Miaka 60 ya kihistoria michezoni

Thursday October 07 2021
60 pic
By Mwandishi Wetu

DESEMBA 9, mwaka huu Watanzania hususan wale wa Tanzania Bara wataadhimisha miaka 60 tangu Tanganyika ipate Uhuru kutoka kwa Waingereza. Ukiitazama historia kuanzia soka na michezo mingine kuna mambo ya kujivunia.

Ilikuwa ni miaka miwili na miezi kadhaa tangu Tanganyika hadi iliposhiriki mashindano ya kimataifa kama Taifa huru.

“Tulikuwa wageni kwenye kila kitu. Kuna muda tulilazimika kutumia ishara ili kupata huduma,” anasema Daniel Thomas, mmoja wa Watanganyika wa kwanza kushiriki Olimpiki 1964 iliyofanyika Tokyo, Japan ambako Tanganyika iliwakilishwa na wanariadha wanne - Hassan Dyamwale, Paschal Mfyomi na Omary Abdallah.

Thomas anasema safari ya Tanganyika katika Olimpiki hiyo ya kwanza baada tu ya Uhuru, ambapo enzi hizo pia alikuwa alikuwa mwalimu wa moja ya shule za msingi huko Musoma vijijini ambako ndiko anaishi, anakumbuka walivyoalikwa Ikulu, Dar es Salaam na Mwalimu Julius Nyerere kuwapongeza mara baada ya kurejea kutoka Japan.

Miaka minne baada ya Uhuru Tanzania iliweka rekodi ya kwanza ya medali ya kimataifa kupitia kwa mwanariadha Theresia Dismas aliyeshinda medali ya shaba kurusha mkuki kwenye Michezo ya Afrika (All Africa Games) ya 1965 iliyofanyika Brazzavile, Kongo.

Mwanariadha mwingine Mtanzania, John Stephen Akhwari alikuwa kwenye timu ya Tanzania iliyoshiriki michezo ya pili ya Olimpiki ya 1968 nchini Mexico. Huko alimaliza wa mwisho mbio za marathoni za kilomita 42.

Advertisement

Katika mbio hizo, Akhwari aliumia na kufungwa bandeji mguuni, huku akivuja damu lakini aliendelea kukimbia polepole huku akichechemea, wakati asilimia kubwa ya mashabiki wakiwa wameondoka uwanjani ndipo alipoingia akiwa anachechemea.

“Nilipohojiwa niliwaeleza taifa langu halikunituma kuanza (mbio), bali kumaliza,” anasema Akhwari ambaye alitumia saa 3.25.27 akiachwa kwa zaidi ya saa moja na bingwa wa mbio, raia wa Ethiopia, Mamo Wolde aliyetumia saa 2.20.26.

Kwa upande wa ndondi, timu ya Taifa ya ngumi ilipata medali ya kwanza ya kimataifa iliyoshinda miaka tisa baada ya Uhuru kupitia kwa Titus Simba kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1970. Tanzania iliendelea kujidhihirisha michezoni kwa kuvunja rekodi ya dunia katika riadha. Filbert Bayi aliendelea kufanya vyema kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwamo Olimpiki huko Moscow, Urusi 1980 alipotwaa medali ya fedha. Kwenye michezo hiyo, Suleiman Nyambui pia alitwaa medali kama hiyo kwenye mbio za mita 5000.

Moja ya mbio kubwa duniani ni ile ya New York Marathon ambayo katika miaka 60 ya Uhuru, Tanzania ina historia ya kuwa bingwa wake mwaka 1989. Juma Ikangaa alikiwa bingwa wa mbio hiyo kubwa alitumia saa 2.08.01 kabla ya kutwaa medali za fedha mara mbili kwenye mbio nyingine kubwa ya Boston Marathon 1988 na 1990. Mbio nyingine ambazo Ikangaa alifanya vizuri ni ile ya Fukuoka na Melbourne Marathon, mashindano ya Afrika ya 1984 na michezo ya Madola ya 1982.

Kwa upande wa wanawake, Mwinga Mwanjala ana rekodi yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki.


Alishiriki michezo ya Olimpiki ya 1980 na ana rekodi nzuri kwenye mbio za mita 800 na 1500.

Zakia Mrisho naye ni miongoni mwa wanariadha waliotamba kimataifa katika mbio za mita 3000 na 5000. Mwaka 2005 alishika nafasi ya tatu katika mashindano ya dunia huko Monte Carlo, Monaco nchini Ufaransa. Pia aliwahi kuwa kinara kwenye mashindano ya Diamond League ya 2004, 2005 na 2009. Failuna Abdi naye alikuwa mchezaji pekee aliyeiwakilisha nchi kwenye Olimpiki 2021 nchini Japan. Wengine ni Alphonce Simbu aliyetwaa medali ya shaba ya dunia kwenye mbio za marathoni na pia kuweka rekodi ya kuingia kwenye tano bora ya Olimpiki ya Rio 2016 na London Marathon huku akibeba dhahabu ya mbio za Mumbai Marathon.

Rekodi nyingine ni ya Samson Ramadhan aliyetwaa medali ya dhahabu ya mwisho kwa Tanzania kwenye Jumuiya ya Madola 2006 nchini Australia, huku Fabiano Joseph akishinda shaba kwenye mbio za mita 10,000. Samwel Mwera, ambaye yupo timu ya Afrika iliyoshiriki mashindano ya Afro Asian, alishinda shaba katika mbio za mita 800. Mwera alipata nafasi hiyo baada ya kuwa bingwa wa mbio za mita 800 kwenye michezo ya Afrika ya 2003 huko Abuja, Nigeria akitumia dakika 1.46.13.

Mwanariadha mwingine ni Fabiano Joseph ambaye alishinda Dola 100,000 kwenye moja ya mbio kubwa za pesa duniani mwanzoni mwa mwaka 2000.

Vilevile katika miaka 60 ya Tanganyika kuna bondia Rashid Matumla ambaye ni miongoni mwa mabingwa wa ngumi za kulipwa nchini wa kihistoria. Matumla au Snake Man kama anavyopenda kujiita ameweka rekodi ya kuwa bingwa wa dunia wa WBU.

Francis Cheka ni bondia mwingine aliyefuata baada ya Matumla na rekodi yake ya kuwa bingwa wa dunia wa WBF.

Cheka alivuliwa ubingwa huo baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, japo baada ya wiki kadhaa alipata msamaha na kupewa kifungo cha nje. Hivi sasa amestaafu yupo nchini Msumbiji alikozaliwa mama yake, Maria Rafael.

Hasheem Thabeet ametikisa vyombo vya habari akiwa ni Mtanzania ambaye alipata mafanikio kwenye mpira wa kikapu. Nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania wa kikapu katika miaka 60 ya Uhuru ametengeneza rekodi ya kuwa Mtanzania kucheza Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) mwaka 2009 na miongoni mwa timu alizocheza ni Memphis Grizzlies, Dakota Wizards, Houston na Oklahoma City Thunder.

Katika miaka ya karibuni, bondia Hassan Mwakinyo aliandika rekodi ya kihistoria 2018 alipomchapa kwa TKO, Sam Eggington nyumbani kwao nchini Uingereza - pambano ambalo lilishtua dunia kutokana na rekodi ya mabondia hao, Eggington akiwa namba nane duniani na Mwakinyo 179. Pambano hilo lilimpandisha Mwakinyo hadi nafasi ya 14 duniani, kabla ya kumchapa Eduardo Gonzalez wa Argentina katika pambano lililopigwa Kenya na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli kumualika Ikulu, Dar es Salaam na kumzawadia kiwanja Dodoma.


Michael Yombayomba

Hadi mauti inamkuta 2015, rekodi ya Michael Yombayomba haikuwa imevunjwa kwenye timu ya taifa ya ngumi za ridhaa.

Yombayomba ni bondia pekee nchini kutwaa medali ya dhahabu ya kimataifa ambayo alishinda 1998 kwenye michezo ya Madola huko Kuala Lumpur, Malaysia. Hata hivyo bondia huyo hakupata nafasi ya kutetea medali kwenye michezo iliyofuatia ya 2002 ya nchini Uingereza.

Wengine walioandika rekodi katika miaka 60 ya Uhuru ni bondia Habibu Kinyogoli na Haji Matumla pamoja na wanariadha Gidamis Shahanga na Zacharia Barie ambao wana historia ya medali kwenye michezo ya Afrika na Madola.


SOKA NAKO MOTO

Ukiachana na mafanikio kwenye michezo hiyo, pia kwenye soka nako kuna alama kadhaa zimewekwa tangu nchi ipate Uhuru, kwani kama nchi ilijishughulisha na mchezo huo hata kabla ya Uhuru.

Klabu na wanamichezo mbalimbali wamekuwa na mchango mkubwa wa upatikanaji wa Uhuru zikiwamo Simba na Yanga zilizoanzishwa zaidi ya miaka 85 iliyopita.

Historia inaonyesha Tanganyika iliasisi Chama cha Soka 1945 na kushiriki michuano mbalimbali hususan iliyohusisha nchini za Afrika Mashariki inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Michezo katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) lililoasisiwa 1926.

Tanganyika ilishiriki michuano ya Kombe la Gossage iliyochezwa kati ya 1926-1966, kisha ikabadilishwa na kuwa Kombe la Chalenji ikichezwa kati ya 1967-1971 na baadaye kuasisiwa tena kwa Kombe la Cecafa 1973 hadi sasa.

Rekodi zinaonyesha taji la kwanza la michuano hiyo wakati ikiwa bado Tanganyika ililibeba 1949 - miaka minne tangu kuasisiwa kwa Chama cha Soka (sasa Shirikisho - TFF) kisha ikabeba tena 1950 na 1951, 1964, 1965, 1974, 1994 na 2010.

Upande wa Zanzibar ililitwaa kombe hilo mara moja tu - 1995.


MICHUANO YA AFRIKA

Mbali na kung’ara katika michuano ya Cecafa, Tanzania pia imefuzu fainali nne tofauti za Afrika ikiwamo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 michuano hiyo ilipofanyika Nigeria na mwaka 2019 ilipofanyika Misri.

Kadhalika, imefuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ardhi za nchi zao (Chan 2009) za kwanza tangu zilipoasisiwa na kisha kufanya hivyo tena mwaka jana, japo michuano ilichezwa mwaka huu.


NYOTA WAWILI

Tanzania iliweka rekodi ya kutoa nyota wawili katika kikosi cha Afrika kupitia michuano ya All Africa Games ya 1973 iliyofanyika Nigeria kwa kipa Omary Mahadh Bin Jabir na Maulid Dilunga kung’ara na Taifa Stars. Wachezaji hao waliungana na wenzao wa mataifa mbalimbali waliounda timu ya Afrika kufanya ziara nchi tofauti ikiwamo Mexico na kusababisha Hayati Maulid kama Mahadhi kubatizwa jina la Mexico.

Pia, Tanzania imefuzu fainali nne tofauti za vijana ikiwamo za Afcon U17 mwaka 2017 zilizofanyika Gabon kisha ikawa wenyeji 2019 na mwaka huu ilifuzu, ila michuano ilifutwa, huku kwa Afcon U20 imeshiriki mara moja - 2021.


NGAZI YA KLABU

Katika ngazi ya klabu Tanzania ina rekodi kadhaa za kujivunia ikiwamo kubeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) mara 13 - Simba ikibeba mara sita ikiwa ndio kinara katika michuano hiyo na Yanga iliyotwaa mara tano ilhali Azam ikiubeba mara mbili.

Licha ya Tanzania kutowahi kubeba ubingwa wa Afrika ingawa ilianza kushiriki tangu 1969, lakini timu za

Simba, Yanga na Namungo zimejitutumia na kufika hatua mbalimbali katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani humu zinazolipa heshima Taifa.

Simba imefika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) 1974, kisha kufika fainali ya michuano ya Kombe la CAF 1993 - taji lililotolewa na mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Moshood Abiola 1992 kabla ya michuano hiyo kuzikwa 2004 kwa kuunganishwa na ile ya Kombe la Washindi Afrika na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika linalochezwa hadi sasa.

Simba pia imefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu 2003, 2018-2019 na 2020-2021 ambapo 2019 na 2021 ilifika hatua ya robo fainali na kukwama mbele ya TP Mazembe na Kaizer Chiefs.

Yanga, klabu iliyoasisi kucheza michuano ya Afrika imewahi kufika mara kadhaa robo fainali ya michuano ya Kombe la Washindi, kucheza makundi mara tatu, 1998 ilicheza Ligi ya Mabingwa na 2016 na 2018 ilifanya hivyo katika Kombe la Shirikisho.

Kwa upande wa Namungo ilifanya hivyo mwaka jana katika Kombe la Shirikisho, huku Malindi ya Zanzibar ikifika hatua za robo na nusu fainali miaka ya 1990 katika Kombe la Washindi.


SOKA LA WANAWAKE

Ndani ya miaka 60 ya Uhuru imeshuhudia pia soka la wanawake likipata heshima kubwa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na All Africa Games kwa miaka tofauti, huku ikitwaa mataji katika michuano ya Cecafa na ile ya Cosafa inayohusisha nchi za Kusini mwa Afrika inapoalikwa kama ilivyo mwaka huu.

Kupitia timu za taifa za U17, U20, U23 na Twiga Stars, Tanzania inatembea kifua mbele katika soka la wanawake Afrika, huku ikiwa na Ligi Kuu bora ya soka hilo iliyoasisiwa 2016 na aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Rais wa TFF, Wallace Karia na katibu mkuu Wilfred Kidao wamekuwa mara kadhaa wakijivunia mafanikio chini ya uongozi wao kwa soka kuonekana kupiga hatua kubwa, lakini pia wakijivunia kuweza kushawishi wadhamini kuwekeza katika soka.

“Hili ni jambo la kujivunia, ingawa bado tunajitahidi kuhakikisha soka linapata udhamini wa kutosha kuwezesha ligi zote kuanzia Ligi Kuu Bara, Championiship na SDL sambamba na ile ya Wanawake (WPL) zinapata udhamini,” anasema Karia.

Kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara iliyoasisiwa 1965 na klabu sita ambazo ni Tobacco au Sigara, Young Africans (Yanga) na Sunderland (Simba) zote kutoka Pwani, Coastal Union na Manchester United (Tanga) na TPC (Moshi) ina udhamini mnono wa mabilioni ya fedha kutoka kampuni ya Azam Media na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mbali na udhamini huo, lakini soka la Tanzania pia limeweka heshima kubwa kwenye mataifa mengine kwa nyota waliobahatika kwenda kucheza soka la kulipwa akianza Sunday Manara, Renatus Njohole, Danny Mrwanda, Henry Joseph, Mbwana Samatta, Saimon Msuva na wengineo.

Makala maalumu ya safari ya nyota wa Tanzania katika soka la kulipwa nje ya nchi pamoja na namna sanaa na muziki ilivyotamba tangu Uhuru, itawajia katika mfululizo wa makala za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.

Advertisement