MJUAJI: Unaikumbuka Kakakuona?

JANA kulikuwa na ufunguzi wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Wenyeji Ivory Coast walikuwa wakicheza na Guinea Bissau. Najua matokeo unayo.

Katika michuano hiyo ya 34 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957, Tanzania nayo inashiriki kwa mara ya tatu ikipangwa Kundi F na timu za Morocco, Zambia na Congo DR itaaanza mechi zake Januari 17 dhidi ya Morocco.

Tuachane na michuano hiyo ambayo itamalizika Februari 11, leo nimeikumbuka Timu ya Taifa ya Tanzania iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji ikiwa na wachezaji wengi wasiokuwa na majina makubwa katika soka la Tanzania.

Sio wengi wanaoikumbuka timu hii iliyoitwa Kakakuona. Nakumbuka kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars Mdenish Kim Poulsen naye aliwahi kuunda timu ya taifa ya Vijana ikiitwa Future Taifa Stars mbali na Taifa Star ambayo iliwapa uzoefu wachezaji wengi.


TURUDI KWA KAKAKUONA

Mwaka 1992 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Chalenji na kuwakilishwa na timu mbili. Timu kubwa iliitwa Victoria iliyoundwa na wachezaji wazoefu na waliotisha enzi hizo na ilipangwa kituo cha Mwanza na ile ya kikosi cha pili iliitwa Kakakuona kilipelekwa Arusha kikiwa na wachezaji wengi vijana lakini wenye vipaji kwelikweli.


ILIANZIA ARUSHA

Kakakuona ilianzia mechi ikiwa kundi moja na Uganda, Kenya na Shelisheli (Seychelles) ikijulikana kwa jina lingine kama Tanzania B.

Kundi A lilicheza mechi zake Mwanza ambapo liliongozwa na timu nyingine ya Tanzania ikiitwa Tanzania A au Victoria. Kundi hili A pia lilikuwa na timu za Malawi, Ethiopia, Zambia na Zanzibar.


MOGELLA, GAGA WAIKATAA

Katika hatua ambayo haikutarajiwa na wengi, wachezaji mahiri wakati huo, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ na Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’ walikataa kujiunga na timu hiyo iliyonekana kuwa na wachezaji wengi chipukizi.

Mogella na Gaga waliikataa Kakakuona iliyokuwa ikifundishwa na makocha wazawa, Sunday Kayuni na Charles Boniface Mkwasa kwa kuwa walitamani kuchaguliwa katika kikosi cha timu ya wakubwa iliyokuwa na wachezaji wengi maarufu.


KAKAKUONA YAPASUA

Katika hali isiyotarajiwa na wengi, kikosi cha Kakakuona  ambacho kilikuwa chini ya nahodha, Sekilojo Chambua kilifanya vizuri tofauti na Victoria iliyokuwa na mastaa wengi.

Ilianza mechi Novemba 16, 1992 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta dhidi ya Seychelles na kuifumua kwa mabao 3-0. Mabao ya Razak Yusuf ‘Carecca’ katika dakika ya 24 na Christopher Michael dakika ya 33. Bao la tatu lilikuwa la kujifunga la Gonzalez dakika ya 89.

Katika mchezo wa Novemba 19, Kakakuona iliivimbia Timu ya Takifa ya Uganda, The Cranes kwa kutoka nayo sare ya bao 1-1.

Bao la Kakakuona likifungwa na Careca dakika 48 likiwa la kuchomoa lile la Sam Ssimbwa la dakika la 13. Novemba 22, Kakakuona  ilitoka sare tasa na Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars.


VICTORIA ILIKUWAJE?

Novemba 16 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Malawi. Bao la kusawazisha la Victoria lilifungwa kwa penalti na Fumo Felician dakika ya 71. Bao la Malawi likifungwa na Young Chimodzi dakika ya 69.

Novemba 18, Victoria ilikubali kichapo cha  bao 1-0 kutoka kwa Zanzibar Heroes bao la Issa Raadhili Lambo katika dakika 48.

Novemba 20, timu hiyo ilijitutumua na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ethiopia. Ni kutokana na mabao ya Said Mwamba dakika 4 na Fumo dakika 43. Bao la Ethiopia lilifungwa na Asnaka dakika 56.

Siku moja baadaye, Victoria ilicheza dhidi ya Zambia na kukubali kichapo cha mabao 2-1. Bao la mapema la dakika ya 4 la Jones Lunyamila yalijibiwa na mabao mawili ya Kelvin Mutale ya dakika 33 na 56.


NUSU FAINALI YA KIBABE

Victoria iliishia hapo. Katika kundi lake Zambia na Malawi zilifuzu nusu fainali na huku Kundi B, Kakakuona na Uganda zikifuzu kucheza nusu fainali.

Novemba 25, Kakakuona ikacheza dhidi ya Malawi na kushinda mchezo huo kwa bao 1-0 lilifungwa na Chambua katika dakika ya 60 na kuifuata The Cranes iliyokuwa imetangulia fainali baada ya kuifunga Zambia kwa penalti 4-2 baada ya sare tasa.

Fainali zikacheza timu zilizokuwa Kundi B, Uganda na Tanzania B au Kakakuona.

Fainali ilipigwa Novemba 28, jijini Mwanza na Kakakuona ilifungwa kwa tabu sana bao 1-0 lilipachikwa wavuni na Issa Seketawa dakika ya 77. Uganda ikanyakua ubingwa.


WALIOUNDA KAKAKUONA

 Joseph Katuba, Sahau Said Kambi na Bure Mtwagwa. Wengine ni Kaunda Mwakitope, Mohammed Mtono, Salumu Kabunda ‘Ninja’, Gasper Lupindo na Mustapha Hozza. Wengine ni James Charles, Christopher Michael, Jumanne Challe na Omary Said. Pia,  kina Thomas Kipese,  Justine Mtekele, Sekilojo Chambua, Jimmy Mored, Mbuyi Yondani, Said John, Razak Yusuf na Celestine ‘Sikinde’ Mbunga.bunga.