MJUAJI: Tanzania ilifuzu Afcon ya nchi nane 1980

MICHUANO ya ya kuwania ubingwa wa Afrika (AFCON) inatarajiwa kufungua pazia Januari 13 (zimebaki siku sita tu) ambayo tamati yake itakuwa Februari 11, 2024. Habari kubwa ni kufuzu kwa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwenye michuano hiyo ambayo safari hii itafanyika Ivory Coast. Ikumbukwe hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Stars kufuzu michuano hiyo.

Mwaka 1980, Taifa Stars ilikuwa kati ya timu nane zilizofuzu AFCON ikiwa sambamba na Algeria, Misri na waliokuwa mabingwa watetezi, Ghana na timu nyingine zikiwa ni Ivory Coast, Morocco na wenyeji Nigeria.


ILIANZA RAUNDI YA KWANZA

Katika kutafuta nafasi, Stars haikuanza katika hatua ya awali bali ilianza raundi ya kwanza kwa kucheza na Maurituas Aprili 16, 1979 katika Uwanja wa George V, Maurituas na kufungwa mabao 3-2.

Katika mechi ya marudiano Aprili 29, katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam, Swaziland ilifungwa mabao 4-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 6-3.


MECHI NGUMU

Raundi ya pili, Stars ilikutana na Zambia, Agosti 11, 1979 katika Uwanja wa Taifa na timu hiyo kuondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 lilifungwa na Mohammed Rishard ‘Adolf’.

Mchezo wa marudiano ulipigwa Zambia Agosti 27 katika mji wa Ndola na kuisha kwa sare ya bao 1-1.

Zambia ilitangulia kwa bao la Alex Chola dakika 43 na Tanzania ilisawazisha dakika ya 84 bao lilifungwa na Augustine Peter maarufu kama ‘Peter Tino’.


TINO ANATUPELEKA LAGOS

Mtangazaji maarufu wa Redio Tanzania (RTD) wakati huo, Ahmed Jongo alitangaza mchezo huo kutoka Ndola na baada ya bao hilo alipiga kelele huku akirudia mara kwa mara  akisema Peter Tino anatupeleka Lagos. Msemo huo ulikuwa maarufu sana wakati huo.

Katika kundi lake Tanzania ilipangwa na nchi za Nigeria, Misri na Ivory Coast.


MKAMBI NA BAO LA KWANZA AFCON

Machi 8, 1980, katika Uwanja wa Sululele, Lagos Tanzania ilikubali kichapo cha mabao 3-1 na wenyeji, Nigeria na bao lake likifungwa na kiungo, Juma Mkambi.

Mkambi ambaye kwa sasa ni marehemu ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika michuano hiyo katika dakika 54.

Machi 12, Stars ilirudi Sululele dhidi ya Misri na kukubali kichapo cha mabao 2-1. Bao la Stars likifungwa na Thuen Ali dakika 86.

Machi 15, Stars ilishuka Sululele dhidi ya Ivory Coast na kutoka sare ya 1-1 bao la Stars likifungwa tena na Thuen Ali katika dakika 59.

Katika michuano hiyo ilibainika kwamba Stars ilikuwa inakuwa vizuri zaidi katika kipindi cha pili ambapo ndipo ilipofunga mabao yake matatu.

Timu ilipourudi ilipokewa na baadhi ya viongozi na kufanyiwa sherehe katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga jijini Dar es Salaam na kuvishwa mashada ya maua na stori ikaishia hapo.


KIKOSI KILICHOENDA

Makipa walikuwa ni Athuman Mambosasa, Juma Pondamali ‘Mensah’ na Idd Pazi ‘Father’

Mabeki: Leopard Tasso Mukebezi, Mohamed Kajole ‘Machela’, Daud Salum ‘Bruce Lee’ Ahmed Amasha ‘Mathematics’, Leodigar Chilla Tenga Jellah Mtagwa, Rashid Idd ‘Chama’ na Salim Amir

Viungo, Juma Mkambi ‘Jenerali’, Hussein Ngulungu, Mohamed Rishard ‘Adolf’, Willy Kiango na Mtemi Ramadhani.

Washambuliaji: Omary Hussein ‘Keegan’, Augustino Peter ‘Tino’, Thuwen Ali na Mohamed Salim


AFCON YA PILI 2019

Baada ya miaka 39, tangu Stars ilipofuzu kwa mara ya mwisho Afcon ilifanya hivyo tena mwaka 2019.  Kundi la Tanzania liliundwa na nchi za Uganda, Lesotho, na Cape Verde.

Stars ilianza kinyonge kwa kutoa suluhu na Lesotho, Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Septemba 8, ikaenda kutoa sare tasa na Uganda ugenini na Oktoba 12, katika Uwanja wa Cabo Verde ikakubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Cape Verde.

Oktoba 16, Stars ilipata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Cape Verde baada ya kushinda 2-0. Na Novemba 18, 2018 Stars ilipoteza 1-0 kwenye Uwanja wa Setsoto jijini Maseru. Ushindi uliyoipeleka Misri kwenye fainali za Afcon ni wa 3-0 wa Machi 24 dhidi ya Uganda jijini Dar es Salaam.


HATA POINTI MOJA!

Katika fainali hizo za mwaka 2019 zilizofanyika Misri, Stars haikutoka hata na pointi tofauti na mwaka 1980 katika Kundi C, ilipopata moja. Ikiwa Kundi moja na Senegal, Algeria na Kenya ilipoteza michezo yote.

Juni 23, ilichapwa na Senegal 2-0. Juni 27 ikachapwa na Kenya 3-2 na kuhitimisha Julai Mosi na kuchapwa 3-0 na walioenda kuwa mabingwa, Algeria.

Safari hii kikosi hicho kiliambulia mabao mawili tu yaliyofungwa na Simon Msuva na Mbwana Samatta dhidi ya Kenya


KIKOSI KILICHOENDA MISRI

Aishi Manula, Metacha Mnata na Aron Kalambo. Hassan Ramadhani, Gadiel Michael, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Himid Mao ‘Ninja’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Yahya Zayd na Aggrey Morris.

Wengine ni  Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Ally Mtoni, John Bocco ‘Adebayor’, Thomas Ulimwengu, Farid Mussa, Saimon Msuva, Mbwana Samatta ‘Popat’, Rashid Mandawa, Abdillahie Mussa, Vincent Philipo na Erasto Nyoni. Stars itafanya nini Ivory Coast? Tusubiri.