MJUAJI: Maajabu ya Simba Afrika mwaka 1974

SIO watu wengi wanaojua hili. Lakini kulikuwa na maajabu fulani hivi hadi Simba ilipofika nusu fainali ya Klabu Bingwa wa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) mwaka 1974.

Hadi chama hilo la Msimbazi linatinga hatua hiyo ambayo ni historia kwa timu za Tanzania mabao yake mengi ya ugenini yalifungwa na Adam Sabu ‘Gerd Muller’ na Abdallah ‘King’ Kibadeni.

Kitu cha ajabu, wachezaji hao hawakuhusika kabisa na mabao ya nyumbani, wao walifunga ugenini tu na kuifikisha Simba nusu fainali.


ADAMU SABU KIBOKO

Hata hivyo, ni mshambuliaji Adamu Sabu ndiye aliyeweka historia zaidi ya mwenzake Kibadeni King’ kwa kufunga mabao mengi zaidi ya ugenini.

Katika mchezo dhidi ya Linare ya Lesotho ukipigwa ugenini, Simba ilitoka nyuma na kushinda 3-1 kwa mabao ya Sabu, Haidar Abeid na Abbas Dilunga ‘Sungura’.

Katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam, Simba ilishinda 2-1 na mabao yake yakifungwa na Kessy Manangu na Saad Ally.

Katika hatua iliyofuata, Simba ugenini ilishinda dhidi ya Zambia Army (Green Buffaloes) kwa mabao 2-1.

Mabao ya Simba yalipachikwa na Sabu na Abdallah Kibadeni na kitu cha ajabu katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam, Simba ilishinda 1-0, marehemu Abbas Dilunga.


SABU NA KIBADENI TENA

Baada ya ushindi huo, Simba ilfuzu kwa robo fainali na kucheza dhidi ya Accra Hearts of Oak ya Ghana, Simba ilishinda ugenini 2-1 ni Sabu na Kibadeni tena walipachika mabao ya Mnyama na katika mchezo wa marudiano hapa ukaisha kwa sare tasa 0-0.


SABU, KIBADENI WAKWAMA

Simba ikatinga hatua ya nusu fainali na kuwa timu pekee ya Tanzania iliyofikia hatua hiyo hadi sasa.

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mahalla el Kubra ya Misri, nyumbani Simba ilishinda 1-0 kwa bao la Saad Ally la dakika ya mwisho la kona ya Kibadeni.

Lakini ugenini kushindwa kufunga kwa Sabu na Kibadeni kukaifanya Simba kufungwa 1-0 hata baada ya dakika 30 za nyongeza 0-0.


VITUKO VYA WAARABU

Katika mchezo huo, Simba ilifanyiwa kila aina ya hila na Waarabu hao hasa kipa Athuman Mambosasa, alifanyiwa vituko vingi sana kwa sababu alikuwa kikwazo kwa wapinzani kupata ushindi mnono.Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 3-0, inadaiwa wachezaji Kibaden, Mohammed Kajole na Sabu walipiga nje penalti kwa makusudi ili kulinda usalama wao ambapo kama wangeshinda mchezo huo wasingeweza kutoka salama uwanjani.

Achana na rekodi hiyo ya nusu fainali ya Klabu Bingwa ambayo haijawahi kufikiwa na timu yoyote ya Tanzania, ikiwamo Simba yenyewe licha ya ushiriki kwa misimu zaidi ya miaka 50, Wekundu hao walikuja kuishangaza Afrika mwaka 1993! .


Usikose Jumapili ijayo kwenye gazeti la Mwanaspoti!