Miamba ya magoli na maajabu ya penalti

Muktasari:
- Hilo nalo lilizua utata kama lile ambalo lilikuwa la mwendo kasi na kupita pembeni huku waliokuwa wahesabike wamefungwa wakisema sio bao na wapinzani wao wakisema ni bao.
HAPO zamani magoli katika kandanda yalikuwa sababu kubwa ya mizozo na hata kuifanya michezo kumalizika kabla ya muda uliopangwa. Magoli ya zamani hayakuwa na jiti au ubao wa juu na kwa hiyo hata mpira uvuke juu vipi katika eneo lilipokuwa kati ya nguzo za goli, basi yalihesabika kuwa ni bao.
Hilo nalo lilizua utata kama lile ambalo lilikuwa la mwendo kasi na kupita pembeni huku waliokuwa wahesabike wamefungwa wakisema sio bao na wapinzani wao wakisema ni bao.
Utata huo ambao wakati mwingine ulisababisha wachezaji na mashabiki kupigana, ulifanya magoli kufanyiwa marekebisho makubwa hadi kufikia namna yanavyoonekana hivi leo. Hapo mwanzo haikuwapo sheria ya upana wa goli wakati ilipokuwa inatumika miti au mbao kwa kuweka nguzo mbili, na hapakuwepo mwamba uliounganisha hiyo miti au mbao.

Halikuwa jambo la ajabu katika miaka ya nyuma kukuta goli moja kuwa pana kidogo kuliko jingine au nguzo imepinda kidogo na kulifanya goli kuwa jembamba kidogo katika baadhi ya sehemu. Mwamba wa goli ulianza kuwekwa kama pendekezo 1875 na kuwa ni lazima kuanzia 1882, na sheria kutungwa kwa goli kuwa na upana wa futi 24 na urefu wa futi 8 kutoka chini. Kipimo hicho kinatumika hadi leo, lakini vipo vipimo ambavyo ni vidogo kidogo kwa magoli ya watoto, vijana na wanawake.
Katika siku za karibuni baadhi ya wataalamu wa mchezo wa kandanda na wachezaji marufu wastaafu wamekuwa wakishauri upana wa goli uongezwe kwa futi moja na urefu inchi sita, lakini pendekezo hilo kila likijadiliwa matokeo yake ni kuwekwa kapuni.
Mwamba wa juu wa goli ulianza kutumika katika fainali ya Kombe la FA kule England 1872 kati ya Wanderers and Royal Engineers katika Uwanja wa Kennington ambapo Wanderers walishinda bao 1-0. Lakini huo mwamba ulikuwa wa utepe wa kitambaa na ilionekana kama hatua muhimu ya kupunguza migorogo, na ilipofika 1882 utepe ulionndolewa na kuwekwa mwamba wa ubao. Hata hivyo kuwekwa kwa mwamba wa ubao haukumaliza utata, bali ulipunguza matatizo.

Adhabu ya tuta yaani penalti panapokuwa na mchezo mbaya ndani ya eneo la hatari haikuwepo zamani. Adhabu hiyo ilianzishwa 1890 na William McCrum ambaye alikuwa mfanyabiashara na alicheza soka kama kipa. Kuwepo kwake kulikubalika katika mkutano uliofanyika katika mkutano wa Chama cha Kandanda cha Shefield, England 1891 na 1902 iliangizwa rasmi katika mfumo wa kandanda na kuwekwa kipimo kinachotumika hadi sasa cha yadi 12 (mita 11) kutoka lilipo goli.
Wachezaji walitakiwa wawe nje ya eneo la hatari pale penalti inapopigwa. Mwaka 1905 ilitungwa sheria ya kumtaka kipa asitikisike akiwa amesimama kwenye mstari wa goli mpaka mpira utapopigwa, lakini sheria hiyo ikafutwa na kukubaliwa 1997 kutikisika anavyotaka wakati penalti inataka kupigwa.
Lakini, 1970 likazuka tatizo jingine katika upigaji wa penalti - nalo ni la anayepiga mpira kusita wakati akipiga mpira, tabia iliyoanzishwa na aliyekuwa akitambulika kama Edson Arantes do Nascimento (Pele) ambaye aliaga dunia 2022 akiwa na miaka 82. Kwanza ilikatazwa na ilipotokea mchezaji alitakiwa apige tena mpira, lakini baadaye uamuzi huo ukatengwa mnamo 1985.

Kwa miaka mingi zilitumika njia mbalimbali kutafuta mshindi pale timu zikienda sare katika michezo ya mtoano. Awali, ilikuwa inatumika njia ya kurudia mchezo, lakini nayo ilikuwa na tatizo kwa vile ilikuwa inatokea timu zinakwenda sare mara mbili hadi tatu na kutopatikana mshindi.
Kwanza ukawekwa muda wa nyongeza wa dakika 30 zilizogawiwa pande mbili kila moja kwa dakika 15 na baada kuongezewa muda wa dakika chache kwa zile zilizopotezwa kwa makusudi au kukawiza mchezo alipotokea mchezaji kujeruhiwa au kutoelewa.
Njia moja nyingine iliyotumika ni kurusha sarafu na atakayebahatika ndiye huwa mshindi. Hii ilianza kutumika mara chache kuanzia 1867, lakini ikapewa nguvu kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1960.

Miongoni mwa klabu ambazo zilipoteza ushindi kwa aina hiyo ni Yanga ya Dar es Salaam ilipotolewa na Asante Kotoko ya Ghana 1969 katika mashindano ya Afrika. Matumizi ya sarafu kuamua mshindi yalizusha lawama nyingi na hasa katika mashindano ya Ulaya, Olimpiki na Kombe la Dunia. Baada ya mjadala mrefu ikakubaliwa mtindo wa kupiga penalti tano baada ya kupulizwa filimbi ya kumaliza muda wa kawaida.
Katika mashindano ya Kombe la Ulaya 1976 ndipo ukatumika mtindo huu, na mchezo wa kwanza ulikuwa katika fainali kati ya Czechoslovakia na Ujerumani ambapo Wajerumani walishinda 5-4. Katika kutafuta Kombe la Dunia pia ulitumika.
Katika historia fupi ya kutumika mtindo huo wa kupigiana matuta kupata mshindi mchezo ulioweka historia ya kuwa na penalti nyingi mpaka mshindi kupatikana ni kati ya Dimona na Shimson Tel Aviv zote za Israel. zilihitajika kupigwa penalti 56 ndipo akapatikana mshindi Septemba 18, 2004.

Mwaka 2006, mchezo wa robo fainali za Afcon uliofanyika Misri kati ya Cameroon na Ivory Coast uliweka rekodi ya kupigiana matuta katika mashindano hayo. Ivory Coast ilishinda 12-11. Kabla ya hapo 1992 Ivory Coast iliifunga Ghana 11-10 katika mchezo wa fainali wa Afcon katika Uwanja wa Leopold Sedar Senghor uliopo Dakar, Senegal.