Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 21 ilivyokomeshwa na Azam

AZAM Pict

Muktasari:

  • Baada ya ushindi wa mabao 2-0 kule Zanzibar, wiki iliyopita katika mechi ya kwanza, Azam ikajihakikishia tiketi hiyo ikishinda kwa kishindo mabao 7-0 nyumbani pale Azam Complex, ikisafisha nyota.

KAMA ulivyosikia, Azam FC imefanikiwa kuandika historia mpya, baada ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikikata tiketi hiyo kibabe kwa kuing'oa KMKM ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0.

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 kule Zanzibar, wiki iliyopita katika mechi ya kwanza, Azam ikajihakikishia tiketi hiyo ikishinda kwa kishindo mabao 7-0 nyumbani pale Azam Complex, ikisafisha nyota.


MIAKA 21 YA HISTORIA

Azam ilikuwa inazishuhudia timu nyingine zikitinga makundi tena wakitumia uwanja wao wa Azam Complex, lakini sasa baada ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, ikafanikiwa kubadilisha heshima yao kwa kukata tiketi hiyo ya kwenda hatua ya juu baada ya zile mechi za mtoano.

Huu ukiwa ni msimu wake wa 11 kushiriki tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 2004, Azam ilikwama mara 10, safari hii imetoboa.

Azam iliyoanza kushiriki michuano ya CAF mwaka 2013, ilikuwa haijawahi kucheza makundi ambapo mara mbili imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na 2024-2025, zote imeishia hatua ya awali.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya msimu huu kufuzu makundi, huko nyuma imewahi kujitahidi na kufika hatua ya pili.

Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2013 na kuishia hatua ya kwanza, kisha 2014 (hatua ya awali), 2016 (hatua ya pili), 2017 (hatua ya kwanza), 2019–2020 (hatua ya kwanza), 2021–2022 (hatua ya pili), 2022-2023 (hatua ya pili), 2023-2024 (hatua ya kwanza).

AZA 03

IBENGE SHUJAA WA MCHEZO

Tiketi ya Azam kwenda makundi imekuja chini ya utawala wa kocha Mkongomani, Florent Ibenge, akivunja mfupa uliowashinda makocha waliomtangulia.

Azam chini ya Ibenge imecheza mechi nne za mtoano, ikishinda zote bila ya kuruhusu bao, lakini utamu ni kwamba imekuwa ikicheza soka la utulivu mpaka inajihakikishia tiketi hiyo ya kwenda makundi.

Ibenge ni kocha mzoefu kwenye mashindano ya Afrika na endapo ataendelea kuaminiwa ndani ya Azam, haitashtua kuona timu hiyo ikienda mbali zaidi ya hatua ya makundi kwa kuwa amewahi sio tu kuzifikisha mbali klabu mbalimbali bali amewahi kulibeba taji hilo la Shirikisho.

Huenda kazi yake njema ikazidi kumpa ulaji ndani ya Azam, kwani amesaini mkataba wa mwaka mmoja, wenye kipengele cha kuongezeka kama huduma yake itawaridhisha mabosi hao wa Chamazi.

AZA 04

AZAM NZITO, KMKM WEPESI

Haikuwa mechi ngumu kwa Azam, kwani ilitawala vizuri mchezo huo hata mabao yake yalithibitisha kwamba matajiri hao wa Chamazi walikuwa na kitu kizito mbele ya KMKM, ambao walishindwa kufanya kitu kikubwa kwenye lango la wenyeji wao.

Azam ilianza kuonyesha ukubwa wake kuanzia ugenini hadi ilipoikaribisha nyumbani Chamazi, unaweza kusema imefuzu kibosi sana tena kwa ushindi mzito.


AZAM MBELE MOTO, NYUMA BALAA

Huwezi kuacha kuipongeza safu ya ushambuliaji ya Azam imeimarika zaidi, ambapo msimu huu hakuna mechi ambayo imetoka bila kufunga bao kwenye mashindano inayoshiriki na hata ukuta wao hauvuji sana kulinganisha na msimu uliopita.

Uimara wa safu hiyo ya ushambuliaji unatokana na uzito wa eneo la kiungo ambalo nalo limekuwa likionyesha ukomavu kwenye kutengeneza mashambulizi.

Washambuliaji kama Jephte Kitambala, Nassor Saadun, Abdul Sopu, winga Idd Seleman 'Nado', na nyuma yao akiwampo Feisal Salum 'Fei Toto', Yaya Zayd wameifanya Azam kucheza kwa utulivu na kuwamaliza kirahisi wapinzani.

Katika ulinzi, akisimama golini Zuber Foba au Issa Fofana, hakuna kinachoharibika, wakati walinzi wa kati Landry Zouzou na Yoro Diaby, huku pembeni akiwapo nahodha Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo, kumekuwa na utilivu wa hali ya juu.

Wakati Azam ikifuzu hatua ya makundi kwa kufunga jumla ya mabao 13 ikiifunga El Merreikh Bentiu jumla ya mabao 4-0, kisha KMKM ikachapwa 9-0, nyavu zake hazijaguswa kabisa.


FEI TOTO WA MOTO

Mchezo dhidi ya KMKM, Fei Toto alifanya makubwa, alitoa asisti nne za mabao peke yake, mbili kwa Kitambala na waliyofunga Nado na Sopu.

Fei alikuwa sehemu ya kutengeneza mabao hayo yaliyoiadhibu KMKM, akithibitisha thamani yake ndani ya matajiri hao wa Chamazi.

AZA 01

NDANI MTITI, NJE MTITI

Mechi hiyo ilikuwa ni bure kuishuhudia, hakukuwa na kiingilio kwa mashabiki na wakaitika kweli, ambapo iliwalazimu mpaka saa 9:00 alasiri mageti kufungwa baada ya watu kujaa huku nje kukiwa na watu zaidi ya wale waliokuwamo ndani. Kumbuka mechi ilianza saa 11:00 jioni.

Haikuwa rahisi kwa Askari wa Jeshi la Polisi, kudhibiti umati huo ambao uliitikia wito wa kufika kutazama historia ya Azam ikienda makundi.

AZA 06

MATAJIRI JUKWAANI

Pengine ilikuwa historia kwa mashabiki wa Azam, baada ya kuwaona watoto wa familia ya Bakhresa wakiwa uwanjani wakiwa sehemu ya umati huo.

Jukwaa kuu kulikuwa na Abubakar, Omar na Yusuf Bakhresa wote ni watoto wa Said Salim Bakhresa, wakiwa sehemu ya historia kushuhudia timu yao ikienda makundi.

AZA 05

MACHOZI YA POPAT

Baada ya mchezo huo kumalizika tukio lililoteka wengi ni pale Makamu wa Rais wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin Amin 'Popat', aliposhindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya timu hiyo kufuzu makundi.

Popat alijikuta akilia kutokana na Azam kukwama kwa muda mrefu kwenda makundi na wakati wote akawa anatulizwa na Rais wa Klabu hiyo, Nassoro Idrissa 'Father', na hata baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho.


MSIKIE FEI

Moja kati ya wachezaji bora ndani ya Azam ni Feisal Salum ambaye alishusha hat-trick ya asisti katika mechi hiyo na kuisaidia timu hiyo kuvuka kibingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei amesema, alikuwa akisaka rekodi ya timu sio yake, ndio maana alihakikisha anatengeneza nafasi za kutosha.

Amesema kuwa, anamshukuru Mungu kwamba amekuwa sehemu ya rekodi ya Azam kutinga makundi.

"Azam iko kwenye mikono salama ikiwa na kocha Florente Ibenge, uzoefu wake kimataifa utatufikisha mbali, hatuwezi kujisifu kwa ubora wetu kama wachezaji.

"Tumefuzu kwenda makundi baada muda mrefu, kwa sababu ya ubora wa kikosi lakini huwezi kuacha kusifu utendaji kazi wa kocha Ibenge ambao umeipeleka Azam kwenye historia mpya."