Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Modest kaziachia klabu zetu maswali mazito

Muktasari:

  • Modest aliishi kipindi kigumu akiwa kitandani akipatiwa matibabu na ndugu zake kwa upendo, lakini akiwa mbali sana na wadau wa soka waliomfahamu vyema na hata timu alizozitumikia kwa moyo mmoja katika miaka ya 1990 yaani timu zilizokuwa sehemu ya historia yake hazikuwa karibu naye.

JANA ulimwengu wa soka Tanzania ulimpoteza mmoja wa wachezaji wake mahiri wa zamani, Alphonce Modest, beki wa zamani wa Pamba, Simba na Yanga aliyefariki dunia mjini Kigoma baada ya kuugua kwa takribani miaka 15.

Modest aliishi kipindi kigumu akiwa kitandani akipatiwa matibabu na ndugu zake kwa upendo, lakini akiwa mbali sana na wadau wa soka waliomfahamu vyema na hata timu alizozitumikia kwa moyo mmoja katika miaka ya 1990 yaani timu zilizokuwa sehemu ya historia yake hazikuwa karibu naye.

Hali hii ni funzo kubwa kwa klabu kubwa za soka nchini na wadau wake. Huu si utamaduni wa Kiafrika na hasa si Kitanzania. Asili ya utamaduni wetu ni kujuliana hali, kushirikiana katika furaha na huzuni na kufarijiana katika ugonjwa.

Hakuna haja ya kusubiri hadi mauti yatukute ili tuonyeshe upendo ilhali walizitumikia klabu zetu kwa moyo mmoja. Modest alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu na ni wakati huo ilikuwa ni jambo zuri kwa timu na wadau wa soka kuonyesha mshikamano wa kweli.

Tunaziomba Simba na Yanga kama klabu kubwa na timu nyingine zenye historia ya kipekee nchini ziachane na utamaduni huu wa kutojulia hali wachezaji waliowahi kujenga historia ya timu. Bila wachezaji kama Modest, majina na ukubwa zilionao sasa usingekuwapo.


Historia ya timu kubwa za Tanzania haijajitengeneza kwa bahati, bali kwa jitihada za wachezaji waliotumikia timu hizo kwa moyo wakipigania ushindi bila malipo makubwa au kutukuzwa. Ni kutokana na kujisahau timu nyingi za enzi za Simba na Yanga hazipo na historia zao zimeshafutika.

Huu uwe wakati wa mabadiliko. Tunashauri kila klabu kubwa nchini kuwa na kitengo maalumu kwa ajili ya masuala ya wachezaji wa zamani. Kitengo hicho kiangalie namna bora ya kushirikiana na wachezaji walio katika hali ngumu hasa magonjwa kuhakikisha wanapata matibabu na faraja ya kijamii.

Hali ya Modest, ambapo kulikuwa na wakati hata kupata dawa ilikuwa shida haipaswi kujirudia kwa wengine. Hii itakuwa ni ishara dhahiri kwamba wachezaji wa zamani wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa kama sehemu ya historia ya timu na taifa.

Modest alitumikia soka kwa moyo na alizipambania timu na taifa akitumia muda wake mwingi kwa ajili ya kulifanya taifa lifurahi, badala ya kusaka maisha yake kwa kuwekeza katika mambo mengine hata kama ni kilimo.

Ni jukumu la wadau wa soka hasa timu kubwa na zenye heshima kuhakikisha wachezaji kama Modest wanapokea heshima wanayostahili wakiwa hai.

Tumkumbuke Modest si tu kwa maombolezo, bali kuhakikisha wachezaji wengine hawakumbwi na kile kilichomkumba na kukosa msaada wanapokuwa wagonjwa. Hili pia linapaswa kuwa jukumu la serikali hususani kwa wachezaji waliochezea timu za taifa za michezo mbalimbali.