MJUAJI: Kibadeni avamiwa na vibaka ufukweni

KOCHA wa Simba, Abdallah Kibadeni

WIKI iliyopita tulianza kumwangazia staa wa zamani Simba na Taifa Stars, Abdallah Seif ‘Kibadeni’ au King Mputa. Tuliona jinsi staa huyo alivyoponea chuchupu kutua Jangwani na baadaye akatua Msimbazi. Pia, tuliona jinsi jina la Kibadeni lilivyopatikana na alivyoweka rekodi ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ dhidi ya Yanga katika mchezo wa ligi ya Tanzania mwaka 1977 ...SASA ENDELA…


ILIKUWA ni Jumanne, Aprili 10, 1973, staa wa Simba Sports Club na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Abdallah Athuman Seif ‘Kibadeni’ alipovamiwa na majambazi na kujeruhiwa.

Kibadeni au King alipatwa na dhahama hiyo saa nne usiku alipokuwa maeneo ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Kutokana na matatizo hayo, staa huyo mfupi na mwenye umbile dogo alilazwa katika Hospitali ya Muhimbili (sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili) wadi ya Kibasila namba 13.


VIBAKA WATOKEA VICHAKANI

Taarifa zilizopatikana wakati mchezaji huyo alipokuwa akitibiwa hospitalini hapo zilisema alishambuliwa ghafla na vijana wawili wakati alipokuwa akitaka kuingia ndani ya gari lake baada ya kununua madafu.

Ilidaiwa vibaka au majambazi (kama walivyoitwa kipindi hicho) walitokea vichakani na kumlazimisha King kusimama huku wakiwa na lengo la kumdhuru.

Mchezaji huyo alipoona ni watu hatari alikimbia na vibaka wale wakaanza kumkimbiza lakini kwa bahati mbaya, staa huyo wa Simba alianguka na hapo akakatwa panga katika mkono wake wa kushoto.

Kitendo hicho kilimfanya Kibadeni kuwa na alama katika mkono huo hadi leo hii.

Hata hivyo, Kibadeni alijitahidi na kufanikiwa kuwakimbia vibaka wale hadi akakifikia kikundi cha Wahindi waliokuwa wakipunga upepo katika ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Mmoja kati ya Wahindi wale alimchukua Kibadeni na kumpakiza ndani ya gari lake hadi Hospitali ya Aga Khan kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.

Taarifa kutoka kwa msemaji wa Hospitali ya Muhimbili, ilithibitisha kupokewa kwa mchezaji huyo na kusema kwamba alikuwa akiendelea vizuri.


KAMBI YA STARS

Taarifa nyingine za tukio hilo zilizotolewa na Kibadeni mwenyewe zilisema, alikuwa katika Hotel ya Holiday Inn iliyopo maeneo ya Posta na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilikuwa imeweka kambi hapo.

Inadawa siku hiyo kulikuwa na tuzo na Kibadeni alitoka muda wa jioni hadi ufukweni na akanunua soda na dafu akiwa ameshika mkononi, wakati akiwa anaenda kwenye gari lake aliwaona vijana wawili wakiwa wameziba nyuso zao na vitambaa.

Hapo ndipo kadhia hiyo ilipotokea.

Kibadeni alikaririwa akisema: “Walikuja kwa ajili ya kunidhuru. Wakati nataka kujikinga nikawapiga na chupa ya soda walikwepa, wakatoa panga na kunikata kidole, hawakuchukua kitu chochote,” alisema na kuendelea:

“Nilipoanguka wakaja Wahindi kunisaidia kunipeleka mpaka Hospitali ya Ocean Road, ikashindikana kunitibia nikapelekwa Muhimbili, zoezi la tuzo kwangu ikawa ndio basi tena, mpaka leo sikujua kwa nini nilifanyiwa hivyo.”


MABEKI WAKALI

Katika historia yake ya kusakata kabumbu, Kibadeni alikuwa akiwahofia sana mabeki wawili wa Yanga, Juma Shabani na Boi Wickens.

Pindi alipokuwa akikutana na mabeki hao kazi ilikuwa inakuwa ngumu sana kiasi cha kumfanya kulala na viatu.

Katika kikosi chake, Kibadeni alikuwa anawakubali sana wakongwe wenzake ambao ni makipa Athumani Mambosasa (Omary Mahadhi), Shaban Baraza (Daud Salumu), Mohammed Kajole (Hamis Askari), Mohammed Bakari ‘Tall’na Aloo Mwitu.

Athuman Juma (Khalid Abeid), Willy Mwaijibe, Khaidary Abedi, Adam Subu, King Kibaden (Seif Manangu) na Abas Dilunga (Martin Kikwa).

Je, unataka kujua zaidi kuhusu Kibadeni? usikose Jumapili ijayo.