umoja na ushirikiano kikosini humo.

Kwa upande wa Kocha wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi anasema licha ya kufundisha timu mbili msimu huu akianzia na TMA ya Arusha, ambazo zote ameshindwa kuzipandisha Ligi Kuu, ila amejifunza Ligi ya Championship inahitaji nguvu ya kiuchumi.