KMKM yapigwa 9-0, Azam FC ikitinga makundi CAF
Muktasari:
- Mechi iliyopigwa leo Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi jijini Dar, imeshinda mabao 7-0 dhidi ya KMKM, wakati mechi ya kwanza ilishinda kwa mabao 2-0, ikipigwa Uwanja wa New Amaan Complex, uliopo Zanzibar, wikiendi iliyopita.
AZAM FC inayonolewa na kocha Florent Ibengé, imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kishindo baada ya kuifunga KMKM kwa mabao 9-0 nyumbani na ugenini.
Katika mechi iliyopigwa leo Oktoba 24, 2025 Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, Dar es Salaam imeishinda mabao 7-0 KMKM wakati ile ya kwanza ilishinda kwa mabao 2-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar wafungaji wakiwa Jephte Kitambala na Pascal Msindo.
Leo, kipindi cha kwanza Azam ilitumia dakika sita kupata mabao matatu ukiacha kosakosa zilizokuwepo, kisha ikafunga bao la nne dakika ya 43.
Fei Toto alitoa pasi ya bao la kuongoza lililofungwa na Iddy Nado dakika 23 ambapo alishangilia na wenzake kisha akamkumbatia kocha Ibenge.
Dakika ya 26 Nado aliyetoa pasi ya bao la pili lililofungwa na Jephte Kitambala na dakika ya 29 Fei Toto alitoa pasi kwa Kitambala akiifungia Azam bao la tatu, hivyo mchezaji huyo kafunga mabao mawili ndani ya dakika tatu na kutoa asisti moja.
Baada ya Kitambala kufunga bao la pili, aliushika mguu wa Fei Toto akiwa amepiga goti, kisha kuufuta kuonyesha namna anavyomkubali.
Dakika ya 43 Nado alifunga bao la nne, mpira ulianza kwa Abdul Suleiman 'Sopu' aliyempa mpira Kitambala akatoa pasi ya mwisho ya bao, hivyo dakika 45 za kipindi cha kwanza Azam FC ilikuwa inaongoza kwa mabao 4-0.
KIPINDI CHA PILI
Dakika ya 47 Azam ilipata bao la tano lililofungwa kwa kichwa na Pascal Msindo ilhali dakika ya 53 Abdul Suleiman 'Sopu' alifunga bao la sita akipokea pasi ya Fei Toto. Pia Sopu alifunga bao lingine dakika 55 likiwa la saba kwa Azam pasi ya Fei Toto.
MASHABIKI
Vaibu la mashabiki lilikuwa juu, huku wengine wakionekana na bango lililokuwa linamhusu kocha wa timu hiyo lilioandikwa 'In Ibenge We Trust' wakimaanisha kumwamini kocha huyo na bango lingine liliandikwa 'Welcome Ibenge tunataka ubingwa na makundi, asante Ibenge'.
Kikosi cha Azam: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Zouzou Landry, Yahya Zayd, Abdul Suleiman 'Sopu', Himid Mao, Jephte Kitambala, Feisal Salum 'Fei Toto' na Iddy Nado.
Kikosi cha KMKM: Adam Rihaji, Ahmed Isahaka, Arafat Farid, Moh'd Ali, FirdausSeif, Imran Mohamed, Nasir Sheha, Jasper Yaw, Mzee Hassan, Ali Hassan na Haji Makame.
Azam ikiwa imetangulia kuingia makundi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hivi sasa inasubiriwa Yanga inayocheza kesho Jumapili dhidi ya Silver Strikers, Simba dhidi ya Nsingizini Hotspurs hizo zitachezea Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati Singida Black Stars dhidi Flambeau du Centre mchezo utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.