Msindo aishika Azam, Stars Tshabalala ajipange

Muktasari:
- Beki huyu wa kushoto ni tumaini la timu ya Taifa na Azam FC na ameonyesha ana umuhimu mkubwa katika vikosi hivyo.
SI kwa bahati mbaya kuitwa kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars. Ni kwa sababu ya uwezo wake wa kukaba na kupandisha mashambulizi na amekuwa mmoja wa nyota wanaoibeba Azam FC msimu huu. Huyu ni Pascal Msindo.
Beki huyu wa kushoto ni tumaini la timu ya Taifa na Azam FC na ameonyesha ana umuhimu mkubwa katika vikosi hivyo.
Huenda nyota huyu wa Azam FC akaonekana wa kawaida kwa macho ya wengi na hii ni kutokana tu na utamaduni uliojengeka kwa mashabiki wa soka nchini kuamini wachezaji wa Simba na Yanga ndio bora zaidi na wamekuwa wakiwaimba sana.
Hata pale Azam, wapo wachezaji wanaoimbwa kutokana na ubora wao akiwamo kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na wale wa nafasi ya ushambuliaji, huku wakisahau maeneo mengine ambao kuna nyota muhimu kama beki, viungo na hata makipa.
Mwanaspoti linakuchambulia uwezo na ubora wa nyota huyu ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kilichoweka kambi jijini Tanga, kujiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Morocco utakaopigwa Machi 26.

MORO KIDS HADI KWA MATAJIRI WA JIJI
Msindo alijiunga na kikosi cha wakubwa cha Azam FC mwaka 2022 baada ya kuonyesha kiwango bora katika timu ya vijana ya klabu hiyo ambayo ilimnasa kutokea kituo cha kulea na kuibua vipaji vya soka cha Moro Kids cha Morogoro.

Kipaji chake kiliibuliwa na matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kwenda Morogoro kusaka vipaji na ndipo alipopata nafasi ya kucheza soka la ushindani baada ya kusogezwa Dar es Salaam.
Mbali na Aam FC, Msindo pia amewahi kutumikia kikosi cha timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 na mara kadhaa amekuwa akiitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’.
Kwa sasa ana miaka mitatu ndani ya kikosi hicho kutokana na ubora anaoendelea kuuonyesha matajiri hao hawajaona tabu kumuongeza mkataba ambao unamfanya aendelee kuhudumu kwenye kikosi hicho hadi 2027.
KUKABA, KUSHAMBULIA
Ubora wa sifa ya beki mzuri wa kisasa wa pembeni hasa kushoto ni yule mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia. Awe na kasi na kufika sehemu husika kwa wakati. Hizi ni miongoni mwa sifa alizonazo Msindo ambaye ni mzuri kwa kutumia mguu wa kushoto.

Ndiye beki wa pembeni ambaye amefunga mabo mengi kwa sasa akiingia kambani mara tatu hii ni kutokana na kuwa na uwezo wa kupandisha mashambulizi kwa timu pinzani, kucheza kwa kasi ya hali ya juu mwanzo mwisho kunamfanya kuonekana kuwa ni beki mwenye mapafu ya mbwa.
MBADALA WA TSHABALALA
Msindo ni mbadala sahihi wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa bora kwa miaka 10 katika kikosi cha Simba na Taifa Stars.
Ni wazi mabeki hawa wawili wa kushoto ambao wamemfanya kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Morocco, kutokuwa na wasiwasi endapo mkongwe Tshabalala ambaye amekuwa bora eneo hilo, akikosekana kwa kuamini kuna chaguo lingine sahihi ambalo ni Msindo.

PUMZI, KUJIAMINI
Ubora wa Msindo unafananishwa na wa Tshabalala kutokana na kuwa na pumzi ya kutosha na ni mzuri wa kukaba na kuipandisha timu mbele pamoja na kupiga krosi na kurusha mipira.
Hizi ni sifa zinazoendelea kuwakosha mashabiki mbalimbali wa timu zao, Msindo, Azam na Tshambalala, Simba na zimekuwa zikinufaisha timu zao.

Pia ni wazi kati yao kumeibuka vita mpya ya nafasi kutokana na wote kuwa na uwezo sawa.
Tofauti na wachezaji wengi nchini, Msindo anajiamini sana akiwa uwanjani na hata nje ya uwanja na hakika ameitendea haki jezi yake namba 12 ambayo ameichagua kuivaa.
ALIMKALISHA SIDIBE
Kuonyesha kama habahatishi, beki huyu alimkalisha Cheikh Sidibe ambaye licha ya kupata nafasi mara kwa mara baada ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha, alishindwa kurudi na kuendana na kasi ya Msindo na aliondoka katika timu hiyo na kujiunga na HJK Helsinki ya Finland.

Amekuwa hatetereki kila anapopata nafasi na amekuwa akionyesha ubora wake kuanzia mazoezini. Tofauti na nyota wengine ambao wamekuwa wakilewa sifa na kuishia kupoteza vipaji vyao, kwake kinachombeba ni kazi tu na ndiyo maana imekuwa rahisi kuitwa Stars.
MIFUMO INAMKUBALI
Azam FC inapenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1. Mfumo huu unategemea zaidi viungo na mabeki wa pembeni kupandisha mashambulizi na kuwachezesha washambuliaji.
Hapa ndipo Msindo na Feisal Salum ‘Feitoto’ wanaingia na mashambulizi mengi ya Azam yamekuwa yakianzia kwao na licha ya kutokuwa na fursa nyingi za kulisogelea goli, uwezo wao wa kupiga mashuti ya mbali umekuwa na mchango mkubwa wa kupata mabao huku wakifanya kazi kubwa ya kutengeneza nafasi za mabao wakijaribu pia kuingia eneo la boksi.

Wakati mwingine kocha wa Azam FC amekuwa akitumia mfumo wa 4-4-2 unaopendwa na makocha wengi. Kutokana na sifa ya Msindo ya kupandisha timu, pia imemsaidia kushiriki katika kutengeneza nafasi na pia ana maamuzi mazuri ya mwisho na mtulivu awapo na mpira.
MSINDO TIMU ZA TAIFA
AFCON U-17 = 2019 (Tanzania)
AFCON U-20 = 2021 (Mauritania)
CECAFA U-23 = 2021 (Ethiopia) Wakashinda ubingwa
CHAN = 2021(Cameroon)
KUFUZU AFCON 2025 Morocco (Alikuwepo kwenye kikosi kilichofuzu)
Hivyo amebakiza kucheza Olimpiki na Kombe la Dunia.