Prime
Mnyama na Pantev walivyochana ‘mkeka’ huku wanatabasamu
SIMBA ilikuwa timu ya kwanza ‘kufuzu’ kwenda makundi miongoni mwa timu nne za Tanzania Bara. Walishamaliza kazi pale Eswatini wiki moja iliyopita baada ya kushinda mabao 0-3 ugenini. Jana waliamua kuchana mikeka ya watu waliokuwa wamecheza kamari.
Katika timu zote za Tanzania Simba ndiyo iliyocheza mechi mbili ndani ya dakika 90. Baada ya kushinda mabao hayo ilikuwa kwamba hakukuwa na namna tena kama Nsingizini ingeweza kufanya maajabu katika uwanja wa Temeke.
Mabao matatu ni mengi hasa unapofungwa nyumbani. Kuna timu huwa zinafanya maajabu kwa kugeuza kibao, lakini mara nyingi zinakuwa zimefungwa ugenini halafu zinaenda kufanya maajabu nyumbani. Ingewezekana vipi Nsingizini kupigwa mabao matatu nyumbani halafu ikafanye maajabu ugenini?
Mechi ilikufa wiki moja iliyopita kule ugenini na Simba walipoteza morali ya kupata matokeo mazuri katika uwanja wa nyumbani. Tunaweza kusema hivyo ingawa bado kuna mambo yanatia shaka kidogo.
Licha ya kwamba timu haikupania sana, lakini uwezo wa mchezaji mmoja mmoja bado unatia shaka. Mfano ni Ellie Mpanzu. Ukosaji wake wa mabao pamoja na uchezaji wake binafsi umekuwa ukiigharimu Simba na hata jana uliigharimu.
Kibu Dennis alikuwa wa moto katika mechi iliyopita na alisaidia kuiua mechi, lakini mechi hii alikuwa anacheza ovyo. Mashuti yake yasingeweza hata kumuua panya anayezurura. Alipaswa kurudia kilekile alichofanya Eswatini.
Lakini eneo la ulinzi la Simba pia lilitia shaka na nusura jamaa wapate mabao mawili kama wangetulia. Kulikosekana umakini na labda nirudie nilichosema hapo juu kwamba matokeo ya ugenini yalipoteza umakini wa mechi.
Ambacho mabosi wa Simba na wachezaji hawakifahamu ni kwamba tayari Simba imepoteza pointi kadhaa katika viwango vya ubora wa CAF kupitia suluhu hiyo. Simba haijashika nafasi ya tano kwa ubora kwa bahati mbaya. Ni mkusanyiko wa pointi nyingi zinazotokana na timu kushinda mechi nyingi za CAF mfululizo na kwa muda mrefu.
Lakini pia ni kufika mbali katika michuano tofauti. Hawakupaswa kupuuzia sana mechi hii. walipaswa kushinda. Lakini pia kwa kuwatendea haki mashabiki ambao walijitokeza uwanjani kutazama mechi hiyo huku wakiwa na asilimia 99 ya kufuzu bado walipaswa kushinda mechi yenyewe.
Mashabiki wachache waliojitokeza katika pambano la jana ni wale waaminifu na wenye mapenzi ya dhati na timu. Kujisumbua kutoka mbali na kufika uwanjani kwa ajili ya pambano ambalo limeshakufa, shabiki anapaswa kuzawadiwa ushindi na timu yake.
Meneja Dimitar Pentev naye alipaswa kuendelea palepale alipoishia wiki iliyopita. Kwamba ingeonekana kila kitu kimebadilika baada ya yeye kukabidhiwa timu. Hata hivyo, mechi ya janai tumeguna na tunasubiri mechi ijayo.
Mwisho wa siku timu zote nne za Bara zimefanikiwa kwenda makundi. Simba, mtani Yanga, Singida Big Stars na Azam. Zote zitakuwa zinapishana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya mechi za makundi. Hii ina maana gani? Tumeendelea kuwaacha mbali majirani zetu. Sisi tumewekeza katika klabu zetu. Matajiri wa hizi klabu wametia pesa na wamekusanya rundo la wachezaji wenye ubora kutoka katika nchi mbalimbali. Wenzetu bado hawajafikia hatua yetu.
Wametuacha wenyewe tukijaribu kupambana na mataifa kutoka Afrika Kaskazini. Majirani zetu kama Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi hawajatia pesa nyingi katika mpira. Kuanzia kuleta wachezaji wengi wa kigeni na makocha bora wa kigeni. Mishahara ya hawa watu ni mikubwa na ndio ambayo inafanya kwa sasa tujitanue katika anga za kimataifa.
Hata rafiki zetu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo siku hizi hawatii pesa siku hizi. Kaka yetu Moise Katumbi alipoamua kuacha kutumbukiza pesa nyingi katika kikosi cha TP Mazembe mpira wa DR Congo umekosa mwakilishi mzuri katika mechi za kimataifa. Wachezaji wazuri wa DR Congo wameamua kuja Tanzania badala ya kubaki kwao. Mchezaji kama Fiston Mayele zamani angecheza TP Mazembe badala ya Yanga. Matokeo yake alipotoka AS Vita ameanza kuzurura katika vikosi vya nje.
Wachezaji wa Zambia zamani TP Mazembe ilikuwa nyumbani kwao, lakini sasa hivi wanacheza Tanzania. Hata Yanga walimchukua Kennedy Musonda baada ya kumuwania na TP Mazembe, lakini Hersi Saidi akawazidi kete Mazembe. Mchezaji kama Clatous Chama zamani angekwenda zake Mazembe kuungana na kina Reinford Kalaba, lakini alikuja zake Simba na mpaka sasa kacheza klabu tatu tofauti za Bara. Usishangae kuona Singida wanalipa vizuri kuliko klabu nyingi za DR Congo.
Hata kocha wao bora kwa sasa yupo Tanzania. Florent Ibenge. Ule mradi wa AS Vita tuliutawanya na leo wanawachukua baadhi ya wachezaji ambao wameonekana kupitwa na wakati katika soka la Tanzania kama vile Yannick Bangala. Kuna wakati TP Mazembe walimchukua Mukoko Tanombe baada ya kusugua benchi Yanga.
Kwa ninavyoona sioni dalili yoyote ya timu za Tanzania kuua miradi yao kwa sasa. Azam wameendelea kutia pesa nyingi kikosini. Wangeweza kumuuza Fei Toto kwa kiasi kikubwa cha pesa kwenda nje, lakini wamekataa.
Yanga nao wamegoma kumuuza Clement Mzize kwa dau kubwa la pesa kwa sababu wanataka kushindana kimataifa. Simba nao wamekuwa katika msimu mwingine mzuri na wametia pesa nyingi katika dirisha kubwa lililopita. Singida inamiliki wachezaji wazuri kama Chama na Khalid Aucho. Hapo hapo kumbuka kwamba wameweza kukaa na kocha kama Manuel Gamondi ambaye ni mtalaamu. Usidhani analipwa pesa kidogo.