MJUAJI: Bakhresa alijenga jengo la Pan Africa

SIO watu wengi wanaolifahamu hili. Mfanyabiashara mkubwa nchini, Said Salim Bakhresa aliwahi kutoa (na bado anatoa) mchango mkubwa sana katika soka la Tanzania.

Achana na taarifa za kuwahi kuwa mweka hazina wa klabu ya Simba miaka ya 1980. Achana na habari za kuanzisha Azam FC na kuweka uwekezaji wa nguvu katika soka la Tanzania.

Tajiri huyu ambaye ni nadra sana kuonekana hadharani ndiye aliyejenga ghorofa moja (floor) ya jengo la Klabu ya Pan Africans pale Mtaa wa Swahili na Kariakoo, Dar es Salaam.


WAZUIWA KUANZISHA PAN

Mwaka 1976, baada ya mgogoro wa muda mrefu, Katibu Mkuu wa Yanga, Mohammed Missanga alitangaza kuwafukiza wachezaji 21 wa Yanga.

Wachezaji wote waliotimuliwa na Yanga walienda kujiunga na Nyota Afrika ya Morogoro ambayo ilikuwa na uswahiba na Yanga.

Ni wachezaji wachache tena waliokuwa chipukizi kina Juma Nassor Pondamali ‘Mensah’, Mohamed Rishard ‘Adolf’, Mohammed Yahya ‘Tostao’ na Gordian Mapango ambao walijiunga na Breweries ya Dar es Salaam.

Na baada ya timu kurudi Dar es Salaam na kupata usajili wa Pan Afrika baada ya kuungana na timu ya Zama za Kale wachezaji hao walirudi kundini na kutafutiwa kazi Bohari ya Dawa.

Ikumbukwe Februari 1976, Waziri wa Utamaduni wa Taifa, Mrisho Sarakikya alipiga marufuku kuanzishwa kwa klabu mpya.

Hii ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwazuia viongozi waliotoka Yanga kufanya hivyo, walijua viongozi hao wangefuata nyayo kama za wenzao waliotoka Simba mwaka 1975 na kuunda Nyota Nyekundu.


PAN YAANZISHWA

Agosti 1976 Klabu ya Pan Afrika ilisajiliwa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam baada ya kukubaliwa usajili ilipoungana na Zama za Kale.

Wachezaji wa kwanza waliounda Pan Afrika ni pamoja na kipa wa zamani wa Simba, Athumani Mambosasa.

Mambosasa alijiunga na Pan akitokea Nyota Afrika kwa kuwa lengo lake la kwanza ni kutoka Simba na kujiunga na Yanga. Hivyo akaondoka na wachezaji hao kwenda nao Morogoro.

Wengine ni Ali Yusuf, Boi Idd ‘Wickens’, Nondo, Mikidadi, Muhaji Muki, Omari Kapera ‘Mwamba’ na Kitwana Manara ‘Popat’.

Pia walikuwepo kina Juma Matokeo, Leodeger Tenga ‘Injinia’, Juma Shaaban, Gibson Sembuli, Jellah Mtagwa, Sunday Manara ‘Computer’ na Mohamed Migea.

Wengine ni Zakaria Digosi, Idd Said China, Kivera James, Idd Sululu na Said Juma.

Pia kina Mohamed Hussein, Michael Mapunda, Ahmed Johari, Hassan Mohamed Mwangi, Kassim Manara, Adolf, Mohamed Yahya ‘Tostao’, Gordian Mapango, Jaffar Abdulrahaman, Mohammed Mkweche, Juma Nassoro, Juma ‘Mensah’ Pondamali na Haruna Hemed.

Awali Pan ilihifadhiwa na Kikundi cha Taarab cha Egyptian Mtaa wa Swahili na Mkunguni kwa Bi Hanifa na baadaye kumiliki Jengo lao Mtaa wa Swahili na Kariakoo.


MANGARA AMWIBUA BAKHRESA

Zamani kulikuwa na ushirikiano mkubwa wa michezo kati ya Bara na Zanzibar.

Kila mwaka katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka kulikuwa na ugeni wa timu kutoka Bara kwenda Zanziba na mwaka unaofuata za Zanzibar zinakwenda Bara.

Mfano Simba walikuwa wageni au wenyeji wa Kikwajuni, Yanga walikuwa na Mlandege na Pan ikaanzisha urafiki na KMKM. Kilikuwa ni kipindi cha timu za Zanzibar kuja Dar es Salaam.

Kiongozi wa Pan, Mangara Tabu Mangara akawa anatafuta ufadhili wa kuwaweka hotelini wageni wake kutoka Zanzibar, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Hapo ndipo alipomfuata Bakhressa aliyekuwa na hoteli maeneo ya Gerezani, jijini Dar es Salaam.


MANGARA HADI KWA NYERERE

Hata hivyo, alikutana na kipingamizi. Inadaiwa tajiri huyo bidhaa zake za mchele, ngano na nyinginezo zilikuwa zimekamatwa na serikali.

Habari za ndani zaidi zinasema mfanyabiashara huyo alimwambia Mzee Mangara alikuwa amekwenda kuazima jamvi msibani. Ndipo alimpompa habari za kukamatwa kwa bidhaa zake.

Baada ya kupewa kisa hicho, Mzee Mangara alimwahidi kumsaidia Balkhressa kumpeleka hadi kwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere.

Kweli Mzee Mangara alifanikisha mpango huo na bidhaa zote za Bakhressa zikaachiwa na serikali.


ZA NDANIII KABISA

Baada ya bidhaa zake kuachiwa na mambo kurudi kama zamani, KMKM walifika Dar es Salaam na kuhudumiwa vizuri na Pan Afrika.

Lakini kwa kitendo alichofanyiwa, mfanyabiashara huyo, habari za ndani kabisa zinasema alimwambia Mzee Mangara atafute kiwanja ili amjengee nyumba ya ghorofa ambayo ingekuwa na floor nne.

Hata hivyo, Mzee Mangara alimwambia mfanyabiashara huyo asimjengee yeye kama yeye, bali aijengee klabu ya Pan jengo ili iweze kujistiri.

Tajiri Bakhressa akamwambia basi kama ni klabu angeijengea ghorofa moja. Kweli alifanikisha ahadi yake hiyo.

Hadi leo Pan pamoja na kwamba imepotea katika ushindani wa Simba na Yanga lakini ina jengo lake pale Mtaa wa Swahili na Kariakoo.


HII NDIO PAN AFRIKA

Kuzaliwa kwa Pan Afrika kuliongeza ushindani kati yake ya Klabu za Simba na Yanga na sokala Tanzania kwa ujumla.

Mwaka 1979, Simba ilitwaa ubingwa na Pan ilishika nafasi ya pili na kucheza Kombe la Washindi Afrika ambapo ilitolewa katika raundi ya pili.

Mwaka 1980 Simba ilibeba tena ubingwa na Pan ikarudia katika nafasi yake katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na katika Kombe la Washindi ikatolewa tena katika raundi ya pili.

Mwaka 1982 ilitwaa ubingwa wa Tanzania na hata ilipoenda kushiriki Klabu Bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa) ilitolewa tena raundi ya pili.

Mwaka 1983, Yanga ilishinda ubingwa na Pan ilishika nafasi ya pili tena na kushiriki Kombe la Washindi la kutolewa raundi ya pili

Mwaka 1989, Malindi ya Zanzibar ilitwaa ubingwa wa Tanzania na Pan ilishika nafasi ya pili tena na kutolewa katika hatua ya awali.

Pan ilikuwa bingwa wa Kombe la Nyerere mara tatu, 1978, 1979 na 1981.



HIZI HAPA NYEPESI NYEPESI

Habari zisizokuwa rasmi zinasema Pan Afrika ilipotezwa na mtaalamu wa tiba za asili (mganga) wa Zanzibar ambaye aliihakikishia klabu hiyo kuchukua ubingwa wa mwaka 1982.

Inadaiwa viongozi wa Pan waliambiwa wakifanikiwa kuwa mabingwa kabla ya kufanya chochote, walipeleke kombe kwa mtaalamu huyo.

Hata hivyo, hilo halikutimizwa baada ya kunyakua ubingwa kwa kuifunga Malindi, mjini Unguja, walipanda boti na kombe lao na kurejea Dar. Wakapuuza masharti ya mtaalamu!


Kwa maoni na ushauri naomba tuwasiliane kwa namba 0713-900017