MJUAJI: Tanga Derby mpira ulipasuka Mkwakwani

KUNA historia zimetokea Tanzania lakini kwa bahati mbaya wengi hawazikumbuki.

Lipo tukio hili lililotokea Julai 23, 1988 katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga katika mchezo wa Tanga Derby uliozikutanisha timu mbili zenye upinzani mkali za Coastal Union na African Sports.


ULIKUWA MWAKA

WA TANGA

Kumbukumbu zinaonyesha mwaka huo ulikuwa mtamu zaidi kwa timu za Tanga, baada ya ‘Wagosi wa Kaya’ kubeba ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na ‘Wana Kimanumanu’ kutwaa ubingwa wa Ligi ya Muungano (kwa sasa haipo tena).

Ligi ya Muungano ilikuwa ikihusisha timu tatu za Tanzania Bara na nyingine za Zanzibar na kushindania ubingwa wa Tanzania kukata tiketi ya michuano ya Klabu Bingwa (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).

Coastal ilibeba ubingwa wa Bara na Sports ilishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na kuiwezesha kushiriki Ligi ya Muungano.

Sports ilipokuwa bingwa wa Muungano, Coastal ilishika nafasi ya pili na timu hizo za Tanga zikapata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa (Klabu Bingwa na Kombe la Washindi wakati huo), huku Wagosi pia wakikata tiketi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup).


LIGI YENYE MSISIMKO

Tofauti na sasa kwenye Ligi Kuu Bara, zamani kulikuwa na msisimko wa hali ya juu, kiasi ilikuwa ngumu kutabiri timu gani ingeweza kubeba ubingwa. Hadi katika michezo ya mwisho ndipo bingwa alipofahamika.

Hadi Coastal inanyakuwa ubingwa kulikuwa na ushindani mkali sana katika nafasi za juu kwa timu za Coastal, Yanga na Sports kwa kutofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.


ZAPIGWA NA WATANI WAO

Timu zote hizo zilikuwa na pointi 26, lakini Coastal ilikuwa imefunga mabao 27, Yanga (24) na Sports (23).

Kabla ya mechi za mwisho za siku Coastal na Yanga zilikuwa juu kwenye msimamo, lakini zote zikapoteza mechi zao kwa kufungwa na wapinzani wao.

Coastal ilikubali kichapo cha mabao 2-0 na Sports na Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 na Simba. Katika mchezo huu kama Yanga ingeshinda ingekuwa bingwa na Simba ingeshuka daraja.


KIBUYU CHA MKWAKWANI

Ilikuwa ni Jumamosi wakati wapinzani hao wa Barabara ya 11 na 12 jijini Tanga ilipochuana kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Hii ndio siku ambayo Coastal ilitwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza na ya mwisho licha ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wana Kimanumanu.

Katika mchezo huu, Sports iliwashangaza watazamaji kwa kuvaa jezi za njano tofauti na rangi za jezi zake zilizozoeleka nyeupe na bluu.


COASTAL WANUNA, WACHEKA

Licha ya siku hii kubaki kwenye kumbukumbu kubwa kwa Wagosi wa Kaya kwa kuchukua ubingwa, lakini ndio siku kila wanapoikumbuka wakiwa wanacheka huku wakinuna. Walicheka kutokana na kutwaa ubingwa na walinuna kwa kufungwa na wapinzani wao.


TUKIO LA KUPASUKA MPIRA

Tukio la kupasuka mpira ukiwa hewani, mpira ulipasuka hewani baada ya shuti kali la nahodha wa Coastal, Yassin Napili, shuti ambalo lilionekana lingeweza kuzaa bao.

Hakuna mchezaji aliyekuwa anamkaba Napili wakati akipiga shuti hilo, wengi waliamini ingeweza kuwa bao kama mpira huo ungefika langoni ukiwa na nguvu zake kwani baada ya kupasuka ukiwa angani ulidondoka chini na kipa wa Sports, Salim Waziri  ambaye aliuokota ukiwa hauna upepo.

Ilikuwa ni katika dakika ya 25 mpira huo ulipopasuka bila kutarajiwa, wakati huo hakukua na timu iliyokuwa imepata bao. Awaku beki wa pembeni wa Coastal, Douglas Muhani aliambaa na mpira upande wa kushoto akamwekea Napili aliyekuwa amepanda, akiwa katika nafasi nzuri kisha  akajiandaa na kupiga shuti kali kwa kipa Salim Waziri kabla mpira huo kufika langoni kwa African Sports ghafla kishindo kikubwa kikasikika uwanjani na kuwashangaza watazamaji.

Kutahamaki mpira ulikuwa umepasuka, hakuna aliyeweza kulieleza tukio hilo kwa ufasaha, ilibidi uletwe mpira mwingine.


SPORTS YAJIPIGIA COASTAL

Sports ilielemewa sana kwenye kipindi cha kwanza lakini ilirudi tofauti katika kupindi cha pili na kufunga mabao mawili yaliofungwa na Juma Burhan ‘Kakoko’ dakika ya 71 akiunganisha kwa shuti kali la krosi iliyopigwa Abbas Mchemba.

Bao la pili lilifungwa dakika 87 na mfungaji bora wa mwaka huo mshambuliaji, Victor Kefa Mkanwa ambaye alimzidi mbio beki Abdallah Tamimu ‘Mdaula’.

Baada ya bao hilo hali ndani ya Uwanja wa mkwakwani ilikuwa ni vurugu tupu kwani muda huo huo kwenye Uwanja wa Taifa simba nayo ilipata bao la pili (kupitia matangazo ya moja kwa moja ya Redio Tanzania).

Habari hiyo iliwapa nguvu mpya mashabiki wa Coastal waliokuwa tayari wameanza kununa na kupata nguvu mpya zilizo wawezesha kuimba ‘Bingwa… bingwa, bingwa…”


VIKOSI VILIVYOCHEZA

Coastal: Mohamed Mwameja, Said Kolongo, Douglas Muhani, Abdallah Tamimu ‘Mdaula’, Yasin Abuu Napili, Ally Maumba ‘White Horse’, Idrisa Ngulungu, Kassa Mussa, Juma Mgunda, Hussein Mwakuluzo na Razak Yusufu ‘Careca’ chini ya Kocha Zakaria Kinanda ‘Arrigo Sacchi’

 Sports: Salim Waziri, Fransis Mandoza, Bakari Tutu, Hassan Banda, Mhando Mdeve, Raphael John, Juma Burhan ‘Kakoko’,  Abbas Mchemba, Victor Mkanwa, Mchunga Bakari ‘Mandela’ na Said Seif. Kikosi hiki kilikuwa chini ya Kocha Syllersaid Mziray ‘Super Coach’.

Wiki ijayo tunaweza kubaki tena Tanga kwa kisa cha Abdallah Luo.