Miaka nane ya Juma Abdul Jangwani

Muktasari:

HAKUNA aliyeamini kama mabeki wakongwe waliokuwa Yanga, Kelvin Yondani na Juma Abdul wangeondoka Jangwani kirahisi kama ilivyotokea msimu huu.

HAKUNA aliyeamini kama mabeki wakongwe waliokuwa Yanga, Kelvin Yondani na Juma Abdul wangeondoka Jangwani kirahisi kama ilivyotokea msimu huu.

Yanga iliachana na wachezaji hao wakiwa waliodumu muda mrefu na waliokuwa wametengeneza ukuta imara wa timu hiyo, na hii ilitokana na kushindwa kukubaliana nao kwenye masilahi mikataba mipya ambayo wangesaini.

Hiyo ni kutokana na namna ambavyo wachezaji hao walivyokuwa viongozi na kukaa muda mrefu katika kikosi hicho wakishinda mataji mbalimbali.

Yondani inaelezwa kwamba ametua zake Namungo wakati Juma Abdul alitimkia Zambia na kujiunga na Klabu ya Indeni FC akipishana na Hassan Kessy aliyeachwa Nkana FC.

Mwanaspoti lilimtafuta beki huyo wa kulia na kufanya naye mazungumzo ya namna ambavyo aliondoka katika kikosi cha Yanga mpaka alipotua kikosi cha Indeni, na kufunguka maisha yake ya miaka minane ndani ya klabu hiyo kongwe nchini na Afrika Mashariki na Kati.


YEYE, YANGA KIROHO SAFI TU

Wengi wanajua kwamba kuondoka kwa Abdul katika kikosi cha Yanga ni kama vile jamaa atakuwa alimaindi, lakini mwenyewe wala hajali.

Mawazo ya wengi kuhusu Abdul ni kutokana na namna ambavyo alipambana na timu hasa katika kipindi ambacho ilikuwa ikipitia katika wakati mgumu.

Mwenyewe anasema anajua kwamba suala la kuondoka kwake katika kikosi cha Yanga ni la muda tu kuisha kwa sababu waajiri wake wa zamani walikuwa wanatengeneza timu mpya.

“Nadhani ulifika muda wa wao kuona kwamba ni muafaka wa kutengeneza timu yao mpya, hii itakuwa kwa mchezaji yeyote yule ambaye atakuwa amekaa Yanga muda mrefu,” anasema.


SAFARI YA ZAMBIA

Wakati wote ambao alikuwa akicheza kwa takriban miaka minane - tena akiwa katika kiwango bora, Abdul hakuweza kupata hata ofa ya kufanya majaribio sehemu yoyote.

Lakini baada ya kuachana na Yanga, mchezaji huyo anasema alipokea simu ya wakala na kutaka wafanye kazi pamoja na ndipo alimpa ofa ya kwenda kucheza nchini Zambia.

“Siku zote kwanza Mungu ndio huwa anapanga kila kitu, mimi baada ya kushindwana na Yanga niliamua kutulia nyumbani kwanza ndio nikapigiwa simu na wakala akaniambia anataka tufanye kazi,” anasema.

“Alikuwa ni mtu ambaye ananifuatilia sana na soka la Bongo pia, kwahiyo baada ya kukubali alianza kuangalia katika timu ambazo alikuwa anafanya nazo kazi ipi ina ofa nzuri.

“Baada ya kwenda Zambia unajua kumbe timu ilikuwa mpya na kulikuwa na wachezaji wengi walifika pale ila wasifu wangu uliamini mwalimu ataniamini, nilifanya mazoezi siku tatu kisha nikasaini.”


HAAMINI KUCHELEWA

Wengi wanaona mchezaji huyo kutokana na umri wake wa miaka 27 ambao uko katika hati yake ya kusafiria ni kama vile amechelewa kutoka kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini kwa upande wake bado ana imani na umri wake.

Abdul anasema suala la kutoka kwenda kucheza soka la kulipwa mipango ya Mungu ilikuwa bado haijatimia, hivyo kwa sasa imetimia na ndio maana ametoka.

“Binafsi, naweza kusema kama sio muda niliokuwa nauhitaji mimi, yaani sio mimi ambaye napanga bali ni Mungu na siku zote kila kitu kinatokea kwa sababu Mungu ndio hupanga,” anasema Abdul, beki wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.


MIAKA miNANE YANGA, MAISHA NA MAKOMBE

Unapomuuliza Abdul swali kuhusu mafanikio aliyopata akiwa na Yanga, kidogo anaweza kugeuka mbogo kwani anaonyesha kwamba hataki kuzungumzia maisha yake nje ya uwanja.

“Mafanikio yapo mengi kaka, ulishawahi kuona naonyesha kitu ninachokifanya, sijawahi na wala sipendi ila ukweli namshukuru Mungu kuna vingi tu.”

Kwa upande wa mafanikio ya uwanjani, anasema anajivunia katika kuchukua makombe akiwa na kikosi hicho kwani sio jambo jepesi.

“Tumebeba ubingwa wa ligi mara nne, Kagame (Konmbe la Afrika Mashariki na Kati -Cecafa) mara moja na mimi mwenyewe kuwa mchezaji bora wa FA (Kombe la Shirikisho) na ligi, hili ni jambo kubwa kwangu kiukweli.”


TAMBWE NA PLUIJM

Wakati tukichati na Abdul nilimchomekea swali la yupi ni mshambuliaji wake bora wa muda wote wakati anacheza Ligi Kuu Bara pamoja na kocha bora ambapo anamtaja straika wa zamani Yanga, Amissi Tambwe na kocha Hans Pluijm.

Abdul anasema Tambwe ni mshambuliaji ambaye analijua goli lilipo, huku Pluijm alikuwa kocha ambaye pia ni kama mzazi kwa wachezaji aliowafundisha.

“Tambwe ni mshambuliaji ambaye analijua sana goli na huwa hana mambo mengi zaidi ya kufunga, Pluijm alikuwa ni rafiki kwa kila mchezaji ndani na nje ya uwanja,” anasema Abdul.

“Hiyo ilisababisha kila mchezaji akipewa nafasi kucheza, basi anacheza kwa kujiamini kutokana na namna ambavyo ametengeneza kujiamini kutokana na urafiki wa kocha.”


KIKOSI CHA USHINDI

Kila mchezaji huwa na kikosi chake bora pindi anapokuwa anacheza katika timu fulani, hilo pia hata kwa Abdul lipo na hakusita kutaja kikosi chake.

Anakitaja kikosi hicho bora muda wote akiwa Yanga kuwa ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kelvin Yondani, Thaaban Kamusoko, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa na Deus Kaseke huku akimuongezea Vincent Bossou.


BAHANUZI AMUACHIA ALAMA

Unamkumbuka yule mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi alivyokuwa anatamba akiwa anatamba na timu hii, basi jamaa licha ya kutamba amemuachia Abdul kovu la moyoni.

Abdul anasema tukio ambalo hawezi kulisahau ni mshambuliaji huyo alipokosa penalti katika mchezo wao dhidi ya Al Ahly ya Misri. “Tukio ambalo siwezi kulisahau ni Bahanuzi alivyokosa penalti kwa sababu tulikuwa tayari tuna matumaini ya kuwatoa,” anasema. Katika mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 na kupigiana mikwaju ya penalti, lakini ulimalizika kwa Al Ahly kushinda kwa jumla ya mabao 4-3. Yanga waliwafunga wageni wao hao 1-0 katika Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) na waliporudiana Al Ahly ilishinda 1-0 na kufanya matokeo yawe 1-1.


ABDUL NI NANI?

Ukikutana na Abdul nje ya uwanja ni mtu ambaye hapendelei kupiga pamba na huonekana kama mtu wa kunata, lakini anasema ni mtu wa kawaida. Anasema huwa hapendi mambo mengi anapokuwa nje ya uwanja na anaishi maisha ambayo mtu yeyote huishi anapokuwa nyumbani.

“Mimi nje ya uwanja ni mtu wa kawaida sana kwa sababu napenda kuishi maisha ambayo kila mtu wa kawaida anapenda kuishi, pia mimi ni mcheshi sana.”

____________________________________________________________

Na THOMAS NG’ITU