MJUAJI: Omar Hussein alizitikisa Yanga, Pan

HIKI ni kipindi cha usajili wa dirisha dogo. Timu  zinatumia dirisha hili kufanya marekebisho ya usaji zilizoufanya wakati wa dirisha kubwa.

Katika usajili kuna mambo mengi sana ya nyuma ya pazia huwa yanatokea. Mara nyingi usajili unatokana na ushawishi wa mambo ya fedha.

Mwaka 1976, winga machachari wa Mseto ya Morogoro, Omar Hussein ‘Keegan’ alizua taharuki kubwa ya usajili katika timu mbili kubwa zilizokuwa na upinzani.

Ni timu za Young African (Yanga) na Pan African. Ikumbukwe Pan ilitoka ubavuni mwa Yanga baada ya kuibuka mgorogoro wa muda mrefu.


NENDA RUDI ZA PAN, YANGA

Awali, Omar Hussein alionekana kujiunga na Yanga, lakini bila ya kutarajiwa  akaonekana katika michezo ya kirafiki akiwa na jezi ya Pan African. Hapo aliichezea Pan michezo minne ya kirafiki.

Wiki moja baadaye alionekana tena katika mchezo wa kirafiki akiwa na amevaa jezi ya Yanga akitumikia timu hiyo dhidi ya Mzalendo ya Tanga.


ALILAZIMISHA YANGA

Wakati huo winga huyo machachari alikuwa na umri wa miaka 19,  akiitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania na alikuwa akitoka kuipa ubingwa wa Ligi  ya Taifa (sasa Ligi Kuu) timu yake ya Mseto ya Morogoro mwaka 1975 alikuwa kama mtu aliyekosa msimamo kwa kiasi fulani.

Unaweza kusema  baadhi ya viongozi wa timu za Pan na Yanga kutokana na umri wake walikuwa wakimpa vishawishi. Baadaya kurudi Pan, Omar Hussein mbele ya mkutano wa waandishi wa habari na baadhi ya viongozi na wachezaji wa Pan African, nyota huyo alibainisha hakuwa na dhamira ya kuitumikia Yanga.


ALIFUNGIWA CHUMBANI

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Pan African, Athuman Titi Mohamed alizungumzia suala la mchezaji huyo  kujiunga na Pan, alisema yeye na wenzake wawili walikwenda Morogoro kumfuata mchezaji huyo lakini baadaye aliibukia Yanga wakati wao wakiwa wameshaingia naye makubaliano.

Titi alizungumza kwa niaba ya Omar Hussein alisema mchezaji huyo alitoroshwa na kaka yake, Shaban na viongozi wa Yanga na kumlazimisha kuichezea Yanga.

Alidai mchezaji huyo alifungiwa chumbani na kulazimishwa kucheza mchezo dhidi ya Mzalendo ya Tanga.


USIA WA BABA ASIICHEZEE YANGA

Titi alisema mama yake Omar Hussein alikumbwa na fadhaa baada ya kusikia mwanawe alikuwa amejiunga na Yanga na sio Pan African.

Kiongozi huyo alidai mama wa mchezaji huyo alikuwa akikumbuka usia uliochwa na mumewe (baba yake Omary Hussein) kwamba isitokee mwanawe yeyote akajiunga na Yanga.

Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa kwa mara nyingine tena, Desemba 22, 1976 Omary Hussein alijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kutangaza kurudi kuitumikia Yanga.


AKANA MADAI YA TITI

Mchezaji huyo akiwa ameambatana na mmoja kati ya ndugu zake, Maulid Ramadhani, alisema ataitumikia Yanga na si timu  nyingine yoyote.

Mbele ya wana habari, alikanusha madai yote yaliyotolewa na Mjumbe wa Pan, Titi kwamba alikuwa akizungumza kwa niaba yake. Pia, alikanusha kuwepo kwa usia wa baba yake uliomkataza kuitumia Yanga.

“Sio kweli, sikumtuma mjumbe yule kuzungumza kwa niaba yangu. Kuanzia leo naomba nitambulike kama mchezaji wa Yanga na sijaachiwa usia mbaya na baba kuhusu timu hii,” alisema Omar Hussein na kuhitimisha msuguano kuhusu jambo hilo. 

Mchezaji huyo alidumu ya Yanga kwa takribani miaka 12 na alipata mafanikio makubwa sana.

Winga huyo akiwa mmoja kati ya wachezaji wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki kwa mara ya kwanza Afcon mwaka 1980 kule Nigeria, akiwa na Yanga aliitesa sana Simba.

Hussein ambaye alifananishwa na mchezaji wa zamani wa England, Kevin Keegan aliiifunga Simba jumla ya mabao sita katika michezo tofauti, akiwa ndiye mchezaji kinara wa kufunga mabao kwenye Kariakoo Derby ya Ligi Kuu akifuatiwa na Dua Said aliyetamba na Simba.

Mwaka 1989 alijiunga na Simba na kuvaana na Yanga katika fainali ya Kombe la AICC iliyochezwa jijini Arusha mwaka huo na timu yake mpya kupasuka kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Joseph Machella.

Hata hivyo, Keegan aliitumikia Simba kwa muda mchache kabla ya kutimkia Majimaji ya Songea na baadaye alikwenda Uarabuni kusaka maisha mema ya soka na baadaye kugeukia ukocha akifundisha timu mbalimbali ikiwamo Katavi Rangers.